30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

JESHI LA WANANCHI LAJISALIMISHA TANESCO

Na ESTHER MBUSSI-DAR ES SALAAM


JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka wanaotoa huduma katika jeshi hilo kuzingatia suala la ulinzi na usalama kabla ya kusimamisha huduma hizo.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo,  aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana.

Alizungumzia agizo la Rais Dk. John Magufuli  lililoitaka Shirika la  Umeme Tanzania (Tanesco), kuyakatia umeme mashirika na taasisi zote za serikali zinazodaiwa umeme,   JWTZ likiwa ni miongoni mwa taasisi zinazotakiwa kukatiwa umeme leo kutokana na deni kubwa.

Jenerali Mabeyo alikiri kuwa JWTZ inadaiwa na Tanesco zaidi ya Sh bilioni tatu.

Alisema msingi wa deni hilo ni matumizi makubwa ya umeme ndani ya jeshi hilo hali inayochangiwa na ukweli kwamba limesambaa  nchi nzima.

  Hata hivyo,  alisema   JWTZ  leo limejipanga kupunguza   Sh bilioni moja katika   deni kwa  Tanesco.

“Kwa upande mwingine tunaomba kuwakumbusha tu kwamba suala la ulinzi wa taifa halina mbadala hivyo kusimamisha huduma yoyote ni kuathiri usalama wa taifa.

“Ndiyo maana tunawaomba   wanaotoa huduma kwetu wazingatie suala zima la ulinzi wa  taifa na  kadri tunavyolipa waendelee kutupatia huduma,” alisema.

Alisema ufinyu wa bajeti na matumizi makubwa ya umeme umesababisha jeshi hilo kudaiwa kiasi hicho kikubwa cha fedha.

“Pili ni mipango pamoja na zana tunazotumia ambazo nyingine zinatakiwa kuwashwa muda wote saa wa 24 katika kulinda na kuimarisha ulinzi wa taifa.

“Hili tunaweza kufanya kutokana na kukua kwa teknolojia duniani ambako jeshi linalazimika kuendana na ukuaji huu na usipoendana nao unakuwa nyuma.

“Ufinyu wa bajeti ambao umekuwa changamoto kubwa…mahitaji ni makubwa.

“Lakini baada ya kupokea maagizo haya ya Tanesco, jeshi letu limetafakatri na limefanya jitihada za kupunguza deni.

“Tunadaiwa zaidi ya Sh bilioni tatu tayari nimeagiza watendaji wetu watafute bilioni moja wahakikishe kesho (leo) cheki inawafikia Tanesco haraka. Ni pungufu lakini tunaamini kwa nia njema Tanesco watatusikiliza,” alisema.

Jenerali Mabeyo alisema licha ya kudaiwa na Tanesco , jeshi hilo linadaiwa na wazabuni wengine wanaotoa huduma.

“Tunashukuru Hazina imeanza kutupatia fedha kidogo kidogo   kupunguza madeni hayo.

“Tuna imani tutayamaliza lakini juhudi hizi za kupunguza madeni tunaomba zionyeshwe pia na taasisi nyingine ili Tanesco iweze kutoa huduma bora zaidi kwetu na wananchi kwa ujumla ambao hadi sasa wana shida ya umeme,” alisema.

Alisema jeshi linaendelea kutafakari na kuandaa mikakati mbalimbali   kupitia mashirika yake kama vile Mzinga, Nyumbu na Suma JKT.

Alisema lengo ni kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwamo viwanda vinavyoweza kuzalisha bidhaa   zitakazoweza kutumika na jeshi na wananchi ili mwisho wa siku wapunguze utegemezi wa kila kitu kutoka serikalini.

“Tunaamini tukifanikiwa   hilo tutaondokana na madeni yanayotukabili mara kwa mara na hatua hii pia itainua uchumi wa taifa.

“Kwa kuanzia tayari tumeandaa waraka wa serikali ili ujadiliwe na baraza la mawaziri namna ya kuendeleza Shirika la Nyumbu.

“Naamini waraka huo utakapojadiliwa utapitisha mapendekezo yetu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles