24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli amepata mwamko wa upinzani – Kasaka

kasakaNA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

MWANASIASA mkongwe aliyekuwa kinara wa kudai Serikali ya Tanganyika baada ya kuunda kundi la wabunge 55 maarufu (G55), Njelu Kasaka, amesema hatua anazochukua Rais Dk. John Magufuli zimetokana na msukumo alioupata kutoka kwa wapinzani.

Mbali na hilo, alieleza kushangazwa na watu ambao wamekuwa wakisema kutokana na kasi ya Rais Magufuli, sasa wapinzani hawatakuwa na nguvu.

Pia alisema katika utawala uliopita, nchi ilikuwa hatarini kiuongozi, kinidhamu, kimaadili na kwamba ingeendelea hivyo ingekuwa hatari zaidi.

Kasaka ambaye alipata kuwa Mbunge wa Chunya na baadaye Lupa mkoani Mbeya, alitoa kauli hiyo wakati wa mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika nyumbani kwake Mbagala, Dar es Salaam juzi.

“Nawashangaa wanaosema upinzani hauna nguvu tena eti kwa sababu ya kasi ya Rais Magufuli. Upinzani bado una nafasi, bila upinzani tutaiangamiza nchi hii… hao waliokuwa wanafanya ufisadi ni kwa sababu hakukuwa na chombo cha kuwabana.

“Leo tunaona Afrika Kusini namna upinzani walivyombana Rais (Jacob) Zuma hadi mwenyewe akakiri kurejesha zile fedha,” alisema Kasaka.

Alisema upinzani ndiyo umekuwa ukiibua mambo kwa usalama wa nchi, na kwamba hata Serikali iliyopo madarakani inafanya hayo, huku akilini mwao wakisema upinzani wasipate nafasi.

 

UTAWALA ULIOPITA

Aidha alisema katika utawala uliopita nchi ililegea kinidhamu, kiuongozi kiasi cha kuudhi ambapo kila mtu aliyekuwa ndani ya mfumo wa Serikali alifanya mambo  anavyotaka.

“Nchi yetu katika kipindi kilichopita ililegea sana, ilishuka kiuongozi, kinidhamu… ‘it went so low’ kiasi cha kuudhi. Kila mtu aliyekuwa ndani ya mfumo wa Serikali alifanya vile anavyotaka, hali ilikuwa si zuri kabisa.

“Ingekuwa hatari kama tungeendelea hivyo, pia rushwa ilikuwa jambo la kawaida na watu wamekuwa wakiidai wazi wazi… mimi mwenyewe nimeshuhudia; nilimpeleka mgonjwa nikakutana na vitu kama hivyo,” alisema.

Alisema kutokana na hayo, kulikuwa kuna kila sababu ya nchi kuhitaji mabadiliko na ndiyo maana wagombea mbalimbali walilitumia neno hilo katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

“Hata CCM wenyewe walilitumia neno mabadiliko kwa sababu nchi ilikuwa na hali mbaya, na Magufuli mwenyewe alilazimika kutumia neno hilo,” alisema Kasaka.

Alimtaka Rais Magufuli kujenga demokrasia ya kweli na kutokomeza udanganyifu na rushwa katika uchaguzi.

“Watu wanashinda kwa udanganyifu… wanaiba kura. Unaponyang’anya ushindi wa mtu baadaye mnakuja kupigana. Tunaomba atusaidie kujenga demokrasia ya kweli nchini.

“Nampongeza kwa jambo moja, kuwaambia wanaCCM wenzake kuhusu Uchaguzi wa Meya wa Dar es Salaam, kwamba wakubali pale wanapoonekana kushindwa na baadaye uchaguzi ukafanyika,” alisema Kasaka.

 

WALIOHAMA CCM

Akizungumzia kuhusu makada mbalimbali wa CCM kuhamia upinzani katika uchaguzi uliopita, Kasaka alisema makada hao, hususani Edward Lowassa, walihama kwa sababu ya udanganyifu uliokuwepo ndani ya chama hicho tawala.

“Kina Lowassa walijiondoa kwa sababu ya udanganyifu ndani ya CCM. Lowassa ni miongoni mwa makada 38 waliokuwa wakigombea urais, sasa badala ya kupeleka majina yao ili yachujwe kwenye Kamati Kuu, yakapelekwa majina matano tu.

“Kwanini usipeleke jina lake halafu lijadiliwe kwamba jamani huyu mwenzetu yuko hivi? Mfano mgombea urais wa Chama cha Republican, Donald Trump, hajaondolewa kwenye kinyang’anyiro, lakini wanaelimisha watu kwamba jamani huyu hafai kutokana na hili.

“Lakini sasa mnapokaa watu wachache, tena ‘officially’, hiyo ni hatari… mtu lazima awachukie kwa sababu uchaguzi wenu ni geresha. Hata kama mtu hafai kwanini msieleze matatizo yake?” alisema.

Akizungumzia uchaguzi wa marudio Zanzibar, alisema kwa kuwa waliulazimisha, kwa sasa pande zote wakae chini kuleta suluhu jinsi ya kuleta umoja.

Alisema kutokana na hilo, bado ile hatari ya kuvunjika muungano iko pale pale.

Kasaka na wabunge wenzake 54, mwaka 1993, waliibua hoja ya kutaka kuundwa Serikali ya tatu ambayo ingeitwa Tanganyika, lakini hoja yao ilizimwa vikali na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles