31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Kibano madini chaanza kulipa India

Na Shermarx Ngahemera

WIKI iliyopita Mwenyekiti wa Tume ya madini Tanzania Profesa Idris Kikula aliteta  jijini Dodoma na balozi wa India kuhusu masuala mengi lakini wachunguzi wa mambo wanadai  mambo mengine kuwa ilikuwa  ni matokeo ya kibano cha madini kinachofanywa na Tanzania.

Madai hayo yana mantiki kwani Tanzania imeziba mianya ya utoroshaji rasilimali zake za madini kwa kutunga sheria mbili mwaka jana 2017,  ambazo zinaanza kutoa athari njema kwa kuvuta uwekezaji.

Wachunguzi hao wanadai ni muda mrefu sana India haijawahi kuzungumzia masuala ya madini ingawa ndio mtumiaji mkuu wa madini ya vito ya Tanzania ikiwamo dhahabu na tanzanite ambayo inafanya sababu ya nchi hiyo kutaka kujipanga vilivyo na hivyo kuona umuhimu wa kwenda Dodoma na kuweka mikakati ya baadae ya nchi hizi mbili ikiwemo uwekezaji mwafaka kwenye sekta ya madini.

Taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari ni kuwa Profesa Idris Kikula, amekutana na Balozi wa India nchini, Sandeep Arya, jijini Dodoma kwa lengo la Balozi huyo kujitambulisha pamoja na kufahamu majukumu ya tume hiyo muhimu kwa sekta ya madini nchini.

Ni ukweli usiopingika kuwa sio kawaida kwa balozi kwenda kujitambulisha kwenye tume kwani hakuna shuguli ya moja kwa moja kati yao.  Na vile vile ni muhimu kutambua kwamba diplomasia inayotawala duniani siku hizi ni ile ya uchumi na India ni nchi ya tatu kwa ukubwa wa kibiashara na Tanzania baada ya Ujerumani na China.

Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Kikula, alieleza kuwa Tume imejipanga kusimamia Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya madini nchini na hiyo maana yake ni uwekezaji na uendeshaji wa biashara hiyo nchini.

Takwimu zilizopo zinaonesha India inauza sana tanzanite duniani inayodaiwa kuwa ya magendo kwani daftari za serikali zinaonesha takwimu kinyume chake cha mauzo ingawa Tanzania ni nchi pekee chanzo cha madini hayo.

Pili Tanzania imepiga marufuku kusafirisha nje tanzanite ghafi ya ukubwa na uzito fulani mdogo kutokana kukosa mafundi wa kukata nchini na hivyo kuleta zahama kwa viwanda vya Jaipur jimbo la Rajastahan, India ya kaskazini Magharibi,  ambako zaidi ya watu laki tatu wameajiriwa kukata vito kutoka Tanzania na haswa tanzanite.

Zuio hilo ni ngumu kumeza kwa India na hivyo ni mkakati sahihi kwao kutazama namna ya kuendelea kufanya biashara katika mazingira mapya ya uwepo wa Tume na udhibiti ulioimarishwa.

Ujenzi wa uzio wa ukuta kule Mirerani kuzuia utoroshaji na uwepo wa tanzanite ya magendo imefanya hali kuwa sio njema kwa ulanguzi wa madini hayo na hivyo kuhitaji mtazamo mpya kulinda maslahi ya kila nchi.

Isitoshe India ni mnunuzi mkuu wa dhahabu duniani kwa matumizi ya vito na kwenye vifaa vya Tehama na utafiti na hivyo Tanzania ni muhimu kwa upatikanaji dhahabu na India ni mwekezaji mpya anayetaka kushiriki uwekezaji huo haswa ikifahamika kuwa ilikuwa inashugulikia kusafisha makinikia kutoka Tanzania ambayo yamezuiwa kwenye makontena bandarini.

Isitoshe uchumi wa India unakua haraka na kutokana na Marekani kuyumbisha uchumi wa dunia kwa tozo na fedha ya Dola kuwa ghali ni vema India ikanunua akiba yake ya hazina ya dhahabu kutoka Tanzania. Chanzo cha Afrika Kusini karibuni migodi mingi itafungwa kwani dhahabu  huchimbwa kina zaidi ya kilomita 10 chini ya ardhi na kuifanya iwe ghali zaidi ya bei ya mauzo yake na hivyo kukosa mvuto kibiashara.

Sheria mpya chungu

Prof Kikula alisema Sheria ya Madini ina matakwa mapya  mahsusi yaliyoainishwa kama vile  kuweko na maudhui ya ndani  (local content), utoaji wa huduma kwa jamii kwenye shughuli za uchimbaji madini (corporate social responsibility) au CSR na mhusika kufanya kiapo cha uadilifu kwenye shughuli za uchimbaji madini (integrity pledge). Maendelezo hayo hayakuweko hapo zamani na hivyo balozi  Arya yuko sahihi kwenda kupata taarifa kutoka kwa Tume ili kupeleka taarifa sahihi kwa wawekezaji wa India.

Prof Kikula alisema Tume imejipanga pia kutoa leseni haraka iwezekanavyo na kuwasaidia wachimbaji wadogo.

Akizungumzia namna Tume ya Madini ilivyojipanga katika kutatua changamoto ya migogoro kwenye Madini nchini, alisema tume hiyo inaandaa mpango wa kutatua migogoro kuanzia katika ngazi ya kijiji, kata, wilaya na taifa kwa ujumla.

“Sheria imetoa mwanya kwa mamlaka mbalimbali kutatua migogoro na tume ikiwa ngazi ya mwisho ili kurahisisha ushughulikiaji mambo na migogoro.”

Alisema migogoro mingi inatatulika katika mamlaka za vijiji, kata na wilaya.

Lengo ni kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na Tume  kwa kushirikiana na  Wizara ya Madini wamejipanga kuwa na wataalamu wenye weledi kwenye usimamizi wa sekta ya madini na kusisitiza umuhimu wa mafunzo.

“Mafunzo kwa wataalamu  tunayapa kipaumbele sana,” alisema Mwenyekiti waTume, na alimwomba Balozi kuendelea kuitangaza sekta ya madini nchini mwake. Alisisitiza kuwa Tanzania ina maeneo mengi yenye madini yaliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Naye Balozi  Arya, alisema India ipo  tayari kushirikiana na Tume ya Madini hususani katika kutoa ufadhili wa masomo kwa watumishi wa Tume.

Alisema India imekuwa ikitoa mafunzo ya muda mrefu  katika ngazi za shahada za uzamili na za uzamivu katika vyuo vyake bora na kusisitiza kuwa itaendelea na mpango wake huo.

Teknolojia ni uwanja mojawapo India inajulikana kuwa ni mahiri kwa kila namna ikiwamo madini na mafuta ambapo Tanzania ina mengi ya kujifunza toka huko.

Kampuni moja ya India imewekeza kwenye utafutaji mafuta ya petroli na gesi, kampuni ya Swala Oil.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles