22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

HUN SEN: Kubwa lao lililoidhibiti Cambodia kiganjani

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

‘UKUU wangu usiopingika haukutokana na nguvu zangu binafsi bali udhaifu wao,’ ni kauli ya kukumbukwa iliyojaa dharau na nyodo kutoka mdomoni mwa Waziri Mkuu mwenye nguvu wa Cambodia Hun Sen miaka mingi iliyopita.

Aliitoa kauli hiyo akijibu siri ya mafanikio yake ya kudumu muda mrefu kuliongoza taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Asia kwa mkono wa chuma bila kupingika au fulani kuinua sauti ya kumpinga.

Katika hilo alimaanisha maadui wake ni watu dhaifu wasio na uwezo au ubavu wa kukabiliana naye kwa njia yoyote ile iwe ya heri au shari.

Sen aliye madarakani tangu mwaka 1985 na ambaye ni mmoja wa mawaziri wakuu waliotawala muda mrefu zaidi duniani.

Anasifiwa kwa kusaidia kupaisha uchumi na kuleta amani na utulivu baada ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na uliokuwa utawala dhalimu wa Khmer Rouge, ambao unahusika na moja ya mauaji makubwa kabisa ya watu katika karne ya 20.

Lakini Hun Sen (68) pia anaonekana kuwa mtawala wa kiimla mwenye rekodi mbaya ya haki za binadamu na yu tayari kusambaratisha mara moja changamoto yoyote ya kisiasa itakayomkabili.

Haoneshi dalili za kustaafu na Juni mwaka jana (2018), aliapa kutawala kwa miaka mingine zaidi ya 10 ilhali tayari yu madarakani kwa miaka 34 sasa.

Chama chake tawala cha Cambodian People’s Party (CPP) kimeidhibiti nchi kwa miongo kadhaa, lakini katika mwongo huu, kimekuwa kikikabiliwa na chaguzi zenye upinzani mkali.

Hata hivyo, kilienda katika uchaguzi mkuu wa mwisho wa Julai 2018 bila ushindani baada ya chama kikuu cha upinzani cha Cambodia National Rescue Party (CNRP) – kuvunjwa.

Chama hicho kililichomsumbua sana kilivunjwa kwa amri ya Mahakama lakini kwa ushawishi wa kina Hun na CPP kwa madai ya jinai na uhaini wa viongozi wake. Viongozi wake akiwamo mkuu mpya Kem Sokha walikamatwa na wengine kuikimbia nchi.

Kutokana na CNRP iliyokuwa tishio kuharamishwa chaguzi za mwaka jana zilikataliwa na Serikali za Umoja wa Ulaya na Marekani zikisema hazikuwa halalli.

Hun Sen, ambaye amekuwa akikabiliwa na miito ya kuwekwaa vikwazo lakini hajali hilo na anaonekana kujiimarisha na moja ya vitu vinavyompa kiburi ni sapoti kubwa ya China.

Wachambuzi wa mambo wanasema anwaandaa wanawe watatu, ambao wote wanashikilia nyadhifa zenye nguvu chamani, jeshini au serikalini ili mmojawapo hususani Jenerali Hun Manet awe tayari kumrithi wakati atakapong’atuka.

Changamoto zilizoanza kumkabili kwa nguvu mwongo huu ni za kila aina, zisizotarajiwa, lakini pia zenye kudhihirisha kwamba lolote hutokea pale wanyonge wanapochoka kukandamizwa kwa mno.

Kabla ya kuharamishwa kwa CNRP alikuwa akikabiliwa na nguvu ya umma kuanzia maandamano ya upinzani hadi migomo ya wafanyakazi, ambayo inakumbushia nguvu alizotumia mwaka 1998.

Waliandamana katika mitaa ya mji mkuu, Phnom Penh wakipiga ngoma, filimbi, miluzi na kupaza sauti ‘Hun Sen, kwenda zako.’

Sen akaingiwa na hofu kwa namna majeshi yake yanavyoshughulikia maandamano na migomo hiyo tangu chama cha upinzani cha Cambodian National Rescue Party (CNRP) kilipoyaitisha.

Wafuasi 20,000 wa CNRP walikuwa wakiandamana kila siku kabla ya idadi kufikia 50,000 wakati wafanyakazi na wakulima walipojiunga nayo.

CNRP ilikuwa pamoja na mambo mengine ikishinikiza kuitishwa kwa uchaguzi mpya kufuatia chaguzi zenye utata na kasoro nyingi zinazokibakisha madarakani chama chake hicho.

 Kukiwa na viwanda zaidi ya 560 vinavyoajiri wafanyakazi 800,000, sekta ya nguo ya Cambodia ni sekta kubwa kuliko zote nchini humo ikitengeneza mapato ya dola bilioni tano kwa mwaka na kuchangia asilimia 80 ya mauzo yote ya nje ya taifa hilo.

Sehemu kubwa ya viwanda hivyo ilikuwa ikifungwa mara kwa mara, hali iliyoiumiza kichwa serikali kutokana na upotevu wa mapato.

Wakati vikosi vya usalama vikionesha tahadhari katika kuchukua hatua na kuonesha uvumilivu kila maandamano yanapoibuka, dalili za kupotea uvumilivu zikajionesha kwa kadiri ya miaka.

Mshauri Binafsi wa Hun Sen, Ros Chantrabot,alionya upinzani unaendesha ‘siasa za kunyonga’ kwa kushinikiza kujiuzulu kwa waziri mkuu.

 “Wanaenda mbali mno. Wanatengeneza tatizo moja baada ya lingine. Wanapaswa kuja kwenye meza ya mazungumzo kutafuta suluhu ili kuepusha kuibuka kwa machafuko makubwa na kuigawa nchi.”

Kauli yake kwa jicho la haraka inaonekana Hun Sen anahofu na vuguvugu pamoja na uwezekano wa kuamuru kutumika kwa nguvu kubwa, kitu ambacho pia anahofia kitaigawa nchi.

Mwaka 1997, askari watiifu kwa Hun Sen na CPP walipigana vita kali na kuyashinda majeshi tiifu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu mwenza Norodom Ranariddh, ambaye chama chake kilishinda uchaguzi uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1993.

Uchaguzi huo ndio uliohitimisha vita ya wenyewe kwa wenyewe ya miongo zaidi ya miwili iliyoichana chana nchi ikiwamo kipindi kinachonuka damu cha Pol Pot cha 1975-1979 kilichoshuhudia watu milioni mbili wakifa.

Hun Sen tayari analo jeshi la kisasa lililofuzu vyema linalojulikana Kikosi cha Ulinzi wa Waziri Mkuu (PMBU), ambacho kinaaminika kuwa na askari zaidi ya 10,000 na ambacho kazi yake kuu ni kumlinda Hun Sen kwa uaminifu.

Waziri Mkuu huyo wa Cambodia yuko madarakani tangu enzi za Ronald Reagan katika Ikulu ya Marekani miaka ile ya 1980 na kwa kauli yake aliwahi kusema hatarajii kung’atuka hadi atakapofikisha umri wa miaka 90.

Hun Sen anahesabiwa kuwa mmoja wa wanasiasa wa Asia wafuasi wa farsafa ya Machiavelli.

Wana-Machiavelli, ni wanasiasa wanaotumia zaidi werevu, hila na udanganyifu kudumisha mamlaka zao na kutekeleza sera za utawala wao.

Hu Sen huhakikisha yeyote yule anayetishia utawala wake anaozea jela au kukimbilia uhamishoni.

Kipindi chote ilichopitia nchi yake kuanzia vita ya wenyewe kwa wenyewe, mchakato wa amani wa Umoja wa Mataifa (UN) na chaguzi kadhaa, kada huyo wa zamani wa kikomunisti daima alihakikisha anafanikiwa kuwa juu kabisa katika uongozi wa nchi.

Kipindi cha mwongo mmoja uliopita, pia alisimamia ukuaji wa uchumi na utulivu katika nchi iliyogubikwa na umasikini uliotopea na karibu iharibiwe na ‘viwanja vya mauaji’ vya uliokuwa utawala katili wa kikomunisti wa Khmer Rouge.”

Wakati wa ziara ya aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama mwaka 2014, Hun Sen alitetea rekodi yake ya haki za binadamu, akimwambia Obama kuwa Cambodia ina mazingira ambao yanaifanya iwe na sera ilizo nazo, na alieleza shauku ya nchi yake kuimarisha uhusiano na Marekani.

“Hun Sen ni mwerevu, mwenye akili, mjeshi, mwingi wa mbinu na anayejitegemea kimaamuzi,” anasema mwanahistoria David Chandler, mtaalamu wa Cambodia katika Chuo Kikuu cha Monash nchini Australia na ambaye ni mkosaji wa utawala wa Hun Sen.

 Siku hizi, Hun Sen amejitengenezea staili yake kama baba mkongwe wa taifa na amedhamiria kupata heshima kimataifa sambamba na sifa ya kukuza uchumi.

 Pamoja na wasiwasi kuhusu staili yake ya utawala wa kiimla na iliyojaa ukiukaji wa haki za binadamu, mwerevu Hun Sen amefanikiwa kudumisha mmiminiko wa misaada ya kimataifa ambayo bado inachangia sehemu kubwa ya bajeti ya taifa la Cambodia hususani kutokea China.

Lakini wakosoaji wengi wanasema mara nyingi kile Hun Sen anachothubutu kufanya ni matumizi ya nguvu kubwa na kuingilia mahakama ili kuhakikisha anabaki madarakani.

“Utawala wa kikatili na machafuko wa Hun Sen kwa zaidi ya miongo mitatu  umesababisha mauaji yasiyomithirika na ukiukaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu ambao umepita bila kuchukuliwa hatua,” Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch lenye makao makuu mjini New York lilisema katika ripoti yake mwaka jana.

Viongozi wa wafanyakazi, wanasiasa, waandishi wa habari na wanamazingira ni miongoni mwa watu waliouawa kikatili na utawala wake kwa miaka mingi.

Pamoja na yote hayo, Wacambodia wengi bado walikuwa wakimwagia sifa kwa kuindoa nchi yao katika kile ambacho wanaona jehanamu la utawala wa Khmer Rouge.

 Utawala huo wa kipindi kile cha Pol Pot ulikuwa ukilazimisha ‘jamii safi’ ya kilimo kama njia pekee ya mfumo wa maisha.

 Baadaye Vietnam ikaivamia nchi hiyo mwaka 1979 na kuupindua utawala huo usiosahaulika, na Cambodia ikawa imevunjika vipande vipande: kila taasisi ya kisiasa, kijamii na kiutamaduni ilikuwa shaghalabaghala.

 Akiwa amezaliwa katika familia ya wakulima wadogo mashariki ya kati mwa Cambodia, Hun Sen awali alishiriki katika jeshi la Khmer Rouge dhidi ya serikali iliyoungwa mkono na Marekani.

Akapoteza jicho vitani.

Lakini akakimbilia Vietnam mwaka 1977 na kuungana katika uvamizi wa Wavietnam. Kufikia mwaka 1985, akatangazwa kuwa waziri mkuu.

Lakini, kwa miaka mingi baada ya kuanguka kwa Khmer Rouge, Marekani bado iliendelea kuwatambua viongozi wake, ambao walikimbia na kuanzisha vita ya msituni, kama wawakilishi halali wa Cambodia katika Umoja wa Mataifa (UN).

Hali hiyo ilimuuma Hun Sen, ambaye mara nyingi alilieleza hilo wakati alipohisi anaonewa na sera za Marekani.

Ametengeneza ushirika muhimu na China ambayo imekuwa ikimwaga kwa moyo mweupe misaada na uwekezaji kwa mshirika wake huyo wa hakika kisiasa.

 Ndiyo maana huwakaribisha viongozi wa China kwa heshima kubwa na bashasha tofauti na wale wa Marekani.

 Sifa ya Hun Sen kupenda ubabe na vurugu ilijidhihirisha wazi wakati alipoendesha mapinduzi dhidi ya serikali yake mwenyewe ya ushirika mwaka 1997 kama tulivyoainisha hapo juu.

 Majeshi tiifu kwake yaliyashinda yale ya waziri mkuu mwenza — ambaye chama chake ndicho kilichoshinda chaguzi zilizofanyika miaka minne kabla na kumpa Hun Sen kwa mara nyingine madaraka kamilifu.

 Kwa kutumia kila njia, amefanikiwa kubakia madarakani tangu hapo akishinda chaguzi baada ya chaguzi.

 Katika miaka ya hivi karibuni, wapinzani wa Hun Sen wamekuwa wakijikuta mbele ya hakimu zaidi kuliko kukabiliana na mtutu wa bunduki, makundi ya haki za binadamu yanasema.

 Kiongozi wa upinzani Sam Rainsy — aliyekuwa mwanasiasa pekee wa Cambodia mwenye uwezo, bashasha na rasilimali za kumwangusha Hun Sen — amekimbilia uhamishoni kuepuka kifungo cha miaka 12 jela baada ya kutiwa hatiani katika kile wakosoaji wanachosema uthibitisho wa mateso ya kisiasa yaliyomo nchini humo.

Maendeleo ya kiuchumi ni moja ya mambo yaliyokuwa yakiipa kiburi serikali ya Hun Sen, ukichukulia pale ilipoanzia na jinsi ambavyo utawala wa Khmer Rouge ulikuwa umeharamisha matumizi ya fedha.

 Msemaji wa Baraza la Mawaziri nchini humo Phay Siphan anaeleza kuwa Cambodia imeshuhudia ukuaji wa uchumi kipindi cha miaka 10 iliyopita na inatarajia kuendelea na kuwa na kipato cha dola 1,000 kwa kichwa mwaka  2013.

Anadai Hun Sen ‘ni mtu sahihi na katika wakati muafaka kwa ajili ya kuelekea soko huria na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

“Serikali ilipitisha sheria ya kwanza ya kupambana na rushwa ambayo pia inahitaji maofisa kutangaza mali zao, Phay Siphan alisema.

 Sheria hiyo, hata hivyo haijazuia kushamiri kwa biashara miongoni mwa familia za vigogo, upendeleo na rushwa.

 Wanasiasa wa upinzani na makundi ya kupambana na rushwa kama vile Global Witness yanamtuhumu Hun Sen kwa kusimamia uuzaji wa misitu kwa kampuni za magogo na kuwafurusha wakulima wengi wadogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles