25.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 30, 2022

Contact us: [email protected]

Huduma ya kujipima TB mwenyewe kwa njia ya simu yazinduliwa


Na VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM

Serikali imezindua huduma za Kifua Kikuu (TB) kwa njia ya mitandao ya simu za mkononi (Mobile Health) ambapo sasa kupitia njia hiyo wananchi wataweza kujichunguza wenyewe iwapo wanakabiliwa na maambukizi ya ugonjwa huo au la.

Aidha, imezindua mfumo wa kusajili na kufuatilia wagonjwa kwa njia hiyo ambao utatekelezwa katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Arusha, Geita na Mwanza.

Mifumo hiyo imeandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) kwa kushirikiana na Path Tanzania/KNCV -challenge TB na Cardno-MHealth PPP Tanzania.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, wakati alipokuwa akizindua huduma hiyo mpya ya upimaji.

Alisema hatua hiyo imelenga kuongeza kasi ya uibuaji wa wagonjwa wapya wenye maambukizi ya ugonjwa huo nchini.

Alisema ugonjwa wa TB unashika nafasi ya tisa kwa kusababisha vifo duniani, ni ugonjwa pekee wa kuambukiza unaoongoza, ukifuatiwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Alisema inakadiriwa mwaka 2016 watu milioni 10.4 duniani waliugua TB, watu milioni 1.7 walifariki dunia.

“Kwa mujibu wa ripoti ya TB ya Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2017 Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye wagonjwa wengi wa TB.

“Takwimu za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) za mwaka 2017 zinaeleza waligundulika wagonjwa wa TB 69,818, asilimia 90 walitibiwa na kupona.

“Hata hivyo, inakadiriwa kuwa, wagonjwa wanaofikiwa ni asilimia 44 tu, yaani kuna wagonjwa 84,000 wenye TB ambao wapo kwenye jamii wanaendelea kuambukiza,” alisema.

Alisema changamoto iliyopo ni kwamba inakadiriwa kila mwaka Watanzania 27,000, sawa na watu 74 kila siku, sawa na watu watatu kila saa hufariki dunia kwa TB.

Awali akizungumza, Mratibu wa Uhamasishaji Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma wa Wizara hiyo ya Afya, Agatha Mshanga, alisema mifumo hiyo ni huduma ya uchunguzi binafsi wa TB na matibabu pamoja na elimu kuhusu TB.

“Lengo kuu ni kuongeza uibuaji wa wagonjwa na kuboresha upatikanaji wa huduma ya kujichunguza itakuwa kwa nchi nzima,” alisema.

Alisema jumla ya watoa huduma 520 wamepatiwa mafunzo jinsi ya kuwasajili wagonjwa hao pamoja na watoa huduma wa kujitolea katika ngazi ya jamii 200 wamefundishwa.

lisema namba ambayo itatumika kufanya uchunguzi binafsi ni *152*05#, kisha chagua nambari sita na ufuate maelekezo kujibu maswali yanayoulizwa kupitia mfumo huo.

Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk. Beatrice Mutayoba, aliishukuru mitandao ya simu za mkononi, Vodacom, Tigo na Airtel iliyokubali kufanya huduma hiyo, ambayo itakuwa bila malipo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles