24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 30, 2023

Contact us: [email protected]

Kichina kufundishwa sekondari

akwilapoNA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Leonard Akwilapo, amezindua mpango maalumu wa kufundisha somo la Kichina katika shule za sekondari.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Akwilapo alisema mpango huo umeanzishwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China, ambapo taasisi ya Confucius Philosophy itatoa mafunzo hayo.

“Tayari tumeanza kutoa elimu hiyo kwa kidato cha kwanza na cha tano ambapo kwa hapa Dar es Salaam tumeanza na sekondari ya Zanaki na Benjamin Mkapa, Mkoa wa Morogoro ni Kilakala na  Morogoro Sekondari na mkoani Dodoma ni Uwanja wa Ndege na Dodoma Sekondari,” alisema Akwilapo.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu imekuja wakati ambao mwanafunzi raia wa China aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Feza ya Jijini Dar es Salaam, Congcong Wang, akiwa ameacha gumzo kutokana na kushika nafasi ya kwanza kwa kupata alama B katika lugha ya Kiswahili.

Alisema ni fursa sasa kwa wanafunzi na Watanzania kujifunza lugha hii itakayowezesha kuwasiliana na kufanya biashara na Wachina.

Aliongeza kuwa tayari wamepokea walimu wa kujitolea 12 kutoka China ambao watagawanywa katika shule sita ambazo ni za majaribio.

“Tumeanza kufundisha walimu wazawa watakaokuwa wakifundisha lugha hiyo shuleni ambapo masomo hayo yameanza katika vyuo vikuu vya Dodoma, Dar es Salaam na chuo cha waislamu cha Morogoro,” alisema Akwilapo.

Akwilapo alisema kutokana na nchi hizo mbili kubadilishana wanafunzi, mpaka sasa kuna wanafunzi wengi wa hapa nchini wanaosoma China, lakini changamoto kubwa ilikuwa lugha.

Naye Mkurugenzi wa Ubalozi wa China nchini, Gao Wei, alisema kuna umuhimu wa Watanzania kujifunza lugha hiyo kutokana na ukaribu na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,282FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles