24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Jecha ni gumzo

GRACE SHITUNDU -DAR ES SALAAM

MCHAKATO wa kumpata atakayekiwakilisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kinyang’anyiro cha urais Zanzibar unaonekana kuwa si wa kitoto baada ya jana aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi  visiwani humo (ZEC), Jecha Salim Jecha kujitokeza kuchukua fomu.

Jecha ambaye si tu amepandisha joto bali ameongeza idadi ya wagombea waliojitokeza kuchukua fomu ya urais CCM kufikia 14 visiwani Zanzibar, hatua yake hiyo tayari imezua gumzo.

Pamoja na kuhoji ni lini amekuwa mwanachama wa CCM, ilihali ni miaka michache tu alikuwa akishikilia wadhifa mkubwa wa Mwenyekiti wa ZEC lakini hatua yake hiyo imekumbusha wengi uamuzi wake wa kutangaza kufuta wengine wanaita kimizengwe matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 visiwani humo.

Itakumbukwa hatua yake ya kufuta uchaguzi huo na kuitisha mwingine ambao ulisusiwa na kilichokuwa chama kikuu cha upinzani visiwani humo cha CUF, iliibua vita kali ya maneno dhidi yake yeye binafsi na Serikali zaidi akidaiwa kuvunja sheria na Katiba.

Pamoja na kuwako kwa vita hiyo ambayo imeacha makovu visiwani humo, Jecha wakati akitangaza kufuta matokeo hayo kupitia runinga ya serikali visiwani humo ZBC alieleza sababu kadhaa za ikiwamo ile ya  kudai kuwa uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.

Alisema uchaguzi huo ambao aliyekuwa mgombea wa urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alidai kuwa ameshinda kwa asilimia 52 haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria za uchaguzi.

Alisema baadhi ya makamishna wa tume hiyo, walishindwa kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba na badala yake walikuwa ni wawakilishi wa vyama vyao.

Septemba 2, 2016, Rais Dk. John Magufuli akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Gombani ya Kale  mkoani Kaskanizi Pemba ya kuwashukuru wananchi baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa CCM alipendekeza Jecha apewe tuzo kwa kusimamia uchaguzi vizuri.

“ Nampongeza sana mheshimiwa  Jecha kwa kusimamia uchaguzi na umeenda vizuri sana na kama kuna tuzo mheshimiwa Shein (Rais wa Zanzibar Dk. Mohammed Shein ) utazitoa umpe Jecha  hiyo tuzo,”alisema rais Magufuli huku akishangiliwa na umati wa wana-CCM waliokusanyika kumsikiliza.

Kauli  hiyo ya Rais Magufuli ilikuja katika wakati ambao kulikuwa na vita baridi kati ya Maalim Seif na Dk. Shein.

Katika vita hiyo, Maalim Seif alikuwa ameendelea na msimamo wake wa kutotambua uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 21, 2015 ambao ulimpa ushindi Dk.Shein huku CUF wakisusia uchaguzi huo.

Jecha ambaye  miaka miwili baadaye yaani Aprili 18, 2018 baada ya kufuta matokeo hayo na kufanyika uchaguzi mwingine uliomwingiza madarakani, Dk. Shein ambaye sasa anamaliza muda wake  aliondoka kwenye wadhifa huo wa Mwenyekiti wa ZEC baada ya kukaa kwa miaka minne tu.

Tangu wakati huo alipotangaza kuondoka ZEC amekuwa kimya hadi alipojitokeza jana kuchukua fomu.

Baada ya kukabidhiwa fomu, Jecha alitoa wasifu wake na kusema endapo atateuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo atawaunganisha wakazi  wa Zanzibar, atasimamia maendeleo ya nchi na kusimamia haki za watu wote bila kubagua.

MCHAKATO ULIVYO

Mchakato huo wa kuwania urais kupitia tiketi ya CCM  unaonekana kuwa wa moto kutokana na idadi ya wachukua fomu sambamba na majina makubwa ya waliojitokeza katika nyanja za siasa.

Kati ya waliochukua fomu kuna Mawaziri wanaotumikia uwaziri wao katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuna mabalozi, viongozi wastaafu na makada wengine wa CCM.

Uchukuwaji wa fomu umeanza juni 15 na zoezi hilo litaendelea hadi Juni 30 na kufuatiwa na vikao vya CCM kupitisha jina moja la mgombea atakayemrithi Dk. Shein.

Idadi hii inaelezwa kuongeza ushindani wa kinyang’anyiro na  kuwafanya wajuzi wa siasa kushindwa kubashiri moja kwa moja ni nani atasimamishwa na CCM katika kuwania nafasi hiyo.

Hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho alikutana na kufanya mazungumzo na Rais anayemaliza muda wake  Dk. Shein jijini Dodoma.

Pamoja na kwamba hadi sasa katika makada hao 14 waliochukua fomu, kuna majina makubwa ambayo yanatajwatajwa, CCM imekuwa haitabiriki hasa katika uteuzi wa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar.

Makada wengine wa CCM waliochukua fomu hadi sasa ni pamoja na Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ulinzi wa Tanzania, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia ni mtoto wa Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi.

Yumo pia mwanamama pekee hadi sasa  Mwatum Mussa Sultan kwenye orodha hiyo, Haji Rashid Pandu ambaye kitaaluma ni mwalimu, na Abdallah Mohammed Ali (kitaaluma ni Daktari).

Wengine ni aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, Balozi Ali Karume ambaye ni mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Abeid Karume, Balozi Mohamed Hijja Mohamed, Mohamed Jaffar Jumanne.

Pia Balozi Meja Jeneral Mstaafu Issa Suleimani Nassor, Mhandisi Mbwana Bakari Juma, Mbwana Yahaya Mwinyi  kutoka Umoja wa vijana CCM na Omari Sheha Mussa aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara ya Fedha kipindi cha utawala wa Dk Salmin Amour.

Tangu lilipoanza zoezi la kuchukua fomu lianze Juni 15 aliyefanikiwa kurudisha fomu hadi sasa ni Balozi Ali Karume.

Pamoja na Jecha majina yanayotajwa kuongeza chachu katika kinyang’anyiro hicho ni Profesa Mbarawa, Dk Mwinyi, Balozi Ali Karume na Shamsi Vuai Nahodha.

Mbarawa na Mwinyi kwa muda mrefu walikuwa wakitajwa kuwa huenda mmoja wao ataibeba bendera ya chama hicho.

Profesa Mbarawa aliyetumika katika Wizara ya Ujenzi na sasa Wizara ya Maji  huku akionekana kuaminiwa na Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani.

Naye Waziri Dk Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais wa serikali ya awamu ya pili ameonyesha kutumikia na kudumu katika wizara ya Ulinzi kwa muda mrefu pasipo kutumbuliwa hasa katika kipindi hiki cha tumbuatumbua ni baadhi ya taswira ambazo wachambuzi wanaziangalia katika mchuano wa sasa wa nani atakayepitishwa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.

Hata hivyo kuwepo kwa majina ya Balozi Ali Karume na Shamsi Vuai Nahodha nako kunaongeza chachu zaidi hasa kwa siasa za visiwani Zanzibar.

Balozi Ali Karume ambaye si mara ya kwanza kujitokeza kuonyesha nia kama ilivyo kwa Nahodha naye ameongeza moto baada ya kuonyesha kuwa anatamani kuwa Rais kama ilivyokuwa kwa baba yake na pia ndugu yake Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Karume.

Nahodha ameongeza chachu katika kinyanganyiro hicho hii ikiwa ni mara ya pili kwa kada huyo kuomba ridhaa ya kuwania nafasi hiyo.

Katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2010 Nahodha alichukua fomu ambapo hata hivyo jina lake halikurudi kwa wananchi kutoka Dodoma, ingawa katika mchakato huo jina lake na la aliyekuwa Makamu wa Rais Dk. Ghalib Bilal yalitajwatajwa sana lakini Dk Shein aliteuliwa na kuchukua urais wa Zanzibar.

Utoaji fomu ulianza Juni 16 katika ofisi za chama hicho Kisiwandui mjini Unguja na Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya oganizasheni Zanzibar, Cassian Galos Nyimbo.

Kwa utamaduni wa chama hicho, Rais akimaliza mihula miwili ya miaka mitano mitano hustaafu na kuwaachia wengine kugombea nafasi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles