28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE, MAALIM SEIF WATAKA JPM AWATIMUE WALIOSABABISHA KIVUKO KUZAMA

Na EVANS MAGEGE


MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, amemtaka Rais Dk. John Magufuli achukue hatua kwa watu wote waliohusika na uzembe uliosababisha Kivuko cha Mv Nyerere kuzama Ziwa Victoria.

Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kutokana na tukio hilo, Rais Dk. Magufuli anatakiwa kuwachukulia hatua watu waliofanya uzembe huo, kama anavyofanya kwa wengine.

Alisema pasipo kujali vyama vya siasa, msiba huo ni wa kitaifa, hivyo aliwataka Watanzania kupiga kelele ili watu wawajibishwe kwa uzembe.

“Tunamtaka Rais achukue hatua awawajibishe… amewawajibisha watu wengi kwa makosa ambayo alidai ni kupambana na ufisadi na kadhalika, katika hili tunamtaka achukue hatua na asiseme sichukui hatua kwa sababu Mbowe katoa kauli, lakini ajue nimezungumza kama Mtanzania ambaye nina uchungu na Watanzania ambao wanakufa.

“Lazima tufike mahali ambako wale waliopewa wajibu wa kuhakikisha maisha yetu yanakuwa salama wanachukuliwa hatua,” alisema.

Mbali na hilo, Mbowe pia alisema serikali inatakiwa kutangaza idadi ya watu, majina pamoja na mizigo yao iliyokuwamo katika kivuko hicho.

“Huu ni msiba wa kitaifa, inampasa Rais azungumze na Watanzania, isitoshe kwa Msigwa wa Ikulu kupeleka taarifa TBC kwamba Rais anatoa pole, Rais azungumze na Watanzania awape pole na tunategemea akizungumza na Watanzania atatambua msiba huu kuwa ni wa Taifa na kutoa maelekezo ya maombolezo ya kitaifa,” alisema Mbowe.

Mbowe pia aliitaka Serikali kulipa fidia kwa watu wote waliopoteza maisha na mali zao katika kivuko hicho.

Alisema utaratibu wa kawaida wa vyombo vya usafiri, mfano mabasi, magari  hukatiwa bima, hivyo kivuko kinachobeba roho za watu lazima kuwapo na utaratibu wa bima ili wanapopoteza maisha, familia zao zilipwe fidia.

Alisema taarifa alizonazo kivuko kilichozama kilikuwa na maboya machache, hivyo kusababisha watu wengi kupigania na kujikuta wanakufa maji.

Kwamba maboya machache yaliyokuwapo yalikuwa yamefungiwa katika moja ya vyumba vya kivuko hicho.

Awali alisema taarifa alizonazo ni kwamba kivuko cha MV Nyerere kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 101 na mizigo tani 20, lakini hadi ajali inatokea kivuko hicho kinadaiwa kuzidisha idadi ya abiria na mizigo.

Alisema kutokana na ajali hiyo, inaonyesha Taifa halina maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na ajali zinazotokana na vyombo vya usafiri wa majini.

“Mtakumbuka mwaka 1996 tulipoteza zaidi ya Watanzania 1,000 kwa ajali ya Mv Bukoba, ilipaswa kuwa funzo kwetu, lakini mwaka 2011 Meli ya Mv Spice Islander ilizama katika Bahari ya Hindi na zaidi ya watu wengine 2,000 walipoteza maisha.

“Mwaka 2012 Meli ya Staget nayo ilizama wakafa abiria mamia kwa mamia, lakini hatukujifunza, sasa jana kivuko kimezama  saa nane mchana, lakini mpaka saa 12 hakuna operesheni yoyote ya uokoaji ya watu wenye taaluma au vifaa vya kuokoa ambavyo vilikuwa vimefika katika eneo la ajali,” alisema.

Alisema watu waliokuwa wanahangaika kuokoa ni wavuvi wadogo wadogo, na kwamba hapakuwapo askari au wanajeshi.

Mbowe alikwenda mbali kwa kuhoji kipaumbele cha nchi, na hata kushangazwa na kauli iliyotolewa na upande wa serikali ya kusitisha zoezi la uokoaji kwa sababu ya giza.

“Kweli tumeshindwa kuwa na taa ya kuokolea watu umbali wa mita 100 kutoka nchi kavu? Tumeshindwa hata kutumia jenereta la kawaida kwa kuipakia kwenye mtumbwi  kisha watu wawashe umeme na kuwamulikia wanaofanya kazi ya kuokoa? Ina maana hapo waliridhika kwamba wote waliokuwa majini wamekufa? Kweli hili jambo linaumiza sana,” alisema Mbowe.

Aliongeza kuwa, nchi haina huduma za uokoaji wa haraka katika maziwa yote makubwa na baharini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles