23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

IFAHAMU STIEGLER’S GORGE, FAIDA, UPINZANI WA KIMATAIFA

Sehemu ya maporomoko yaliyopo kando ya Mto Rufiji

Na EVANS MAGEGE,

STIEGLER’S Gorge si jina geni masikioni mwa Watanzania, kutokana na uhalisia wa kuwa jina hilo limehusishwa kwenye masuala ya nishati ya umeme kwa takribani miongo minne sasa.

Hata hivyo, inawezekana ufahamu wa jina hilo haumaanishi utambuzi wa asili ya jina la Stiegler’s ndani ya Bonde la Mto Rufiji.

Udadisi wa MTANZANIA Jumapili  kuhusu Stiegler’s Gorge umebaini kuwa, jina hilo ni  la mpelelezi Stiegler, ambaye alikuwa raia wa nchini Uswiss.

Kwa mujibu wa Kitabu cha Tanzania The Limits to Development from Above, ambacho kimeandikwa na Kjell Havnevik, kimeainisha kuwa asili ya jina hilo ni kutokana na tukio la mwaka 1907, ambapo Stiegler alikanyagwa kanyagwa na tembo hadi kufariki dunia.

Inaelezwa kuwa, mpelelezi huyo akiwa katika shughuli za uwindaji ndani ya Pori la Akiba la Selous, alivamiwa na tembo na kuuawa kisha mwili wake kusukumwa mpaka kwenye maporomoko ya maji yaliyopo katika eneo hilo la Mto Rufiji.

Hata hivyo, vyanzo vingine vinadai kuwa, Stiegler hakuuawa na tembo, bali alianguka kwa bahati mbaya ndani ya bonde hilo na kupoteza maisha.

Kwa ujumla simulizi ya kifo cha Stiegler katika eneo hilo la maporomoko ya maji ya Mto Rufiji ndiyo iliyozaa jina Stiegler’s Gorge.

Mtandao wa Kimataifa wa Africantourer unaelezea Bonde la Stiegler’s Gorge kuwa linafanana kwa ukaribu na lile la Canyon la nchini Marekani.

Africantourer unatanabahisha kuwa, Stiegler’s Gorge ni sehemu ya Mto Rufiji ndani ya Pori la Akiba la Selous. Eneo hilo linatajwa kama ‘mpalio mwembamba’ wenye urefu wa kilomita 8, upana wa mita 50 na kina kutoka kilele chake cha maji ni mita 100.

Utafiti wa RUBADA 

Utafiti uliofanywa miaka ya sabini na mwanzoni mwa miaka ya themanini (1978-1980) na Shirika la Kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (RUBADA ) kwa kushirikiana na kampuni ya kigeni ya M/s Norplan/Hafslund, ulionyesha kuwa mradi wa Stiegler’s Gorge una uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme mwingi wa maji (hydro-power) zaidi ya umeme ambao Tanzania inahitaji.

Matokeo ya utafiti huo pia yalionyesha kuwa mpalio wa Stiegler’s Gorge una uwezo wa kuhimili mitambo mitatu mikubwa ya kuzalisha umeme.

Mtambo wa kwanza ukizalisha megawati 400 ambao ungefungwa upande wa Kaskazini mwa bwawa, mtambo wa pili ungekuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 800, ambao ungefungwa upande wa chini ya bwawa, na mtambo wa tatu  wenye uwezo wa kuzalisha megawati 900 ambao ungefungwa upande wa kusini mwa bwawa.

Kwa ufupi, jumla ya megawati 2,100 zingezalishwa kutoka Stiegler’s Gorge; kiasi ambacho ni karibu ya mara mbili ya kinachohitajiwa

Faida ya Stiegler’s Gorge

Leo hii linapotajwa jina la Stiegler’s Gorge, fikra za Watanzania zinajielekeza kwenye faida moja tu ambayo ni ukombozi wa uchumi wa taifa hili.

Faida hiyo si nyingine, bali ni nishati ya umeme. Kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli amekuwa na shauku ya kutengeneza bwawa la maji kwenye bonde hilo, ambalo litakuwa na  uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 za umeme.

Kusudio hilo si geni, bali ni mwendelezo wa kutimiza dhamira ambayo aliiweka Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, takribani miongo minne iliyopita. Mwali Nyerere alikuwa na wazo la kujenga bwawa la umeme katika eneo hilo ili kusaidia nchi kupata umeme wa kutosha.

Stiegler’s Gorge, ambayo kwa mujibu wa taarifa ya satellite inapatikana umbali wa kilomita 185 kutoka jijini Dar es Salaam, kwa sasa inaangaliwa kama kitovu kitarajiwa cha kuimarisha mzizi mkuu wa  uchumi wa nchi huko tuendako.

Kama mradi huo utakamilika utazalisha umeme maradufu ya unaozalishwa sasa na mazingira hayo yatasaidia kupatikana umeme wa uhakika kwa nchi nzima.

Kwa muktadha huo, dhamira ya sasa ya Rais Magufuli inakusudia kuwapo kwa nishati ya umeme inayojitosheleza ili kukidhi dira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ambao ni mhimili mkubwa wa lengo la nchi kuingia kwenye mfumo wa  uchumi wa kati kwa nchi.

Katika kutimiza dhamira ya mradi wa uzalishaji mkubwa wa umeme kutoka kwenye Bonde la Stiegler’s Gorge, Rais Magufuli amesisitiza umuhimu wa kujenga bwawa la kuzalisha umeme kwenye eneo la Stiegler’s Gorge.

Julai Mosi mwaka huu, wakati akifungua maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya  Biashara (Sabasaba), Rais amewaeleza wawekezaji kuwa changamoto ya umeme wa uhakika itakwisha, kwa sababu Tanzania itakuwa na umeme wa megawati kati ya 4,000 na 5,000 pindi mradi wa Stiegler’s Gorge utakapokamilika.

Rais amesisitiza kuwa, mvua inyeshe au jua liwake, atatekeleza mradi huo mkubwa ambao umeshindikana kwa zaidi ya miaka 40 baada ya kuwekewa vikwazo mbalimbali.

Kwa udadisi wa juu juu uliofanywa na gazeti hili, unaonyesha kuwa, chimbuko la wazo la kuwa na mradi wa Stiegler’s Gorge lilipata nguvu zaidi mwaka 1975, wakati  Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipoyapambanua mawazo yake juu ya umuhimu ya kuwa na mradi mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme katika bonde hilo.

Hata hivyo, utekelezaji wa mradi huo ulipata vikwazo vingi, hususan vya uharibifu wa mazingira, ambavyo viliibuka kila panapokaribia utekelezaji wa mradi huo, tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza mpaka hivi sasa Rais Dk. Magufuli ameazimia kuutekeleza.

Ukimwacha Mwalimu Nyerere, wamepita marais wengine ambao ni Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na wote kwa sababu hizo na nyingine walishindwa kuutekeleza mradi huo.

Ikumbukwe matumaini ya Watanzania ya kupata umeme wa bei nafuu wa maji wa  Stiegler’s  Gorge yalipata msukumo mpya, Septemba, mwaka 2011 wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo, Bernard Membe na maofisa kadhaa wa Tanzania, walipokwenda Sao Paolo, Brazil na kufanya mazungumzo na wenzao wa huko kuhusu uwezekano wa nchi hiyo kuisaidia Tanzania  katika mradi huo.

Waliporejea nchini, umma ukatangaziwa kuwa mradi wa umeme wa maji wa Stiegler’s Gorge utaanza karibuni, na utatekelezwa na wataalamu kutoka Brazil.

Umma ukaambiwa pia ifikapo mwaka 2015 Watanzania wataanza kuufaidi umeme wa bei rahisi wa Stiegler’s Gorge.

Hata hivyo, mpaka utawala wa awamu ya nne unaondoka madarakani matumaini hayo hayakutimia kama ilivyoahidiwa.

Hatua za mwanzo za JPM

Katika kile kinachoitwa dhamira ya Rais Magufuli ya kutekeleza wazo hilo la Mwalimu Nyerere, Juni 28 mwaka huu alikutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.

Ikumbukwe kuwa, Ethiopia ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotajwa kufanikiwa kuzalisha umeme mwingi unaozidi megawati 60,000 kutoka vyanzo mbalimbali kama maji, upepo, jua na joto ardhini.

Katika maelezo yake, Rais Magufuli alisema mradi huo utakaozalisha umeme wa megawati takribani 2,100 utatekelezwa kwa fedha za ndani, ambazo alisema zipo na kwamba upembuzi yakinifu umekwishafanyika.

Anasema anafahamu zipo kelele nyingi za watu watakaohoji fedha za ujenzi zitakakopatikana, lakini atatekeleza mradi huo na endapo atapata wafadhili wenye masharti nafuu ataungana nao.

Anasema mradi huo ukikamilika, ikichanganywa na megawati 1,460 zinazozalishwa sasa na megawati 600 zinazozalishwa kutoka miradi ya Kinyerezi I, II, III, nchi itaweza kuzalisha megawati 4,000 hadi 5,000.

Upinzani wa kimataifa

Pamoja na serikali kuweka bayana ujenzi wa bwawa la kufua umeme katika eneo la Stiegler’s Gorge kuwa utaathiri asilimia tatu tu ya Pori la Akiba la Selous, baadhi ya mashirika ya kimataifa yamekuwa na msimamo ule ule wa miaka mingi wa kupinga mradi huo kwa hofu ya uharibifu wa mazingira.

Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyama Pori la WWF, katika andiko lake la katikati ya wiki hii linasomeka kuwa, ujenzi wa bwawa la Stiegler Gorge utasababisha uharibifu wa mazingira ya Mto Rufiji kuelekea Bahari ya Hindi.

Maelezo ya WWF yanafafanua kuwa, uharibifu huo utagusa moja kwa moja ardhi ya eneo hilo na maeneo mengine ya pori.

Kwamba ujenzi wa bwana hilo utachukua tani milioni 16.6 kwa mwaka za mmonyoko wa ardhi.

Pia kutakuwapo na madhara ya kemikali zitokanazo na shughuli zitakazofanyika katika eneo hilo.

Mtazamo huo wa WWF unajikita katika tishio la kutokea mmomonyoko mkubwa wa ardhi, kuibuka kwa maziwa, pia hali na kuvurugwa muundo wa delta ya Rufiji.

Katika kulitambua hilo, Rais Magufuli ameweka bayana kuhusu vikwazo vya kimazingira kwa kusema hawezi kusikiliza kelele za watu wa mazingira kwa sababu ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kuhifadhi mazingira, tofauti na inavyofahamika.

“Mbuga ya Wanyama ya Selous ipo Tanzania na wenye maamuzi ya kuchimba bwawa la kuzalisha umeme au la ni sisi,” alisema Dk. Magufuli.

Uhai wa Stiegler’s Gorge na ulinzi wa vyanzo vya maji

Pamoja na kwamba Mto Rufiji una historia ya kupitisha maji kwa mwaka mzima, lakini tayari athari za kimazingira ambazo zinatokana uharibifu wa mazingira zimeanza kujitokeza.

Athari hizo zipo zile za jumla kama mabadiliko ya tabianchi, pia zipo za moja kwa moja, kama shughuli za binadamu kwa maana ya kilimo na ufugaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.

Hali ya mazingira kwa maana ya upatikanaji wa maji kwa mwaka mzima kwenye baadhi ya mito imepungua.

Wataalamu wa mazingira wanasema hali ya maji kwenye mito mikubwa inayoelekeza maji yake katika Mto Rufiji imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka 30 iliyopita.

Bonde la Mto Kilombero, ambalo ndilo linachangia zaidi ya asimilia 60 ya maji kwenye Mto Rufiji, kwa takribani miongo miwili sasa limekumbwa na athari ya kupungua kwa kina cha maji, pia maeneo mengine ndani ya bonde hilo yamekuwa na misimu ya ukame.

Wataalamu wa mazingra wanadai kuwa, Bonde la Kilombero kwa miaka 30 iliyopita lilikuwa na mtandao wa mito zaidi ya 79, iliyokuwa ikititirisha maji misimu yote ya mwaka.

Mtandao huo, sehemu kubwa uliunganishwa na vijito ninavyoingia kwenye mito ya Luhuji, Mnyera, Furua, Mpanga, Kihanzi, Luipa na Ruaha Mkuu ambao unaungana na Mto Kilombero na kumwaga maji yake katika Mto Rufiji.

Inaelezwa kuwa, baadhi ya mito hiyo imepunga maji kwa kiasi kikubwa, hali inayopelekea mito mingine kuwa na wastani wa kukaukiwa maji kwa siku 200 kwa mwaka, tofauti na miaka ya 1980 ambapo mito hiyo ilikuwa na wastani ya kupata ukame kwa siku 12 tu.

Kwa mantiki hiyo, uhai wa Stiegler’s Gorge unategemea pia juhudi za makusudi za kulinda vyanzo vya maji, ili kuhakikisha maji yanaendelea kupatikana kwa wingi ndani ya Mto Rufiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles