23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO ALIYEKWENDA NA SPIKA BANDARINI AFUKUZWA

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli  ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.

Taarifa iliyotolewa  jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Dk. Magufuli   nafasi ya Profesa Ntalikwa itajazwa baadaye.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya Ikulu haikueleza sababu za utenguzi huo.

Profesa Ntalikwa anakuwa Katibu Mkuu wa kwanza kutenguliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano  ya Rais Dk. John Magufuli.

  Spika wa Bunge, Job Ndugai alifuatana na Profesa Ntalikwa alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam jana na waliachana saa 7:30 mchana, wakati  taarifa za kutenguliwa kwake zilitolewa saa 10:55 jioni.

 

 

 

Kwenye ziara hiyo, Spika Ndugai na ujumbe wake walikagua makontena 282 yenye mchanga wa madini yaliyozuiwa bandarini hapo yasisafirishwe nje ya nchi hadi yafanyiwe ukaguzi wa kina.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Spika alisema ataunda kamati maalumu kuchunguza makontena hayo.

Alisema   kamati hiyo itachunguza biashara yote ya madini na itapitia upya mikataba ya madini na sheria zilizopo  kuona kama zina upungufu.

Ndugai  alisema baada ya kamati hiyo kuundwa na kukamilisha kazi yake, Bunge litaishauri Serikali namna ya kufanya.

Katika ziara hiyo, Spika Ndugai alikuwa na wabunge 10 ambao ni wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Bajeti na Nishati na Madini.

“Baada ya ziara ya Rais Dk. Magufuli hapa bandarini, tulishtuka kidogo, lakini baada ya jana (juzi) kuripotiwa makontena mengine 256 tuliona jambo hili si dogo.

“Niliona nije mwenyewe badala ya kutuma wenzangu. Kwa hali ilivyo, tutaunda kamati maalum na nitaipa jina hapo baadaye na itachunguza suala zima linalohusiana na biashara hii kwa ujumla wake.

“Wananchi wengi wa Tanzania wana maswali mengi kuhusu biashara  hii inaendeshwaje, nani mfaidika kwa sababu maswali yamekuwa mengi.

“Hivyo basi wakati umefika kwa sisi kuchukua hatua tunapoona utajiri wa nchi yetu unaondoka,” alisema Spika Ndugai.

KATIBU MKUU NISHATI

Wakati Spika akisema hayo, Profesa Ntalikwa ambaye wakati huo alikuwa hajaondolewa, alisema wizara  nayo itaunda tume itakayohusisha taasisi mbalimbali kuchunguza kilichomo kwenye makontena hayo  kujua kama ni mchanga au ni dhahabu.

Katika maelezo yake, Profesa Ntalikwa alisema angeunda tume ambayo ingechukua sampuli katika makontena hayo na kuzipeleka kwenye maabara kwa ajili ya kuzipima upya.

Hata hivyo, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), alitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kuanza kufanya uchenjuaji wa mchanga wa madini   nchini.

“Je, tuna uwezo wa kufanya smelting (uchenjuaji) hapa nchini?. Nauliza hivyo kwa sababu naona tunapishana kuhusu kilichomo kwenye makontena, au tuna mpango wa kuzuia hii biashara?” alihoji Ghasia.

Akijibu hoja hiyo, Profesa Ntalikwa alisema uchenjuaji unahitaji fedha nyingi na kwamba mchakato unaendelea wa kutafuta mwekezaji katika eneo hilo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, alisema baadhi ya makontena yaliyozuiwa yalikuwa yamefikia hatua za mwisho yakisubiri kupakiwa kwenye meli.

“Baadhi ya makontena hayo  yalifikishwa bandarini hapa mwishoni mwa mwaka jana na mengine mwanzoni mwa mwaka huu.

“Lakini hatua ya kuyatafuta inaendelea, inawezekana mengine yako njiani ama bado yako kwenye machimbo, lakini yakifikika hapa bandarini, lazima tutayakamata kwenye ‘scanner’.

“Scanner zimetusaidia kubaini matatizo yaliyokuwa yakifanyika huko nyuma na tunatarajia scanner nyingine sita zitafungwa miezi miwili ijayo.

“Pia, tumefunga kamera na kuna watu maalumu wanaangalia kila kinachoendelea kwenye makontena,” alisema.

UTATA KUHUSU KUWAMO KWA DHAHABU NYINGI

Katika ziara hiyo, mjadala uliibuka kuhusu kiasi cha dhahabu iliyomo katika mchanga huo na namna sampuli zinavyochukuliwa   kwenda kupimwa.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TMAA, Gilay Shanika, alisema katika makontena hayo, shaba ni asilimia 17, fedha asilimia 0.02 na dhahabu asilimia 0.02.

“Kwa taarifa tulizopata, asilimia kubwa ni shaba mengine kidogo ni fedha na dhahabu ni asilimia 0.02…labda tufanye ukaguzi upya.

Baada ya majibu hayo Spika Ndugai alisema kama madini ya shaba ndiyo mengi katika mchanga huo basi Tanzania ilipaswa kuwa nchi inayoongoza kwa uzalishaji badala ya Zambia.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, alipingana na taarifa hizo na kusema kuwa sehemu kubwa ya madini yaliyomo katika mchanga huo ni dhahabu.

“Kwa taarifa za awali tulizonazo ni kwamba makontena 254 kati ya 282 yana madini ya dhahabu. Madini ya shaba ni asilimia nane, fedha asilimia mbili na dhahabu asilimia 90.

Katika mjadala huo, Spika Ndugai pia alionyesha wasiwasi wake juu ya ufungaji wa rakili na kuhoji kwa nini ufanyike Buzwagi na Ulyankulu wakati maabara ya TMAA iko Dar es Salaam.

“Anayechukua sampuli ni mwajiriwa wa TMAA au Buzwagi?  Taarifa zinaletwa baada ya muda gani na nani anasimamia kwamba kinachokuja kiko sahihi?” alihoji Ndugai.

Akijibu swali hilo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TMAA, alisema wao huwa wanachukua sampuli kupitia kwa wakaguzi wao walioko kwenye migodi.

Alisema baada ya hapo  huzilinganisha na majibu ya sampuli zilizochukuliwa na mgodi. Pamoja na hayo, alisema makontena yanayosafirishwa nje ya nchi ni kati ya 55,000 na 60,000 kwa mwaka.

Wiki iliyopita, Rais Dk. Magufuli alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam na kukuta  makontena 20 ya mchanga wa dhahabu. Lakini, baada ya siku tatu, TPA ilibaini kuwapo   makontena mengine 256.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles