22.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

Kessy aikomalia Simba, imuadhibu Angban

kessy alvezNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umepewa siku saba kuhakikisha unamchukulia hatua za kinidhamu kipa Vincent Angban kutokana na kitendo cha kumpiga beki wa kulia wa timu hiyo, Hassan Ramadhani ‘Kessy’.

Wachezaji hao walizipiga baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliozikutanisha timu za Simba na Toto Africans ya Mwanza katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Angban ambaye ni raia wa Ivory Coast, alimchapa makonde ya usoni Kessy baada ya kukerwa na matokeo ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Toto, ambapo beki huyo alionyeshwa kadi nyekundu na kutolewa nje ya uwanja dakika ya 46.

Meneja wa mlinzi huyo aliyetua Simba akitokea timu ya Mtibwa Sugar, Athuman Tippo, aliliambia MTANZANIA jana hakufurahishwa na kitendo cha kipa huyo kumpiga Kessy huku akishangazwa kuona viongozi wamekaa kimya bila kuzungumzia suala hilo.

Alisema kitendo hicho kimedhihirisha wazi ni jinsi gani kikosi cha Simba kimekithiri utovu wa nidhamu, huku akidai kuwa uongozi usipotoa adhabu kali kwa kipa huyo watachukua hatua zaidi.

“Tayari tumeongea na mwanasheria wetu ndiyo maana tumewapa Simba siku saba kuhakikisha wametoa adhabu kwa Angban, wasipofanya hivyo tutaangalia hatua zaidi za kuchukua dhidi yake kutokana na kumsababishia maumivu Kessy,” alisema.

Alisema mlinzi huyo hajaumizwa sana lakini amesababishiwa maumivu sehemu za usoni, kitendo hiki hakistahili kufanyiwa mchezaji yeyote.

Tippo alisema kitendo cha kupigwa kwa Kessy kilimpandisha hasira beki huyo na kufikia hatua ya kutaka kugoma kuendelea kuichezea Simba kuanzia sasa, lakini baada ya kuzungumza naye walimshauri amalizie mkataba wake kabla ya kufanya uamuzi mwingine.

“Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, tumemwambia hakuna haja ya kugomea mechi ni bora amalize mkataba ndipo tufanye maamuzi mengine kama ni kuongeza mkataba au kuachana na Simba,” alisema.

Mbali na Kessy kutolewa nje kwa kadi nyekundu, pia mwamuzi Ahmada Simba wa Kagera alimwonyesha kadi nyekundu kocha wa timu hiyo, Mganda Jackson Mayanja kwa kumtolea maneno ya kuudhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,305FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles