29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM afichua siri ya kumnusuru Naibu Waziri Mambo ya Ndani

Nora Damian -Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kuanza kushughulikia mkataba wa makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji wenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni moja ulioingiwa kinyume cha taratibu.

Pia amemkabidhi nyaraka mbalimbali zinazohusu mkataba huo, huku akieleza sababu za kutomwondoa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Masauni.

Simbachawene aliapishwa jana kubeba mikoba hiyo akitokea Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), baada ya Kangi Lugola kung’olewa wiki iliyopita.

Akizungumza jana, Rais Magufuli alimtaka Simbachawene akaibadilishe wizara hiyo kadiri atakavyoweza na kuwaondoa watendaji wasiofaa na wale wanaopaswa kupandishwa wapandishwe.

“Mkataba wa ovyo kaanze nao, nakupa tahadhari watendaji wako utakaowakuta si kwamba hawayajui.

“Naibu Katibu Mkuu amehusika sana tangu kuanza kwake mpaka mwisho na watendaji wengine Jeshi la Zimamoto,” alisema Rais Magufuli.

Alisema watendaji waliokuwa wakienda kwenye majadiliano ya mkataba huo walikuwa wakilipwa posho ya vikao, safari na kompyuta mpakato (laptop).

“Wengine wanakwenda wakishakaa kwenye kikao wanalipwa Dola 500 ya ‘seating allowance’, Dola 300 ya safari, wanapewa na laptop.

“Kwanini unayejadiliana naye akupe Dola 800, kwanini akununulie laptop, kwa akili za kawaida tu mtu unaweza ukaelewa, kwamba hapa kuna kitu cha ajabu kinafanyika, lakini watendaji wako hawakuliona mpaka ukasainiwa mkataba.

“Wanakwenda kununua ‘drones’, sasa sijui zitahusika kuzima moto, Marekani wala hawatumii. Wanazungumzia mpaka kukopa fedha kwenye benki za nje… kwenye mkataba huu palikuwepo vitu vya ovyo,” alisema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, mazungumzo ya mkataba huo yalianza Aprili mwaka jana na Julai ndiyo yalipamba moto, lakini wakati huo Bunge wala Wizara ya Fedha hawakuwahi kutaarifiwa.

“Waziri Lugola ananiandikia tu barua nithibitishe uendelee, nasema nithibitishe kitu gani wala sikijui,” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia wizara hiyo imehusika kwenye kashfa nyingi na kwamba licha ya viongozi wake kuonywa mara kadhaa wajirekebishe, lakini bado madudu yameendelea kuwepo.

“Wizara ya Mambo ya Ndani imehusika kwenye mambo ya ‘scandal’ mengi, wamekuwa wakiambiwa warekebishe, mawaziri wote huwa nawaeleza, lakini sifahamu huwa kuna mdudu gani pale.

“Nakupeleka wewe (Simbachawene) nenda kayasimamie, unaenda kwenye wizara nafikiri ina mapepo, sasa mapepo hayo yasikuingie, kawe mkali kasimamie, na mimi najua utaweza, ugumu utauleta wewe au utaurahisisha wewe,” alisema Rais Magufuli.

SABABU ZA KUMWACHA MASAUNI

Rais Magufuli alieleza sababu za kutomwondoa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni licha ya wiraza hiyo kukumbwa na kashfa kadhaa.

Mbali ya Lugola, aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, alijiuzulu kisha akateuliwa kuwa balozi baada ya Rais kufanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri.

Mabadiliko hayo yalizua mjadala, huku baadhi ya watu wakihoji kwanini Masauni ameendelea kuachwa licha ya mawaziri watatu kung’olewa katika wizara hiyo tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.

Hata hivyo, jana Rais Magufuli alisema Masauni hakuhusika moja kwa moja kama ilivyokuwa kwa viongozi wenzake.

“Naibu Waziri (Masauni) anajua ingawaje hakuhusishwa sana, alikuwa anapata nakala za madokezo ila ananyamaza. Kwa sababu ni kidokezo tu saa nyingine anakisoma tu na kukiweka… sifahamu kwanini naye alikaa kimya, lakini hakuhusika sana,” alisema Rais Magufuli.

AJIFUNZE KWA MWINYI

Rais Magufuli alimtaka Simbachawene kufanya kazi kwa kufuata taratibu za vyombo vya ulinzi na usalama huku akimtolea mfano Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi ambaye amekaa muda mrefu kwenye wizara hiyo.

“Simbachawene umezungumza vizuri kwamba huna vyota hata moja, vyombo vya ulinzi na usalama vina namna yake ya kuviendesha.

“Mwinyi amekaa muda mrefu Wizara ya Ulinzi, hawezi kuwatukana mabrigedia, anajua namna ya ‘ku – oparate’… tukifuata utaratibu itatusaidia sana namna ya kufanya kazi,” alisema Rais Magufuli.

Pia alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu, kutatua changamoto zilizopo kwenye wizara hiyo.

“Zungu kafanye kazi, kuna ‘challenge’ (changamoto) nyingi, kuna urasimu kwa wawekezaji, hatuhitaji wawekezaji wafanye ya ovyo, lakini pia tunawahitaji kwa ajili ya Serikali kupata mapato na kutengeneza ajira,” alisema Rais Magufuli.

Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema kuna changamoto kubwa kwenye suala la Muungano, hivyo akamtaka Zungu kuzifuatilia kuhakikisha unaendelea kudumu.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha pande zote mbili zinashinda uchaguzi mwaka huu na Muungano wetu unaimarika na Tanzania inaendelea kusonga mbele.

“Mambo ya Muungano ni makubwa kuliko ya mazingira ingawa na mazingira nayo yana ukubwa wake, pole sana na karibu sana katika wizara yetu,” alisema Samia.

KASHFA NYINGINE

Rais Magufuli pia aliibua kashfa nyingine ambayo imesababisha Serikali kushtakiwa na kudaiwa Dola za Marekani milioni 40.

Alisema ndege ambayo ilikodishwa ATCL, ilipofika uwanja ndege haikutumika na kutakiwa kwenda kuchunguzwa, lakini Serikali imeshtakiwa na inadaiwa Dola milioni 40.

“Mwanasheria Mkuu anakwenda London kwa kesi ya utapeli hivyo hivyo, mikataba kama hii inaiingizia taifa hasara kubwa, tunawaumiza wananchi masikini kwa ‘interest’ za ovyo ambazo hazina masilahi kwa taifa,” alisema Rais Magufuli.

ZUNGU, SIMBACHAWENE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Zungu, aliahidi kupambana na mitumba isiyokuwa na viwango, mifuko ya plastiki na urasimu wa utoaji vibali kwa wawekezaji.

“Nilipokuwa nakuja watu waliniuliza nitavaa nguo za mitumba au nitavaa kitu kipya… nimenunua suti mpya.

“Wizara hii ni ngumu, kuna changamotyo kwenye wizara, utendaji wa NEMC (Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira) umepiga vita mifuko ya plastiki, lakini sasa inarudi kwa njia za pembeni.

“NEMC kwanini vitu hivi bado viko nchini, vinapita kwenye mipaka, hili tutalifanyia kazi kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kuanzia vizazi vya sasa na vya kesho,” alisema Zungu.

Alisema pia wawekezaji wote waliotimiza masharti waende haraka kuonana na mamlaka husika wapate vibali ili kusiwe na kikwazo cha kuifanya Tanzania ishindwe kuendeleza viwanda.

“Urafiki upo, lakini kwenye kazi za umma hatutafanya urafiki, tukikutana nje tutaendeleza urafiki wetu,” alisema Zungu.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Simbachawene alisema ataviheshimu vyombo vya ulinzi na usalama na kuviacha vifanye kazi, lakini ikitokea vikafanya makosa atamtaarifu rais.

“Mimi si amiri jeshi mkuu, nitaviheshimu vyombo vifanye kazi yake, vitakapofanya makosa kazi yangu ni kukutaarifu kwamba kuna mambo hayaendi salama,” alisema Simbachawene.

Alisema pia atahakikisha vyombo hivyo vinashiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuzalisha na kufanya shughuli zitakazopunguza kero katika jamii.

MABALOZI

Rais Magufuli alisema mabalozi wapya wameaminiwa kutokana na uadilifu wao, hivyo aliwataka wakafanye kazi kwa bidii huku wakitangaza mazuri ya Tanzania.

“Ninyi nyote mnaijua Tanzania, mkawe watetezi wa Tanzania, mengine yanazungumzwa ya ovyo, lakini ninyi mkayasemee. Wengine msiwajibu, muwe ‘mnawa–ignore’.

Akimzungumzia Balozi wa Tanzania – Geneva, Maimuna Tarishi, alisema licha ya kwamba alikuwa amestaafu, lakini amepewa jukumu hilo kutokana na rekodi nzuri ya utendaji wake alipokuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Tunajua ulistaafu, lakini kazi yako inajulikana, uadilifu na uchapakazi wako tumeona hatuwezi kukuacha ukastaafu, ukatusaidie kwenye mashirika zaidi ya 40 kule Geneva,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, aliwataka mabalozi hao kukemea upotoshaji unaoendelea kwamba kuna ubaguzi wa elimu kwa wasichana.

“Sisi tunajali elimu ya wasichana wote na wale ambao kwa sababu mbalimbali wanaacha masomo, Serikali imekuja na njia mbadala kuhakikisha wanapata elimu,” alisema Profesa Kabudi.

Mabalozi wengine walioapishwa jana na nchi wanazokwenda kwenye mabano ni Profesa Kennedy Gastorn (Umoja wa Mataifa, New York) na Hussein Katanga (Japan).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles