27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

JPM AONYA KUHUSU NJAA

Na ALLY  BADI- LINDI


RAIS Dk. John Magufuli, amesema kama Watanzania hawatalima kwa bidii watakufa kwa njaa.

Aliyasema hayo   jana kwa  nyakati  tofauti alipokuwa  akihutubia  wakazi  wa  Mkuranga mkoani Pwani na  Nangurukuru na Mchinga, mkoani Lindi akiwa njiani kwenda Lindi kwa ziara ya siku mbili.

Kwa mujibu wa Rais Dk. Magufuli, ni vizuri wananchi   wakafanya  kazi  ya   kulima    mazao mbalimbali yakiwamo ya  chakula kwa kuwa ndiyo yatakayowasaidia kukabiliana na njaa.

“Yatumieni mashamba kwa kufanya  kazi ya  kuzalisha  chakula kwa sababu  msipofanya  kazi,   mtakufa  na njaa kwa sababu hakuna  chakula  cha Serikali.

“Fanyeni kazi kwa juhudi na mtumie vizuri  mvua  inayoendelea  kunyesha hivi sasa kwa  kuzalisha  mazao  ya  kilimo.

“Najua mmezoea kusikia maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa njaa, sasa mimi nasema usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata chakula wakati mvua inanyesha Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa.

“Ni lazima tufanye kazi, hivi sasa mvua inanyesha limeni mazao ya chakula," alisisitiza Rais Dk. Magufuli.

Pia, aliwatahadharisha   wana CCM  wanao tarajia  kuomba  nafasi  mbalimbli  za uongozi  kwamba majina yao hayatarudi   watakapotumia rushwa wakati wa kuomba nafasi hizo.

“Ninawaambia wana CCM wenzangu  yeyote atakayebainika jina lake limepita kwa njia ya ujanjaujanja, yaani kwa kutumia rushwa, jina lake likifika kwetu  halitarudi.

“Kiongozi mzuri ni yule anayepata uongozi  kwa njia  halali bila kutumia rushwa. Hivyo ni  vema  wana CCM  wanaohitaji kuomba uongozi wajipange kwa hilo,” alisema.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli, aliweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vigae cha Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited kilichopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Kiwanda hicho kinachoelezwa kuwa ni kikubwa Afrika Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu Dola za Marekani milioni 50 kwa awamu ya kwanza, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku na kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.

Akizungumza kiwandani hapo, Rais Dk. Magufuli aliishukuru menejimenti ya kiwanda kwa uwekezaji huo na kusema amefurahishwa na teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae inayotumika kiwandani hapo.

Kwa sababu hiyo, alipiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na kutaka mchanga wote ufanyiwe uyeyushaji   nchini.

"Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000.

“Naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini, kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi," alisama Rais Dk. Magufuli.

  Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru, alisema pamoja na kiwanda hicho, tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, viwanda 2,169 vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na vipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.

Naye Balozi wa China  nchini, Dk. Lu Youqing, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kutilia mkazo juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi barani Afrika.

“Kwa mujibu wa takwimu za TIC, mpaka mwisho wa Juni 2016 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka China umefikia Dola za Marekani bilioni 6.6 na umezalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 150,000 na zisizo za moja kwa moja 450,000.

“Pamoja na hayo, kiwanda hiki cha Goodwill Tanzania Ceramic Limited, kimejengwa na wawekezaji kutoka China ingawa vipo viwanda vingine vingi vinaendelea kujengwa.

“Hata Mbunge wa hapa Mkuranga ameniambia kuna viwanda zaidi ya 50 vya Wachina vinavyojengwa hapa Mkuranga, nimefurahi   kuona karibu kila sekta Watanzania wanafurahia ushirikiano wa Tanzania na China," alisema balozi huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles