30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ACT Wazalendo yatangaza uchaguzi wa viongozi

Andrew Msechu -Dar es Salaam

CHAMA cha ACT Wazalendo kimetangaza uchaguzi wa nafasi za juu katika chama hicho, ikiwemo ya Kiongozi wa Chama, Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu na nafasi za wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu, alisema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kuwania nafasi hizo na zile za jumuiya za chama ulianza jana na utakamilika Februari 26.

Semu alisema katika uchaguzi huo wa pili kitaifa tangu kuasisiwa kwa ACT Wazalendo baada ya uchaguzi wa kwanza Machi 2015, chama hicho kitaendelea kupigiwa mfano kwa kujali demokrasia, haki, usawa na uzalendo na kuheshimu uhuru wa mawazo na vitendo na uchaguzi huu utajikita kwenye misingi wanayoiamini.

“Ofisi yangu inawatangazia wanachama wote wa ACT Wazalendo nchini kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba nafasi mbalimbali za uongozi wa ndani ya chama ngazi ya taifa na ngome za vijana, wanawake na wazee unaanza leo (jana) Januari 27,” alisema Semu.

Alisema wanachama hai wa ACT Wazalendo wanaruhusiwa kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi zote zilizotangazwa, pale wanapoona wanastahili kuanzia ya Kiongozi Mkuu na baada ya kurejesha fomu, jukumu la kuchuja wagombea litabaki kwa Kamati ya Uchaguzi.

“Wanachama wote wanaruhusiwa kuomba kuwania nafasi yoyote ambayo wanaona kuwa wanataka na wana sifa. Sasa mambo mengine ya kuchuja fomu zitakazorejeshwa yatakuwa chini ya Kamati ya Uchaguzi ambayo itakuwa ikisimamia mchakato wa uchaguzi huo kwa uwazi,” alisema Semu.

Alisema nafasi zinazowaniwa ni pamoja na naibu Kiongozi wa Chama, Makamu Mwenyekiti Taifa-Tanzania Bara, Makamu Mwenyekiti Taifa-Zanzibar, wajumbe wa Halmashauri Kuu nafasi 15 na wajumbe wa Kamati Kuu nafasi nane.

Semu alisema nafasi zingine ni Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake na makamu wake wawili, Katibu wa Ngome na naibu wake, wajumbe watatu wa Halmashauri Kuu Taifa na wajumbe watano wa Mkutano Mkuu Taifa wa ngome hiyo.

Alisema katika Ngome ya Vijana Taifa, nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Ngome, makamu wake wawili yaani wa Bara na wa Zanzibar, Katibu wa Ngome na naibu wake, wajumbe watatu wa Halmashauri Kuu Taifa na wajumbe watano wa Mkutano Mkuu Taifa.

“Katika Ngome ya Wazee Taifa, pia nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Ngome, makamu wake wawili – wa Bara na wa Zanzibar, Katibu wa Ngome na naibu wake, wajumbe watatu wa Halmashauri Kuu Taifa na wajumbe watano wa Mkutano Mkuu Taifa,” alisema Semu.

Akitoa ufafanuzi, Semu alieleza kuwa mchakato huo wa uchaguzi ulianza jana kwa kufungua milango ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu utakaomalizika Februari 26, ukisimamiwa na Kamati ya Uchaguzi.

Alisema baada ya hapo, kuanzia Machi 7, utafanyika uchaguzi wa Ngome ya Wazee, Machi 8 uchaguzi wa Ngome ya Vijana, Machi 9 uchaguzi wa Ngome ya Wanawake na Machi 14 uchaguzi huo utahitimishwa kwa kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa juu wa chama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles