25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Kiapo cha Chadema champeleka Mdee mahabusu

NA AGATHA CHARLES

MBUNGE wa Kawe na MwenyekitiwaBaraza la Wanawake Chadema Taifa (Bawacha), Halima Mdee jana aliitwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa polisi.

Taarifa za kuhojiwa Mdee ambazo zilithibitishwa na chama chake kabla ya baadae kuthibitishwa na Jeshi la Polisi zilieleza kuwa aliitwa na Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kituo cha Polisi Oysterbay kwa kosa la kufanya mkutano usio na kibali jimboni kwake.

Kuhojiwa kwa Mdee kumekuja ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu Chadema itangaze azma yake ya kuandaa ratiba ya kufanya mikutano mchana kweupe.

Kutokana na hatua hiyo, Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake Ahmed Msangi, liliitaka Chadema kufuata utaratibu.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alithibitisha kuhojiwa kwa Mdee.

Kamanda Mambosasa alisema Jeshi la Polisi lilikuwa likimtafuta Mdee tangu juzi kwa kosa la kufanya mkutano usio na kibali.

“Aliomba kibali akaelekezwa kwamba asifanye mkutano kwa sababu kulikuwa hakuna askari wa kulinda mikutano yake. Yeye akakaidi akaendelea,” alisema Kamanda Mambosasa.

Alipohojiwa iwapo Mdee alikamatwa au aliitikia wito wa Jeshi hilo kama ambavyo aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, Kamanda Mambosasa alisema Mwenyekiti huyo wa wanawake wa Chadema alikuwa akitafutwa na si kuitwa.

“Alikuwa anatafutwa kama amejipeleka sijui, lakini alikuwa anatafutwa sio kuitwa,” alisema Kamanda Mambosasa.

Alipohojiwa iwapo kuna uwezekano wa Mdee kuachiwa kwa siku ya jana, Kamanda Mambosasa alijibu kuwa bado alikuwa anashikiliwa.

“Kwahiyo ndio hivyo bado ameshikiliwa,” alisema Kamanda Mambosasa.

Kwa upande wa Chadema, taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene ilieleza hadi saa 11:00 jioni Mdee alikuwa hajapatiwa dhamana.

Makene alisema Mdee aliitikia wito kutoka Ofisi ya RCO wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni na kufika Kituo cha Polisi Oysterbay kwa ajili ya mahojiano.

Alisema Mdee alihojiwa kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi kwenye moja ya mikutano yake ya hadhara aliyofanya Jimbo la Kawe, ikiwa ni mwendelezo wa ratiba ya ziara za kuwatembelea, kuwasikiliza na kuwapatia mrejesho wapiga kura wake jimboni humo. 

Makene alisema mbali na kumshikilia Mdee, polisi wameshikilia simu zake mbili na pia wamewataarifu wanasheria wake kuwa watakwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake wakati wowote kuanzia jana jioni. 

“Chama kimeshangazwa na hatua hiyo ya kushikilia simu na kutaka kwenda kupekua nyumbani kwa mtuhumiwa anayetuhumiwa kufanya uchochezi kwenye mkutano wa hadhara, au ni mwendelezo ule ule kama ilivyokuwa kwa Mbunge Lissu kwenda kupimwa mkojo wakati anatuhumiwa kwa uchochezi?,” alihoji Makene. 

Taarifa hiyo ya Chadema ilieleza kuwa baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kumhoji, kumshikilia na kumnyima dhamana Mdee, chama kiliwaagiza wanasheria wake kuchukua hatua zaidi za kisheria haraka.

Makene katika taarifa hiyo alisema moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kuandaa na kuwasilisha maombi Mahakama Kuu siku ya kesho.

“Kuandaa na kuwasilisha maombi ya ‘habeas corpus’ Mahakama Kuu ifikapo Jumatatu (kesho), kuiomba Mahakama Kuu itoe amri ya kuwaita na kuwahoji polisi kwa kumshikilia Mdee na kumnyima dhamana,” alieleza Makene kupitia taarifa hiyo.

Makene alieleza kuwa haki ya kupata dhamana iko kwa mujibu wa sheria zetu na haitolewi kwa utashi wa mtu wala mamlaka yoyote.

Makene alisema Chadema kinalaani na kukemea vikali kitendo hicho cha polisi ambacho ni ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu.

“Chama kinachukulia tukio hilo la leo (jana) kuwa ni kuendelea kuandamwa wawakilishi wa Chadema wenye nafasi za kiserikali, wakiwemo wenyeviti wa Serikali za Mitaa, madiwani na wabunge, wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao, likiwa limetokea siku chache baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kuhojiwa na kushikiliwa na polisi kwa kutimiza wajibu wake huku jeshi hilo likiwa halijawahi kutoa taarifa iwapo limewahi kuwaita, kuwahoji, kuwashikilia na kuwafikisha mahakamani viongozi wa CCM wakiwemo wabunge wa chama hicho wanaotoa kauli za kibaguzi, chuki na hata kumtishia maisha Mwanasheria Mkuu wa Chama, Tundu Lissu,” alieleza Makene.

Kukamatwa kwa Mdee kumekuja ikiwa ni hivi karibuni tu chama hicho kupitia Katibu Mkuu wake kutangaza kuwa kinaandaa ratiba ya kuanza kwa mikutano ya hadhara mchana kweupe na kujitita katika sera zao pasipo kupambana na mtu.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles