23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya NMB yaahidi kusaidia wakulima wa zabibu

MWANDISHI WETU-DODOMA

Benki ya NMB imekubali kusaidia wakulima wa zao la zabibu mkoani Dodoma, ikiwa ni juhudi za kuunga mkono mpango wa serikali wa kuwainua wakulima.

Ahadi hiyo ilitolewa jijini Dodoma jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NMB,  Albert Jonkergouw, katika hafla fupi ya benki hiyo kwa taasisi za serikali, viongozi wa taasisi na wafanyabiashara.

Mkurugenzi huyo alisema nguvu kubwa imeelekezwa kwa wakulima kutokana na sera ya Tanzania ya viwanda, lakini akasifu mpango wa serikali kuhamia Dodoma ambao umeungwa mkono na benki hiyo.

Jonkergouw alisema katika kuunga mkono uhamiaji Dodoma, NMB wameshapeleka tawi la benki tembezi katika mji wa kiserikali Mtumba na kwamba mipango ya baadaye ni kufanya maboresho makubwa ya huduma za benki katika eneo hilo.

“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za serikali kwa kila hali, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara,  mimi niseme kuwa benki hii ni mali yenu, mna haki ya kuitumia, nasi ni wajibu wetu kuwahudumia,” alisema Mkurugenzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, aliomba uongozi wa NMB kuutazama Mkoa wa Dodoma kwa jicho la pekee kutokana na ongezeko la watu kutokana na ujio wa makao makuu.

Dk. Mahenge aliomba benki hiyo irahisishe masharti katika upatikanaji wa mikopo, ikiwamo kuwapa kipaumbele zaidi wakulima wa zabibu, zao linalotajwa kuwa mkombozi kwa wenyeji wa mkoa huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini hapa, Dk. Alfonce Chandika, alisema Benki ya NMB ni rafiki kwa makundi yote kutokana na huduma zake kuyagusa makundi yote.

Dk. Chandika alisema kwa sasa huduma zinazotolewa na benki hiyo zinapaswa kuwa mfano kwa taasisi nyingine, jambo litakalotoa tafsiri chanya kwa Tanzania ya viwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles