SANTURI YA WAPIGA DILI IMEKWISHA UTAMU

1
714

NA MARKUS MPANGALA,

ZIARA zinazofanywa na Rais John Magufuli zimekuwa kiini cha matamshi mbalimbali ambayo anakusudia jamii ifahamu. Maagizo na misimamo ya serikali ya awamu ya tano yamekuwa yakitolewa kwenye ziara zake.

Ninakubaliana naye kuwa ni lazima kusema msimamo wa serikali na kusisitiza iwe kwa lugha kali au upole. Jambo la msingi ni kuhakikisha hadhira inafahamu kuwa serikali yao inafanya nini na mwelekeo wake ni upi.

Miongoni mwa matamshi yaliyozoeleka ni yale ambayo yanasononesha zaidi, hususan masuala ya wizi, utumishi wenye kiwango duni, matatizo aliyoyakuta serikalini na nchi kwa ujumla pamoja na kiwango kikubwa cha kuporomoka kwa maadili ya uongozi.

Vilevile amekutana na kiwango kikubwa cha kuporomoka kwa maadili ya jamii ambayo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ikizoea baadhi ya mambo na kuyafanya kuwa ya lazima.

Rais Magufuli ameonya, ameasa, amesisitiza na kukemea kila alichoweza. Kubwa zaidi analorudia mara kwa mara ni juu ya wizi wa kutisha ambao umewahi kutokea nchini.

Rais amekuwa akitumia neno ‘wapiga dili’ kuelezea kama kiini cha matatizo na utaratibu wa hovyo unaoikabili nchi tangu zamani.

Kila mkutano wake anaibuka na tuhuma za wizi. Akifanya ziara bandarini anazungumzia wizi. Alizuia usafirishwaji wa mchanga (makinikia) na kudai kuna wizi.

Alifanya ziara mkoani Pwani hivi karibuni, ambapo mambo mawili makubwa yalitokea; wizi uliotamalaki na namna alivyopanga kuukomesha na kuwanyoosha wote waliokuwa wakitumia mianya hiyo kujinufaisha.

Tamko la pili akiwa mkoani humo lilikuwa juu ya nafasi ya wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni. Rais alibainisha kuwa serikali ya awamu ya tano haipo tayari kuona mwanafunzi aliyejifungua anarudi shuleni.

Tamko hilo lilikuwa na maana kwamba shule za serikali kote nchini hazitapokea mwanafunzi yeyote aliyebeba ujauzito na kujifungua kisha akataka kuendelea na masomo yake.

Jambo hili limepokelewa kama fimbo kwa baadhi ya Watanzania. Zipo asasi za kiraia ambazo zimepingana na tamko la serikali ya awamu ya tano.

Kimsingi tamko hilo ni kinyume cha ilani ya CCM, ambayo ilidai wanafunzi watapewa nafasi ya kurudi shuleni baada ya kujifungua.

Hoja yangu si suala la wanafunzi kurudi shuleni, kwa sababu ninaamini kuna mambo yanahitajika kurekebishwa ndani ya jamii yetu kabla ya kuishinikiza serikali ikubali shule zake kupokea mwanafunzi aliyepata mimba au kusababisha mimba.

Kwa sasa Rais yuko ziarani mkoani Mwanza (Kanda ya Ziwa). Amezindua miradi ya maji na kutoa hotuba. Hapo ndipo hasa kwenye hoja.

Wakati Rais akiwa kwenye ziara mikoa ya Mtwara na Lindi alizungumzia suala la wapiga dili na wezi. Akiwa mkoani Dar es Salaam hakuacha kuzungumzia jambo hilo.

Akiwa makao makuu ya nchi huko Dodoma alizungumzia suala la wizi uliofanyika nchini au unaotarajiwa kufanyika na namna anavyopanga kuuzuia.

Kila mkutano wake anatawaliwa na manungu’uniko juu ya wizi uliofanyika nchini na namna alivyojipanga kuukomesha.

Mathalani akiwa wilayani Sengerema, amesema kuwa yeye anafahamu siri nyingi za nchi hii kuliko raia yeyote. Ninakubaliana na hilo pasipo shaka, yeye ni raia namba moja nchini.

Aidha, akiwa Sengerema hapo hapo amesema kuwa hana mpango wa kusafiri kwa sasa, ndiyo maana alimtuma Makamu wake, Mama Samia Suluhu, kudhuhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliomalizika hivi karibuni mjini Adis Ababa, nchini Ethiopia.

Rais pia amebainisha kuwa, amealikwa katika nchi 60 duniani, lakini hajakwenda hata moja. Sababu kubwa anayotoa ni kutaka kudhibiti wizi na wapiga dili.

Zipo taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari mapema wiki hii zikimkariri Rais akisema atasafiri nje ya nchi atakapostaafu, lakini kwa sasa haiwezekani.

Binafsi ninatofautiana na hotuba zake, hasa kwenye ‘maudhui’ ya anachokiwasilisha mkutanoni. Kuzungumzia suala la mimba kwa wanafunzi ni muhimu kwa nia ya kuelimisha jamii.

Lakini kuzungumzia suala la wezi na wapiga dili hilo hapana. Serikali ina mkono mrefu. Mimi ni mtiifu mkubwa wa dola na ninapenda watu waiheshimu dola yoyote duniani ili wao wapewe heshima vilevile na dola. Hatuwezi kushindana na dola.

Sasa hivi natamani kusikia Rais anajigamba na kubainisha kuwa mradi fulani umekamilika, mpango fulani umekamilika, huduma fulani imekamilishwa.

Kusema hivyo sikusudii kubeza juhudi za Rais, natamani ifike wakati tuwe tunakwenda kwenye ziara ambazo Rais akizungumza anasema juu ya miradi iliyokamilika kama alivyofanya katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara.

Kama tukijua fulani mwizi au kundi fulani limetekeleza wizi, ni lazima tukubali kupambana navyo.

Santuri ya wapiga dili imekwisha utamu wake. Ninajipa imani kuwa wasaidizi wake wanafahamu kuwa santuri ya wizi! wizi! wizi! wapiga dili haivutii tena, sasa aigeuze santuri azungumzie miradi, mipango na kujigamba kutekeleza jambo.

Ni lazima kila mkoa utatuliwe kero zake ambazo serikali kuu inatakiwa kuzisimamia. Hii itasaidia Rais akifika eneo hilo azungumzie suala la miradi, mipango, utekelezaji na mambo yahusuyo. Lakini kukumbatia santuri ya wizi na wapigadili kwa miaka miwili sasa na nusu inachusha.

Baruapepe; mawazoni15@gmail.com

1 COMMENT

  1. Ni haki ya kila mtanzania kutoa maoni yake kwa yale anayoona yanafaa kuijuza au kuielimisha jamii, hivyo ni haki ya mwandishi kuelezea alilotaka.Kwa mantiki hii ni haki ya Rais pia kuzungumzia yale anayoona yanafaa kwa watanzania likiwamo hilo la wezi na wapiga dili. Mwandishi kama anaishi Tanzania atakubali kuwa taifa lilifika mahali ambapo wizi hasawa mali za umma ulionekana ni ujanja na alieiba alionekana ndie mwerevu katika jamii na ndio maana ukapewa jina laini la DILI. Itachukua muda mrefu kufikia hatua ya jamii kuuangalia wizi huu kwa jicho tofauti la kuuchukia na ndio maana Rais anaendelea kuwakumbusha na kuwaasa Watanzania kuwa haya yalikithiri na yeye ameapa kupambana na maovu haya.
    Mwandishi kuonyesha kukerwa na haya kunazidi kuthibitisha kuwa kampeni hii ya Rais inazaa bado inatakiwa kuendelea ili kuzidi kuwakumbusha watu mara nyingi inavyowezekana ili wajue kuwa yapo macho bado yanawaangalia wale wanaohalifu. Ni vyema mwandishi pamoja na wale senye mawazo kama yake wakawa wavumilivu tu kwa kukubali kusikia wasichopenda maana vita hii bado haijakwisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here