27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Dk Shein avunja baraza la wawakilishi akizungumzia uchaguzi mkuu

Mwandishi wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali imetunga Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018, ili kuweka utaratibu bora wa uchaguzi na kuondoa kasoro zote zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita.

Kutokana na hali hiyo, alisema ni wajibu wa viongozi wa vyama vya siasa na wanachama kuheshimu, kazi  Tume za Uchaguzi nchini (ZEC na NEC), kwani vyombo hivyo vimeundwa kikatiba.

Akilivunja Baraza la tisa la Wawakilishi, Dk alisema hatua yoyote ya kuchukua maamuzi kinyume na utaratibu uliowekwa na sheria, utasababisha zogo na kuanzisha fujo.

“Zogo na fujo ndio chanzo cha watu kugombana na hatimae kuingiana maungoni, hayo sio madhumuni ya uchaguzi, kwa hivyo uchaguzi wa Oktoba mwaka huu utakuwa huru na haki”, alisema.

Alitoa tahadhari kwa wenye nia ya mawazo ya kutaka kuharibu uchaguzi kwa njia yoyote ile au kufanya fujo,  waondokane na fikra hizo, kwani jambo hilo halitowezekana kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa sheria za uchaguzi, katiba pamoja na fedha za kuendesha uchaguzi huo zipo kutoka Serikalini  na kubainisha kuwa vikosi vya Ulinzi na Usalama viko makini kusimamia uchaguzi huo.

“Nawatangazia mimi na Dk. John Pombe Joseiph Magufuli tupo macho, hatutasinzia seuze kulala, tutatekeleza wajibu wetu na watakaofanya vituko dhidi ya sheria  tutawashughulikia”, alisema.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema Serikali imeamua kuzifungua skuli zote za maandalizi, msingi na Sekondari Unguja na Pemba kuanzia Jumatatu ya Juni 29, mwaka huu.

Alisema hatua hiyo inatokana na corona hivi sasa kuwa shwari kuliko ilivyokuwa a April, Mei na wiki ya mwanzo ya mwezi wa Juni, akibainisha kutowepo kwa mgonjwa hata mmoja katika vituo vyote vilivyokuwa vikiwatibu wagonjwa Unguja na Pemba.

Alisema ni muda wa siku 10 umepita tangu mgonjwa wa mwisho kutoka katika vituo hivyo, hali inayobainisha kuwa ni shwari.

Aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kuandaa mipango madhubuti na kabambe ya namna bora zaidi kwa wanafunzi wanapokuwa masomoni, ikizingatiwa mazingira ya madarasa mengi kuwa na idadi kubwa ya  wanafunzi.

Vile vile,  aliutaka uongozi wa kampuni za Boti na meli zinazosafiri kati ya Zanzibar na Dar es Salaama pamoja na Unguja , Pemba na Tanga kuhakikisha zinachukua abiria kwa mujibu ya viti ya vyombo vyao kama ilivyosajiliwa , kuanzia  Juni 29, mwaka huu.

“Abiria hawataruhusiwa kusimama au kukaa popote wakiwa safarini, Serikali itachukua hatua dhidi ya Kapteni na kukifungia chombo chochote  kitakachokiuka mashart haya”, alisema.

Aidha, Dk. Shein aliwataka wafanya biashara kufanya shughuli zao kwa nidhamu pamoja na kuruhusu shughuli za kijamii kuendelea kama kawaida; ikiwemo arusi, maulidi, hitma na kadhalika, huku akiwataka wananchi kuzingatia taratibu na kanuni za Afya kama inavyoshauriwa na wataalamu ili kuepuka maambukizi, akibainisha virusi vya Covid 19 kuwa bado havijamalizika kabisa.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aligusia maendeleo ya kiuchumi nchini katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, na kusema Serikali imeendelea na juhudi za kutekeleza mipango ya kiuchumi ili kuhakikisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar unaimarika.

“Ilani ilielekeza kuhakikisha mfumko wa bei unabaki katika tarakimu moja na wastani wa pato la kila mwananchi linaongezeka,”alisema.

Aidha, alisema ilani ilielekeza mapato yaendelee kudhibitiwa pamoja na kuwepo nidhamu katika matumizi ya Serikali, kupunguza utegemezi wa wahisani wa maendeleo, misamaha ya kodi isiyokuwa na tija, sambamba na kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Alisema katika kipindi hicho cha miaka 10, Pato la taifa limeweza kukua  kutoka thaamni ya shilingi Bilioni 1.7 (mwaka 2010) hafi kufikia thamani ya shilingi Bilioni 3, ikiwa sawa na mara 1.74, zaidi ya wakati Awamu ya saba ikiingia madarakani.

Alielelza kuwa kasi ya ukuaji uchumi nayo imeongezeka kutoka asilimia 4.3 (2010) hadi kufikia asilimia 7.0 mwaka 2019.

Vile vile, alisema pato la mwananchi nalo limeongezeka kutoka shilingi 942,000 (USD675) mwaka 2010 hadi kufikia shilingi 2,549 (USD1,114) mak 2019, ikiwa sawa na asilimia 170.59.

Aidha, alisema mfumko wa bei ulishuka kutoka asilimia 14.7 (2011) hadi asilimia 2,9 mwaka 2019, na kubainisha hali hiyo imeleta faraja kubwa kwa wananchi kwani wameweza  kupata bidhaa muhimu kwa bei ya kuridhisha.

Hafla hiyo, iliyohudhuriwa na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kasssim Majaliwa, Makamu w aPili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai pamoja viongozi mbali mbali wa serikali, wastaafu na  baadhi ya mabalozi a nchi za nje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles