27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Vituko vya ‘house girls’ vinavyowapasua vichwa wenye nyumba

Na Grace Shitundu – Dar es salaam

WASICHANA wa kazi za ndani maarufu  ‘house girls’, sasa wanaonekana kupasua vichwa vya waajiriwa wengi kutokana na vituko na mambo mbalimbali wanayofanya.

MTANZANIA Jumapili limelazimika kufanya ripoti maalumu kutokana na kupokea malalamiko mengi kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu wasichana wa kazi.

Katika ripoti hii maalumu, ambayo itachapishwa mfululizo kila Jumapili, gazeti hili limefanikiwa kukutana na kuzungumza na waajiri, wasichana wa  kazi, walezi, wazazi wao na baadae mamlaka husika.

Waajiri wengi wanasema pamoja na upatikanaji wa wasaidizi hao kuwa mgumu kwa sababu ya elimu bure pamoja na kuolewa mapema, lakini wale wanaowapata hujikuta wakiishia katika wakati mgumu.

IMANI NDOGO

Agnes Chacha ni mama wa watoto wawili kwa uzoefu wake wa kukaa na wasaidizi hao kwa takribani miaka kumi anasema wengi siku hizi ni waongo, wana kiburi, hawapendi kusemwa.

“Unaweza ukamuachia mtoto na ukamwambia ahakikishe anakula na kuwa msafi wakati wote lakini hafanyi.

“Kwa uzoefu wangu jambo jingine sumu kwao ni kumsema, hawataki kusemwa ( kuambiwa), ukimwambia ananuna,  anaona unamnyanyasa , sasa unajiuliza mbona sisi tulikuwa tukikosa tunasemwa na wazazi wetu au wakubwa wetu na maisha yanaendelea, kuna wengine wanaweza kusema hawapewi chakula kumbe ni uongo.

“Mwingine unaweza ukawa umemuwekea hela yake benki ikafika shilingi 500,000, basi anajiona ana hela nyingi anaanza kiburi na mwisho anaondoka”alisema.

Anasema mwanzoni alijiona labda yeye ana tatizo lakini vituko alivyokuwa akivishuhudia ndivyo vilivyokuwa vikitokea  kwa rafiki zake wa karibu.

“Huko nyuma niliwahi kupata mdada anapenda sana TV na kukodisha CD za ‘series’ hadi anasahau watoto, unaweza ukamuuliza je mtoto amekunywa uji, akakujibu ndio lakini unaukuta kaumwaga, saa zote yeye ni TV,”.

Woinde Nkya anasema pamoja na kwamba wapo wanaowanyanyasa wasaidizi hao lakini pia wapo wengine wanaotumia kivuli  hicho kuficha mabaya yao.

“Msichana anaweza akampigia mama yake kuwa hajanywa hata chai wakati huo ndani kuna kila kitu, watu wengi hivi sasa hawanyanyasi ni wao wenyewe wasichana na mambo yao na tabia zao za uongo,”.

Joyce Lukosi anasema naye amekumbana na visa vingi vya wasichana hasa wale wanaotumia msamiati wa kunyanyaswa.

“Yupo msichana mmoja nililetewa na mdogo wangu kutoka Gairo, alilala usiku mmoja tu akatoroka akasema eti nimempiga sana kisa kavunja glasi wakati tukio hilo halikutokea kabisa,”.

 “Wengine wanakuwa sio wasafi ukimwambia akaoge anaona unamnyanyasa na kuna mwingine alikuwa na miaka 17 tu nilipewa nyumbani alikaa mwaka  mmoja tu akatoroka akaenda kuuza bar nilihakikisha ninamrudisha kwa msaada wa polisi,”.

Alisema kuna mwingine badala ya kulea watoto wako analea watoto wa mwenye nyumba.

USHIRIKINA

Katika mahojiano  hayo, waajiri wengi pia wameonekana kulalamikia suala la ushirikina kwa wasichana wa kazi.

Doris Justine anasimulia;

“Disemba nilipata msichana mdogo tu na mimi kwa imani yangu nikaenda naye kwenye maombi lakini baada ya siku chache mdogo wangu aliyekuja kunitembelea akanieleza kwamba mchunguze msichana wako ana simu, wakati huo mimi nilikuwa najipanga kumnunulia simu ili irahisishe mawasiliano na nyumbani nikiwa kazini nilipomchunguza nikagundua si simu tu ana hizirizi za kutosha.

“Ilibidi nimwite mtu aliyeniagizia tulipombana akasema alipelekwa kwa mganga na shangazi yake na hiyo hirizi ilikuwa ni kwa ajili ya kumlinda na alipewa masharti ya awe anaivaa kwenye nguo ya ndani.

Anasema baadae alipowasiliana na mama yake aligundua aliyempeleka kwa mganga si shangazi yake bali ni mama yake na alipomtaka waichome hiyo hirizi alikubali lakini baadae ikazuka hali ya sintofahamu.

“Nilimweleza mimi siwezi ishi na msichana ambaye ana hirizi hivyo akaichoma, siku ilipochomwa mama yake akaanza kusumbua vibaya mno anataka mtoto wake arudi, aliondoka saa 11:00 jioni jiulize kuna gari muda huo la kwenda mkoani hapa Dar es saalam? Lakini aliondoka.

“Alipoondoka tu niliumwa kitu ambacho siwezi kusimulia nilikwenda hospitali na kupimwa kila kitu lakini wapi niliishia kupona kwenye maombi”.

Steven Ryoba yeye anasema mwanzoni alidhani pengine mkewe ni mkorofi kumbe sivyo.

“kuna wakati tulipata msichana anafunga hirizi mkononi , tulipomuuliza alisema hiyo ni dawa ambayo mtu akitoka mbali na nyumbani ni lazima avalishwe siku hiyo hiyo tulimfungashia virago vyake akarudi kwao.

“Mwingine ilikuwa kila tulipokuwa tukianza kusali yeye analala usingizi mzito kabisa hiyo kuna baadhi huwa wanakuja na ushirikina,”.

WENGI HAWATAMANI

Kama ilivyo kwa wengi waliozungumza na gazeti hili, Clara Msuya ambaye ni mama wa watoto watatu anasema hatamani kuwa na msaidizi tena.

Anasema kilichosababisha ni msichana kumchoma kwa pasi mgongoni mtoto wake mdogo na kisha kutoroka.

“Hadi leo nikikumbuka lile tukio nahisi tumbo la uzazi linanikata, na nimekataa kutafuta msichana tena, nikienda kazini na watoto wanakwenda shule, tunafunga milango tunakutana jioni,”.

NJIA YA KUJA MJINI

Waajiri wengi wanaona wasaidizi wengi wanapokuja kufanya kazi huwa na malengo tofauti.

“Kuna msichana mwingine nilimleta, kufika hapa kumbe nia yake ilikuwa ni kuja kukutana na mwanaume wake nilimkamata anaongea na simu ya kupanga mipango ya kutorokea huko akiwa ndio kwanza ana siku moja tu

“Sikumruhusu amalize hata siku tatu kwangu nilirudisha kwao na kumwambia huyo mwanaume wake atamtumia hela ya kuja Dar,” alisema.

WENGI HAWAKUMBUKI IDADI

MTANZANIA Jumapili limebaini kuwa waajiri wengi hawakumbuki idadi ya wasaidizi waliokaa nao tofauti na waajiri wa zamani.

Zainabu Athumani alipoulizwa amebadilisha wasichana wa kazi wangapi alisema hakumbuki.

Lulu Mwakalindile yeye alisema ni kati ya watano hadi nane kwa muda wa mwaka mmoja.

Mama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Brian alisema yeye alianza kuwa na wadada wa kazi alipojifungua mtoto wake ambaye kwa sasa ana umri wa mwaka mmoja na miezi tisa na tayari amebadilisha wadada wapatao saba.

 Anasema sasa hivi ukibahatika kukaa na msichana mwaka mmoja ni bahati.

Upatikanaji mgumu

Katika mahojiano hayo, waajiri wengi pia wamelalamikia upatikanaji wa wasaidizi hao  kiasi cha kuwachukua miezi mitatu hata zaidi.

“Yaani sasa unaamua kugawa muda mdogo wa kazi na watoto, inafika wakati unawakuwa na wasiwasi wa kupoteza hata ajira, sasa hivi wasichana wengi wako shuleni na ambao hawapo shuleni wanaolewa mapema”. Anasema Clara.

Kutokana na hilo Frola Mbuya yeye anasema ni wakati wa nchi kujipanga na kuanzisha mafunzo yatakayosaidia sasa kupata wataalamu wa kulea watoto iwe mashuleni au majumbani.

“Naona kwa uchache wameanza zipo sehemu sasa hivi unapeleka mtoto asubuhi unampitia jioni, lakini japo ni gharama lakini tunaelekea huko, tutakwenda kusoma kozi za “Babies and Nursing’ wenzetu huko kazi hizi zinawalipa,

“Japo ni jambo gumu, kutokana na hali ya vipato vyetu, lakini kwa gharama, kero na hata hatari tunazoingia sasa za kubadilisha wasichana mara kwa mara tena wasio na ujuzi wa malezi ambao ndio msingi wa hayo yote wakati mwingine huwa nasema wacha tuelekee huko,” alisema.

ITAENDELEA JUMAPILI IJAYO

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles