25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Jaji Mkuu ateswa utoaji haki kwa wakati

Kulwa Mzee -Dar es Salaam

MAHAKAMA, wadau na wananchi wametakiwa kutumia sheria, taratibu za kimahakama, utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ili Tanzania iwe nchi yenye hadhi ya kipato cha kati bila umasikini uliokithiri.

Kauli hiyo imekuja huku baadhi ya malalamiko ya wadau kuhusu kukaa kwa muda mrefu mahabusu kwa kile kinachoelezwa kutokamilika kwa upelelezi.

Hatua hiyo inatajwa kama kikwazo cha kutotolewa haki kwa wakati jambo ambalo linasababisha malalamiko kwa mahakama kama chombo cha kutoa haki.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kuhusu Wiki ya Sheria na kilele cha siku hiyo inayotarajiwa kufanyika Dodoma, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma alisema sheria, utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki kwa wakati, ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Alisema Wiki ya Sheria ni mahsusi kwa utoaji wa elimu ya sheria na taratibu za kimahakama, itaambatana na maonyesho yatakayofanyika kuanzia Januari 31 hadi Februari 5 viwanja vya Nyerere Square, Dodoma.

Profesa Juma alisema kutakuwa na matembezi yatakayofanyika Februari mosi na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

“Kilele cha Wiki ya Sheria ambayo ni Siku ya Sheria nchini itafanyika Februari 6 mwaka huu katika kiwanja ambapo jengo jipya la Mahakama Kuu ya Kanda ya Dodoma litajengwa na mgeni rasmi Siku ya Sheria nchini anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

“Maadhimisho haya yanaashiria kuanza rasmi kwa mwaka mpya wa shughuli za mahakama na huwa yanaambatana na kauli ‘uwekezaji na biashara, wajibu wa mahakama na wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji’.

“Maudhui yanatukumbusha kilicho wazi, kwamba, sheria, utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu  katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

“Maudhui yanasisitiza kwa kila mmoja wetu, mahakama, wadau wa mahakama na wananchi kwa ujumla kwamba tutumie sheria, tutumie taratibu za kimahakama, tutumie utawala wa sheria na tutumie mfumo wa utoaji haki kwa  faida ya kufikia lengo moja kuu ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe miongoni mwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati bila umasikini uliokithiri,” alisema Profesa Juma.

Katika mabanda mbalimbali ya maonyesho, wananchi watapata fursa ya kupata elimu na ufumbuzi wa masuala yanayowakabili.

“Wananchi wengi hawajui sheria, hawajui taratibu za kimahakama, hawaelewi lugha ngumu ya kimahakama, Wiki ya Sheria ni wakati mzuri sana kwa wananchi kuongeza uelewa na ufahamu wao wa sheria na taratibu za kupata haki mahakamani.

“Mahakama ya Tanzania inaamini wananchi wakifahamu taratibu za mahakama, kesi zao zitamalizika haraka na hii ni faida sio tu kwa muda wao, bali pia kwa biashara zao, uwekezaji na shughuli zao za kijamii,” alisema Profesa Juma.

Baadhi ya mambo yatakayotolewa elimu ya sheria ni pamoja na taratibu za ufuanguaji wa mashauri, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, taratibu za mashauri ya mirathi, jinai, madai, ndoa na msaada wa kisheria.

Profesa Juma alisema katika karne ya 21, utoaji haki utafanikishwa kwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), wananchi watapata elimu kuhusu mfumo wa kielektroniki wa kusajili na kuratibu mashauri ambao utazinduliwa katika kilele cha Wiki ya Sheria.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,526FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles