24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 30, 2023

Contact us: [email protected]

‘JPM AMWALIKA RAIS WA MISRI NCHINI’

 

 

NA AZIZA MASOUD

-DAR ES SALAAM

RAIS wa Misri, Abdel Fattah Al Sisi, wiki ijayo anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili nchini.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Dk. Aziz Mlima, alisema kiongozi huyo anakuja nchini kwa mwaliko wa Rais Dk. John Magufuli.

Alisema Rais Al Sisi ataambatana na ujumbe wa watumishi wa Serikali yake pamoja na wafanyabiashara wakubwa wa Misri.

Kwa mujibu wa Dk. Mlima, ziara ya kiongozi huyo ina lengo la kukuza na kuimarisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo mbili.

“Ziara hii itatoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, kikanda na kimataifa,” alisema Dk. Mlima.

Alisema pamoja na mambo mengine, Rais Al Sisi atafanya mazungumzo ya faragha na Rais Dk. Magufuli na baadaye atafanya ya wazi ili wananchi waweze kumsikia.

Alisema Tanzania na Misri zimekuwa na uhusiano katika nyanja mbalimbali, ikiwamo kijamii, kiuchumi, kisiasa, ulinzi na usalama pamoja na medani za siasa za ushirikiano wa kimataifa.

Pia nchi hizo zimekuwa na ushirikiano katika ngazi za taasisi za serikali, kama  Taasisi ya Udhibiti wa Utawala ya Misri  ambayo inashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).

Aliongeza kuwa, ushirikiano mwingine ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, ambazo zimesaini makubaliano ya ushirikiano na Hospitali ya El Shatbyya ya Chuo Kikuu cha Alexandria, nchini Misri.

Alisema nchi ya Misri, ambayo ni ya pili  kwa kuwa na uchumi mkubwa katika Bara la Afrika, takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha pato lake la Taifa (GDP) lilikua kwa Dola za Kimarekani bilioni 266.213.

Alisema sekta kubwa ambayo imechangia pato hilo ni huduma za kibenki, mawasiliano, usafirishaji na utalii, ambayo imechangia asilimia 52.5, wakati viwanda ni asilimia 36.3 na kilimo asilimia 11.2.

Tanzania itakuwa nchi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki kutembelewa na Rais Al Sisi.

Mapema mwaka huu, kiongozi huyo alitembelea nchi ya Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,282FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles