29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA KUU YABARIKI RUZUKU YA LIPUMBA

 

PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetupilia mbali maombi ya Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif, ya kutaka Msajili wa Vyama vya Siasa asitoe ruzuku kwa chama hicho upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Maombi hayo namba 21 ya mwaka 2017 yametupiliwa mbali jana na Jaji Wilfred Dyansobera, baada ya Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata, anayemwakilisha mdaiwa wa pili katika kesi hiyo, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kusema kuwa kesi imeitishwa kwa ajili ya uamuzi.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa wa kwanza ni Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Dyansobera amesema kuwa, anakubaliana na hoja  moja katika pingamizi la AG kwamba vifungu vya sheria vilivyotumika kufungua kesi hiyo si sahihi.

Pia alisema kuwa, anakubaliana na hoja za Bodi ya Wadhamini inayomuunga mkono Maalim Seif, kwamba suala la bodi hiyo kutokuwa na uhalali linahitaji ushahidi wa kina.

Alisema kitendo cha Maalim Seif kusaini hati mbalimbali za kesi bila kupewa mamlaka hilo si pingamizi, kwani mahakama hiyo haiwezi kutoa uamuzi kwa kuangalia kiapo peke yake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uamuzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Mbarara Maharagande, amesema watajipanga upya na kufungua tena maombi hayo Agosti 14, mwaka huu, siku ya Jumatatu wiki ijayo.

Awali katika kesi hiyo, Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata, aliwasilisha hoja za kupinga maombi hayo mbele ya mahakama.Wakili Malata alidai kuwa, maombi hayo hayapo kisheria kwa hoja ya kwamba hakuna bodi halali ya wadhamini iliyoleta maombi hayo.

Alidai kuwa, bodi ya wadhamini iliyofungua kesi hiyo ilimaliza muda wake Agosti mwaka jana na kwamba bodi hiyo si halali.Alisema hoja nyingine ni kwamba vifungu vya sheria vilivyotumika kuwasilisha maombi hayo si sahihi.

Wakili wa Serikali alieleza Mahakama hiyo kuwa, maombi ambayo yameletwa kwenye vifungu hivyo hayaipi mamlaka Mahakama kuruhusu maombi hayo.

Alisema kanuni ndogo ya kwanza na ya pili inaelekeza mapitio hayo ya kisheria yasifanyike mpaka maombi yakubaliwe na Mahakama.Alisema ili isikilizwe, ni lazima kitolewe kibali au nyaraka ambayo ni kiapo ambacho kinaeleza mambo yanayotumika.

Kuhusu hoja ya wadhimini kutokuwa halali, alieleza kuwa hilo ni suala ambalo linahitaji ushahidi, kwa sababu yapo madai kama hayo yanayoeleza kuwa bodi ipo sahihi.Alitanabahisha kuwa, kifungu cha 14 cha sheria ya mwenendo wa mashtaka ya madai kinafafanua kwamba, shuguli zote za wanachama au wadhamini ni za ndani ya chama kwa mujibu wa Katiba ya CUF.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles