24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

KIAMA CHA LESENI KWA MADEREVA

Na LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM


  • Leseni 225 zazuiwa baada ya wahusika kushindwa kuonesha vyeti vya vyuo walivyosoma.

NI kiama. Ndivyo unaweza kusema baada ya Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabara, kutangaza msako mkali wa madereva wanaomiliki leseni bila kusomea.

Sambamba na hatua hiyo, jeshi hilo limesema ukaguzi lililoufanya kwa siku 12 ulihusisha vyombo vya moto  81,533 ambapo madereva 327 walikamatwa kwa makosa mbalimbali, yakiwamo ya leseni na uendeshaji wa magari mabovu na kwamba tayari wamekwishafikishwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu alisema katika ukaguzi zaidi ya madereva 1,800 walikutwa na leseni zilizokwisha muda wake huku wengine 878 wakibainika kutumia leseni za madaraja yasiyostahiki.

Kamanda Musilimu alisema wamiliki 25 wa magari wamefikishwa mahakamani kwa kuruhusu magari mabovu kuingizwa barabarani.

Alisema jumla ya leseni zilizokaguliwa ni 73,904, kati ya hizo leseni 225 zimezuiwa baada ya madereva wake kushindwa kuonesha vyeti vinavyoonesha vyuo walivyosoma.

Kamanda Musilimu alisema madereva waliofikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yanayohusu leseni ni 173, na waliokamatwa wakiendesha magari mabovu ni 154.

“Mfano dereva mwenye leseni ya daraja E anakutwa anaendesha gari la kubeba abiria wakati dereva anayepaswa kuendesha gari la abiria anapaswa kuwa na leseni daraja C.

“Madereva wote ambao wamebainika kuwa na leseni bila vyeti vya shule walikosoma. Leseni zao tumezizuia hadi hapo watakapoleta vyeti kuthibithisha walikosomea. Madereva ambao watashindwa kuthibitisha leseni zao tutazifuta na watakua wamekosa sifa ya kuwa madereva.

“Madereva watakaobainika wanaendesha magari bila kuwa na leseni stahiki kulingana na magari wanayoendesha watakamatwa na kuwekwa mahabusu kabla ya kufikishwa mahakamani na leseni zao zitafungiwa kwa kigezo cha kukosa sifa ya kuendesha magari hayo,” alisema Kamanda Musilimu.

Aidha, kamanda huyo alisema katika kipindi hicho cha Julai 4 hadi 15, mwaka huu, jumla ya vyombo vya moto 81, 533 vilikaguliwa yakiwamo mabasi 4,068, malori 10,643, mabasi madogo (Coaster) 9,473, Hiace 7,327, Noah 2,138, Taksi 1,925, magari binafsi 22,421, pikipiki 6,678 na Bajaji 16,860.

Alisema kati ya magari 48, 896 yaliyokaguliwa, 33,837 yalibainika kuwa mabovu na 1,172 kati ya hayo yalizuiliwa na kung’olewa namba za usajili ili yakafanyiwe matengenezo na kurejeshwa kwa ukaguzi wa mara ya pili kabla ya kuruhusiwa kutembea barabarani.

“Magari 133 yaliyobainika kuwa mabovu kabisa yaliondolewa barabarani na yatafutiwa usajili kwa mujibu wa sheria. Natoa onyo kwa madereva watakaoendesha magari mabovu na wamiliki watakaoruhusu magari yao kuendeshwa barabarani yakiwa mabovu wote tutawanyakua, tutawaweka mahabusu na kuwafikisha mahakamani wakitokea mahabusu kwenda mahakamani,” alisema Musilimu.

Alisema madereva na wamiliki ambao magari yao yatapata ajali na kubainika kuwa chanzo cha ajali hizo ni ubovu wa gari watakamatwa na kupelekwa mahakamani.

“Elimu ya usalama barabarani ilitolewa kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa barabara. Jumla ya madereva 128,875 walipata elimu kati yao madereva wa magari walikuwa 31,870, bajaji 1,171, pikipiki 19,925, baiskeli 5,366 na mikokoteni walikuwa 543.

“Jumla ya abiria 197,633 walipata elimu, pia jumla ya shule za msingi 582 zilifikiwa ambapo jumla ya wanafunzi 78,674 walipatiwa elimu,” alisema Kamanda Musilimu.

Katika hatua nyingine kamanda huyo alitoa siku saba kwa madereva na wamiliki wa magari wanaodaiwa faini za makosa ya usalama barabarani kulipa faini hizo.

Alisema kuanzia Agosti Mosi, mwaka huu utaanza msako wa kukamata magari yanayodaiwa na kuwafikisha mahakamani madereva na wamiliki wa magari hayo.

AJALI SINGIDA

Wakati huo huo, Kamanda Musilimu alisema Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani limetuma ofisa wake mkoani Singida, kuchunguza tukio la ajali ya lori lililoyagonga magari mawili yaliyokuwa yesimamishwa kwa ukaguzi.

Taarifa za awali zilizolifikia gazeti hili kutoka eneo la tukio, zilieleza kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe  wa askari wa usalama barabarani aliyeyasimamisha magari hayo katika eneo lisilo salama.

Kamanda Musilimu alisema aliyetumwa atachunguza sababu ya askari waliokuwa eneo la tukio kuondoka baada ya kutokea ajali.

Alipoulizwa kuhusu agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuhusu magari kutembea usiku, alisema waziri huyo anatarajiwa kukutana na wadau wa usafirishaji Julai 31, mwaka huu kujadili namna mabasi hayo yatakavyofanya safari za usiku.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,051FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles