23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE AGONGA MWAMBA KORTINI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeyatupa maombi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ya kutaka asikamatwe na kuwekwa kizuizini, hadi maombi yake yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Wakili Jenerali Ulimwengu ameungana na Wakili Peter Kibatala kumwakilisha Mbowe mahakamani.

Maombi ya Mbowe yalitupwa jana na jopo la majaji watatu, Jaji Sakieti Kihiyo, Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Khaday baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na Jamhuri.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Mwandambo alisema maombi yaliwasilishwa kimakosa chini ya kifungu namba 2(3) cha Sheria ya Jala (Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria).

“Kifungu cha sheria kilichotumika si sahihi kwa sababu sheria hiyo hutumika pale ambapo sheria zetu ziko kimya, waleta maombi watafute vifungu sahihi vya kuwasilisha maombi mahakamani,”alisema.

Alisema sababu hiyo moja ni ya msingi hivyo mahakama inayatupa maombi na kesi ya kikatiba itasikilizwa Machi 8 mwaka huu.

Katika maombi hayo yaliyotupwa Mbowe aliomba mahakama itoe amri asikamatwe wala kuwekwa kizuizini mpaka maombi yake ya zuio yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Hata hivyo Wakili Ulimwengu alidai watasoma sheria za Uingereza kuangalia vifungu ambavyo vitasaidia kuyarudisha maombi hayo mahakamani.

“Tutatumia siku ya leo na kesho….kesho tutawasilisha maombi haya mahakamani,” alidai.

Kabla ya maombi hayo kuanza kusikilizwa Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata aliwasilisha pingamizi, akiomba mahakama iyatupilie mbali kwa sababu  yako nje ya muda, hayana msingi na kifungu cha sheria kilichotumika si sahihi.

Wakili huyo, alidai mahakama hiyo ni ya madai, hivyo haina mamlaka ya kusikiliza masuala ya jinai.

Alidai suala la Mbowe kukamatwa na Polisi ni la kijinai na Polisi wamefanya kazi yao kwa mujibu wa sheria hivyo maombi hayo hayakupaswa kupelekwa katika mahakama hiyo badala yake walitakiwa kuyapeleka kwenye mahakama husika.

Katika kesi ya kikatiba namba 1ya 2017, mdai ni Mbowe na wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. 

Katika kesi hiyo ya katiba, Mbowe anaomba Mahakama Kuu itamke   kuwa Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kudhalilisha na kukamata.

Mbowe pia anaomba mahakama itengue vifungu vya 5 &7 vya Sheria ya Tawala za Mitaa kwa kuwa ni batili na vinakiuka haki ya katiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles