27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Hali si shwari Simba

5*Mayanja adai hawezi kuondoka mkataba unamlinda

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

WAKATI hali ikionekana si shwari ndani ya klabu ya soka Simba, kocha wa timu hiyo, Jackson Mayanja ameibuka na kudai kuwa yeye ana moyo wa chuma hivyo hana mpango wa kuihama timu hiyo kutokana na kulindwa na mkataba wake.

Licha ya Mayanja kuipa Simba mafanikio kwa muda mfupi aliofundisha tangu Januari mwaka huu, mambo yamezidi kuwa magumu hasa baada ya kikosi hicho kupoteza mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Toto Africans uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tangu aanze kuinoa Simba baada ya kutimuliwa kwa kocha Mwingereza Dylan Kerr, Mayanja ameiwezesha timu hiyo kushinda mechi 11 kati ya 13 walizocheza ambapo imefikisha pointi 57 na kushika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga wanaoongoza kwa pointi 59.

Hali imezidi kuwa tete ndani ya klabu ya Simba baada ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Toto juzi, ambacho kiliwafanya mashabiki kutoa mitazamo tofauti kwa kumtupia lawama kocha, baadhi ya viongozi wa klabu na wale wa Kamati ya Usajili wakitaka waondoke.

Kocha huyo raia wa Uganda aliliambia MTANZANIA jana kuwa yeye si aina ya makocha wanaokimbia timu na hawezi kuchukua uamuzi kinyume na taratibu hadi uongozi utakapoamua kumfukuza.

“Nina mkataba na klabu ya Simba, hivyo siwezi kukimbiakimbia maana nitaonekana wa ajabu kwenye taaluma ya ukocha.

“Kama tatizo limetokana na kufungwa na Toto mwamuzi ndiye hakututendea haki ingawa uzembe wa mabeki pia ulichangia kwa kiasi fulani kutuangusha,” alisema Mayanja.

Mayanja alisema wachezaji walipoteana kwenye safu ya ulinzi na katikati baada ya Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 46, ambapo hali hiyo iliongeza pengo kwa Simba iliyokuwa ikicheza bila nyota wake muhimu, Mwinyi Kazimoto, Jjuuko Murushid na Jastice Majabvi.

“Mimi si kocha mwenye kufanya kazi kwa kubahatisha, kama mwamuzi hakuharibu mchezo tulikuwa na kila sababu ya kupata ushindi, kwani wachezaji walikuwa vizuri na walihitaji ushindi,” alisema Mayanja.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amewajia juu mashabiki wa timu hiyo waliomzonga na kutaka kumfanyia vurugu baada ya mchezo wa juzi wakimtaka aondoke na kuwaachia timu yao.

Poppe alisema mashabiki wanashindwa kutambua majukumu yake ndani ya klabu ya Simba ambayo yanaishia kwenye usajili, huku akidai kuwa hahusiki na masuala ya benchi la ufundi ambayo yanawahusu zaidi wachezaji wanaoingia uwanjani kucheza na kocha.

Alisema kama mashabiki wamezoea kuwafanyia vurugu viongozi wengine wa klabu hiyo wasijaribu kwa upande wake kwani atawavuruga kweli kweli.

“Nilishangaa kitendo cha mashabiki kutaka kunifanyia vurugu, ndiyo maana nilivyoona wanazidi kunizonga ikabidi niwatawanye kwa kurudisha gari nyuma kwa spidi, nawaambia siku nyingine wakinifuata nitawavunja kweli miguu.

“Kwa sasa soka limetawaliwa na mazingira ya rushwa, mwamuzi alivyochezesha juzi ni kama kulikuwa nguvu fulani nyuma yake, siku zote mchezaji anaonywa mara moja kwa mdomo akirudia anastahili kuonyeshwa kadi, si kama naingilia kazi yao ila wanatakiwa kutenda haki,” alisema Poppe.

Katika hatua nyingine, Shirkisho la Soka Tanzania (TFF), limelaani vurugu zilizofanywa na mashabiki hao baada ya mchezo wa juzi likidai kitendo hicho si cha kiuungwana katika soka.

Shirikisho hilo limewataka wanachama na mashabiki kuwaheshimu viongozi waliopo madarakani na kama kuna mambo ya kujadili yakafanyiwe kazi kwenye klabu zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles