28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

JANUARI ATOA SOMO MKUTANO WA MAFUTA, GESI

Na ANDREW MSECHU-Dar es Salaam

MAFANIKIO katika sekta ya mafuta na gesi yanategemea uwezo wa Serikali kujua gharama za miradi  kuweza kukokotoa faida ya rasilimali hizo kwa taifa.

Akifungua mkutano wa wadau wa mafuta na gesi  Dar es Salaam jana, Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema uwezo huo ndiyo utakaoainisha faida inayoweza kupatikana na kunufaisha taifa.

Alisema hiyo inatokana na uvunaji wa rasilimali hizo kuwa jambo jipya katika nchi za Afrika, ambazo kutokana na teknolojia duni, kampuni nyingi zinazowekeza zinatoka katika mataifa ya ulaya.

“Bara la Afrika kwa sasa linaonyesha linaelekea kwa kasi katika uchumi wa mafuta na gesi. Tatizo linaloonekana ni suala la gharama za miradi hii ya utafiti na uchimbaji, ambazo kama serikali zisipokuwa makini kuzijua inaweza isiwe na manufaa kwa wananchi,” alisema.

Alisema  suala la kubaini gharama halisi za miradi zinazotumiwa na wawekezaji ambao ndiyo wenye teknolojia ya uchimbaji na miradi mikubwa inayohitajika ndiyo nyenzo muhimu ya kukokotoa namna ya kupata faida.

Alisema Serikali imekuwa ikiendelea kufanya mabadiliko ya sheria na kuweka mipango na mikakati ya kwa ajili ya kuhakikisha matumizi ya rasilimali ya gesi na mafuta yanakua na manufaa kwa taifa.

Makamba alimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, katika ufunguzi wa mkutano huo wa mwaka unaowakutanisha wafanyabiashara wa mafuta na gesi kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Alisema soko la mafuta na gesi duniani linakua kwa kasi hivyo ni vema kujipanga vizuri.

“Pamoja na mwelekeo wa soko kupanda na kushuka katika vipindi tofauti, mwelekeo ni mzuri kwa nchi za Afrika na kwa nchi yetu pia, hivyo suala la muhimu ni sisi kujiandaa tu ipasavyo,” alisema.

Makamba alieleza kuwa kwa sasa, ukiacha vyanzo vingine, taifa linategemea mafuta na gesi kuzalisha asilimia 53 ya nishati yake, ambayo lazima ihusishe sekta binafsi.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi nchini (ATOGS), Abdulsamat Abdulrahim alisema kongamano hilo la pili linahusisha wadau wote wenye miradi ya mafuta na gesi nchini.

Alisema wadau hao kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekusanyika  kuona fursa zilizopo na zinazoendelea kupatikana katika sekta hiyo  kujua namna ya kuwekeza zaidi.

“Kuna zaidi ya mashirika na kampuni 75 kutoka maeneo mbalimbali duniani ambao wengine wamekuja na ndege zao binafsi.

“Wote wenye miradi mikubwa ya mafuta na gesi wako hapa, hivyo Watanzania tunatakiwa tuitendee nchi haki, tujitokeze na sisi na kuchangamkia hizo fursa,” alisema.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alisema Serikali imeweka mazingira mazuri kuhakikisha wadau wote wapya wa masuala ya nishati wanaojitokeza wanapokelewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles