23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Azam kumaliza ubishi kwa Waarabu leo

AzamNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Azam FC leo wanakabiliwa na kibarua kigumu ugenini watakapovaana na Esperance ya Tunisia katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Uwanja wa Olympique de Rades.

Azam ilitua juzi nchini Tunisia na kufanya mazoezi ya mwisho ya kupasha misuli katika Uwanja wa Hoteli ya Carthage Thalasso kabla ya kuhamia kwenye Uwanja wa Olympique de Rades watakaocheza leo.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuanza majira ya saa tatu usiku kwa saa za Tanzania sawa na saa moja usiku kwa saa za Tunisia, ambapo inaelezwa kwa muda huo hali ya hewa ya nchi hiyo inakuwa ya baridi kali.

Azam itaingia uwanjani ikiwa mbele kwa ushindi wa mabao 2-1, baada ya kushinda nyumbani katika mchezo wa awali wa raundi ya pili uliochezwa Aprili 10, mwaka huu katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Matokeo ya ushindi nyumbani yamewaweka ‘Wanalambalamba’ hao katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, kwani watahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili waweze kutinga hatua ya 16 bora na kuungana na klabu nyingine nane zitakazoondoshwa kwenye Klabu Bingwa barani Afrika.

Azam itawakosa nyota wake muhimu ambao ni mlinzi Pascal Wawa ambaye anasumbuliwa na nyama za paja, mshambuliaji Kipre Tchetche mwenye maumivu ya misuli na kiungo Jean Mugiraneza ‘Migi’ anayetumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Denis Kitambi, alisema wataingia uwanjani na staili mpya ya kubadili mbinu katika kila dakika 15 ili kuwasoma wapinzani wao vizuri na kuwakabili vilivyo huku wakisaka ushindi.

“Tunahitaji kuzitumia kila dakika 15 vizuri, tukifanikiwa kupata bao la mapema itakuwa vizuri zaidi lakini tutahakikisha tunamaliza dakika zote 90 kwa ushindi hata kama tayari tuna mabao, bado yanahitajika mabao zaidi.

“Wapinzani wetu wamebadilisha muda wa mchezo na kutuchezesha usiku ambapo kunakuwa na baridi kali, tumeshtukia hizo ni mbinu za kimichezo lakini tumejiandaa kucheza kwa hali yoyote iwe baridi au joto na tutaingia hatua inayofuata,” alisema Kitambi.

Msaidizi huyo wa kocha Mwingereza Stewart Hall, alisema licha ya kuwakosa wachezaji nyota wa kikosi cha kwanza wanaamini waliopo wanaweza kuziba pengo lililopo na kuipeperusha vyema bendera ya Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles