27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waitaliano kuifumua Manzese

william lukuviNa Agatha Charles

ENEO la Manzese lililopo jijini Dar es Salaam linatarajiwa kufumuliwa na kujengwa majengo ya kisasa kutokana na ramani ya mipango miji inayofanywa na wataalamu.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipogawa ramani 104 kati ya 329 kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ya Dar es Salaam ili kumaliza migogoro ya ardhi.

Lukuvi alisema hadi kufikia Julai, mwaka huu, Dar es Salaam itakuwa na mipango miji yake ambayo kazi hiyo inafanywa na wataalamu kutoka nchini Italia.

“Dar imejaa lakini lazima tujenge, Manzese ihame lazima ije Manzese mpya, iende juu. Hatufukuzi watu pale lakini watatafutiwa namna,” alisema Lukuvi.

Alilitaja eneo jingine litakalojengwa nyumba za kisasa, hoteli pamoja na kumbi za mikutano ni kando ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

“Eneo hilo lazima liwe transformed (libadilike) ili kuendana na uwanja wa ndege wa kisasa ambao unajengwa. Hatuna haja ya watu wamekuja kwa ajili ya mikutano kuja hadi katikati ya mji,” alisema Lukuvi.

Alitaja miji mingine ambayo inatengenezewa mipango miji ni Arusha ambayo itakwenda hadi Meru na Mwanza ambako wataalamu wanaohusika kuutengeneza wanatoka nchini Singapore.

“Hao Singapore ni watu wenye uwezo mkubwa, master plan ya Mwanza na Arusha tumeshawalipa fedha nyingi za wizara hivyo itakuwa tayari. Awali ya Dar ilivyoletwa niliikataa kwa kuwa ilikuwa na upungufu na haikuwa na basement wala data za sasa,” alisema Lukuvi.

Alisema ramani hizo zitawasaidia wenyeviti hao wa vijiji kujua ni yapi maeneo ya wazi na wapi panapaswa kujengwa nini pindi watendaji wa miji wanapokwenda kwa lengo la kufanya kazi.

“Hii ya kuvunja vunja nyumba za masikini kama mwenyekiti wa mtaa hana ramani anashindwa kumtetea mnyonge anayebomolewa. Leo hii mama masikini akivamiwa ardhi yake mwenyekiti anaweza kuingilia, leo hii wenyeviti 104 tunawapa ramani,” alisema Lukuvi.

Alisema hilo litasaidia kuwaondoa wote waliojenga katika maeneo ya wazi pamoja na maeneo ya huduma za kijamii.

Lukuvi alisema kuna watu waliuziwa viwanja tofauti na matumizi yanayofanyika ambapo ni lazima virudishwe.

“Nitaanza na Mbezi eneo ninakoishi, eneo la Shule ya Msingi ya Kata watu wamevamia, jamani mkiona uvunjifu toeni taarifa wilayani kuweni wa kwanza kuwa askari.

“Mfano kati ya majengo 48 yaliyobomolewa Kinondoni, 12 yalimaliziwa na matapeli, kuna waliokuwa wameanza msingi matapeli wakaja kumalizia hao wameshindwa hata kutufikisha mahakamani, lengo letu ni kuzuia uendelezaji holela wa majengo,” alisema Lukuvi.

Alisema Dar es Salaam haina haja ya kuwa na mabwana shamba au nyuki badala yake waongezwe wataalamu wa mipango miji.

Katika hatua nyingine, alisema awamu ya pili itafanya urasimishaji na nyumba zitakazokutwa zimejengwa maeneo mazuri hazitabomolewa.

“Mtaa ulio tayari kurasimishwa watuambie. Kwa uzembe wetu Serikali au kuchelewa, wananchi walituwahi kujenga sasa kama wako pazuri wasibomolewe, nyumba za masikini zitakazorasimishwa zipewe namba na hati,” alisema Lukuvi.

Aliwataka viongozi wa ardhi kwenda maeneo ya matukio wakiwa tayari wametoa taarifa kwa wenyeviti wa mitaa.

Pia aliwataka watendaji waliohudhuria hapo kumfikishia salamu mtu aliyemtaja kwa jina la Mahinga kuwa ndiye kinara wa kutoa vibali vya ujenzi hadi barabarani katika eneo la Kibaha.

Alisema mipango miji itaondoa uvunjifu wa maadili kwa kuweka shughuli moja katika eneo husika.

“Watu wanapiga muziki hadi asubuhi huku grocery wanauza kitimoto hatua mbili ya msikiti, eneo jingine wanauza pombe hatua mbili kanisa. Zipo nyingi lakini zinapaswa kuendeshwa kwa maadili, lazima kurudisha nidhamu, mwenyekiti aanze kurudisha nidhamu,” alisema Lukuvi.

Alisema watu wanaokuja kuomba kujenga wasiangaliwe sura bali waambiwe utaratibu ulivyo na kama ni eneo la kujenga ghorofa moja lijengwe hivyo na si vinginevyo.

“Nyie msivunje lakini mtoe taarifa hata kama ni ujenzi wa choo ambao hauna kibali toeni taarifa lengo ni kuwapa silaha ili tuijenge Dar es Salaam ambayo ndio kioo cha nchi. Jiji limejaa lakini hadi Julai utaona mabadiliko hakutakuwa na uvamizi,” alisema Lukuvi.

Aliwataka wenyeviti hao ambao wana matatizo katika maeneo yao na walikwishatoa taarifa wilayani lakini hazifanyiwi kazi kwenda moja kwa moja ofisini kwake au kutuma ujumbe mfupi kupitia namba ya simu aliyowapatia.

Alisema ili kuboresha waliitoa Pwani katika Kanda ya Dar es Salaam ambako kwa sasa wana uwezo wa kumpatia mtu hati ya nyumba ndani ya mwezi mmoja.

Alisema hadi sasa kuna hati 3,000 za nyumba ambazo wananchi hawajakwenda kuzichukua huku wizara hiyo ikijitahidi kuboresha ili kuingia katika mfumo wa elektroniki ambako hati inaweza kupatikana kwa siku moja.

Awali, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Mikoa, Profesa John Lupala, alisema michoro ya mitaa 104 ilikamilika kati ya mitaa 329 huku iliyobaki ikisubiri urasimishaji.

Alisema katika michoro hiyo, Wilaya ya Kinondoni ilipata 33, Temeke 10 na Ilala 61.

Profesa Lupala alisema katika sensa iliyofanyika ilionyesha Kinondoni ina kata 35 na mitaa 113, Temeke kata 36 na mitaa 105 huku Ilala ikiwa na kata 35 na mitaa 111.

“Kwa maeneo ambayo hayana utata, Machi 30 itakuwa tayari lakini yenye urasimishwaji Juni yatakamilika,” alisema Profesa Lupala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles