32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 1, 2023

Contact us: [email protected]

Ukawa waweka msimamo ushindi meya Dar leo

salum mwalimuNa Waandishi Wetu

WAKATI uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ukitarajiwa kufanyika leo, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeweka msimamo wa ushindi, huku ukikitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutotumia vyombo vya dola kuuvuruga.

Umoja huo unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD, ulifanikiwa kupata mameya wa manispaa za Kinondoni na Ilala, huku CCM wakipata meya wa Manispaa ya Temeke.

Awali katika chaguzi hizo, CCM, yenye idadi ndogo ya madiwani, ililaumiwa kwa kutumia wabunge wa viti maalumu kutoka Zanzibar na mikoa mingine na wabunge wa kuteuliwa ili kuongeza idadi ya wapiga kura, jambo lililofanya uchaguzi wa meya wa jiji kuahirishwa mara kadhaa na kukwamisha shughuli nyingi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisema idadi ya wapiga kura inawabeba kushinda uchaguzi huo.

“Tunakwenda kesho kupiga kura tukiwa na wapiga kura halali 58 wa Kinondoni na kati ya hao, vyama vya Ukawa kwa maana ya Chadema na CUF ni 38 na CCM 20. Wajumbe 54 kutoka Ilala, kati yao 31 ni wa Ukawa na 23 ni wa CCM. Wapiga kura kutoka Manispaa ya Temeke wakiwa 49, Ukawa wakiwa 18 na CCM 21. Jumla ya wajumbe ni 161,” alisema Mwalimu.

Akizungumzia msuguano uliosababisha uchaguzi huo kucheleweshwa, Mwalimu alisema ulisababishwa na CCM na mamlaka zinazosimamia uchaguzi huo.

Hata hivyo, alisema kutokana na vikao vya usuluhishi vilivyohusisha vyama vya siasa vyenye madiwani, yaani Chadema, CUF na CCM, majina maalumu ya wapiga kura yameshapitishwa.

“Mpaka tumefikia hapa, tayari vimeshafanyika vikao vya kupitisha na kuthibitisha majina ya wapiga kura. Wamekubaliana kuwa walioshiriki kupiga kura kumchagua Meya wa Temeke, Ilala na Meya wa Kinondoni ndio hao watakaoshiriki kumchagua meya wa Dar es Salaam,” alisema Mwalimu na kuongeza:

“Jambo lilikuwa wazi siku nyingi, lakini CCM kilikuwa kikifanya jitihada za kuvuruga kwa kuleta mamluki. Tumeona wakileta wabunge kutoka mikoa mingine na kutoka Zanzibar.”

Aliilaumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akisema ilijaribu kuvuruga uchaguzi huo kwa kisingizio cha kuomba taarifa kutoka mamlaka nyingine.

“Kesho tuna taarifa kuwa watu hawa baada ya kushindwa njama za nje wanakusudia kuharibu uchaguzi ndani ya ukumbi kwa ama kufanya vurugu, kuleta polisi wengi, kusingizia kuna vurugu, kusingizia huyu hivi huyu vile. Wakamate madiwani wetu na wabunge wawatoe nje,” alidai Mwalimu na kuongeza:

“Hilo likishindikana wanakusudia kutangaza matokeo kwa nguvu yatakayotoa mshindi kwa CCM. Nadhani wote tunakumbuka kilichotokea Tanga.”

Alisema uchaguzi huo siyo vita wala vurugu na unaongozwa na taratibu, kanuni na sheria inayoonyesha nani anafaa kugombea na nani anafaa kupiga kura.

“Hatutarajii kuona polisi kesho. Ni wajumbe 161 wanapiga kura na mshindi atatangazwa biashara imekwisha. Kwa hiyo hatutarajii kuona magari ya washawasha, mabomu ya machozi wala rundo la askari. Kesho ni uchaguzi wa meya,” alisema.

Amewataka watu wasiokuwepo kwenye idadi ya 58 ya Kinondoni, 49 wa Temeke na 54 wa Ilala kutojitokeza kwenye ukumbi huo ili kuepusha vurugu.

“Uchaguzi ni namba na namba zimejionyesha zinatubeba, tunategemea Isaya Charles Mwita kesho atatangazwa kuwa meya wa Dar es Salaam na atatangazwa ili awatumikie wananchi,” alisema.

Kuhusu uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilombero, Mwalimu alisema utata wake unafanana na wa Dar es Salaam na kuzitaka mamlaka kutafuta suluhu ili uchaguzi huo ufanyike mapema.

“Tukimaliza figisufigisu ya Dar es Salaam, tunaelekea Kilombero, eti zinatafutwa tafsiri za nani mpiga kura halali na nani siyo. Kama lilivyomalizwa Dar es Salaam, wapiga kura halali wanajulikana. Kilombero nako tunataka uchaguzi uitishwe chini ya wapiga kura halali,” alisema Mwalimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles