HONGERA MAYANGA, UMEONYESHA KITU BONDENI

0
523

Na ABDUL MKEYENG-DAR ES SALAAM


KIKOSI cha timu ya soka taifa Tanzania (Taifa Stars) kimerejea nchini kikitokea Afrika Kusini kilipokwenda kushiriki michuano ya Baraza la Mpira wa Miguu nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA) ambako kikosi hicho kilitinga hatua ya nusu fainali na kutolewa na Zambia.

Stars ilienda kushiriki michuano hiyo kama nchi mwalikwa kutoka kwa nchi mwanachama wa Baraza la soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kufika hatua hiyo ambayo tangu Stars ianze kushiriki michuano hiyo haijawahi kufika hatua hiyo. Kiufupi haya ni mafanikio makubwa kwa soka la Tanzania.

Mara zote ambazo timu hiyo iliitwa kushiriki michuano hiyo haijawahi kufika hatua nzuri na kubwa kama ya namna hii. Stars imetolewa nusu fainali kwa kufungwa mabao 4-2 dhidi ya Zambia. Licha ya yote mwaka 2017 katika michuano hiyo unatakiwa kuwa mwaka wa kihistoria kwetu.

Mpaka timu hiyo inakwenda nchini humo kushiriki fainali hizo haikuwa inapewa nafasi ya kufanya vizuri na mashabiki, wadau wa soka. Sababu hiyo ni kutokana na timu yenyewe kupata sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Lesotho mchezo wa kutafuta nafasi za kushiriki michuano ya Mataifa Afrika nchini Cameroon mwaka 2019.

Sare hiyo ya mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, uliwafanya watu hao kutokuwa na imani na kikosi hicho na kila mmoja akiamini Stars imeenda nchini humo kushiriki na sio kushindana kama ilivyo kwa mataifa mengine.

Lakini haikuwa hivi, Stars ilienda kugeuka moja ya timu imara ndani ya michuano yenyewe na kufikia hatua ya kuwang’oa hadi wenyeji Afrika Kusini kwa kuwafunga bao 1-0. Bao lilifungwa na mshambuliaji Elias Maguri.

Stars ilikuwa na kiwango bora na nidhamu ya hali ya juu. Haikuwa jambo la ajabu kuona michezo mitano iliyocheza kikosi hicho, michezo minne ikitoa wachezaji bora wa mchezo (Man of the Match). Ndiyo timu pekee iliyotoa wachezaji bora wa michezo yake tofauti na mataifa mengine 11 yaliyoshiriki michuano hiyo.

Katika pambano la kwanza dhidi ya Mauritius, ambapo Stars ilishinda kwa mabao 2-0 mabao yaliyofungwa ya Shiza Kichuya, ilishuhudia baada ya pambano hilo Kichuya akitangazwa mchezaji bora wa mechi.

Pambano la pili Stars iliyocheza dhidi ya Malawi ilimalizika kwa sare tasa na kumshuhudia kiungo mshambuliaji wa Stars Muzamir Yassin akitangazwa mchezaji bora wa mechi na mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya Angola uliomaliika kwa sare ya kufungana bao 1-1, bao la Stars likifungwa na Simon Msuva, ilishuhudia Msuva akipewa heshima ya kuwa mchezaji bora wa mechi.

Mchezo wa robo fainali dhidi ya wenyeji Afrika Kusini ulimalizia kwa Stars kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0, lililofungwa na Maguli na nyota huyo anayekipiga Qatar akapewa tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Ni mchezo mmoja tu wa Stars dhidi ya Zambia ambao tulipoteza kwa idadi kubwa ya mabao ndiyo hatujaweza kupata tuzo ya mchezaji bora, lakini michezo yote tulipata heshima hiyo. Hivi bado hatumuamini kocha Salum Mayanga na kikosi chake?

Sifa zote za Stars kwenye michuano hiyo zinatakiwa kuanzia kwa benchi la ufundi lililo chini ya Mayanga. Kocha huyo wa zamani wa klabu za Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar anatakiwa kupongezwa kwa kile ilichokifanya Stars kwenye michuano hiyo.

Kocha huyo mzawa amethubutu kuwajenga wachezaji wake wacheze kitimu na kumfanya kiungo wa Simba Muzamiru Yassin kuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi chake waliowavutia mawakala wa soka nchini humo.

Chini ya Mayanga, Muzamiru amekuwa moja ya viungo mahiri wa kupiga pasi kwa washambuliaji na moja ya pasi inayokumbukwa ni ile aliyompigia Maguri kuwaua wenyeji kwenye mchezo wa robo fainali.

Mafanikio ya mwisho kwa Stars ilikuwa mwaka 2010 kwa timu ya taifa Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kulitwaa taji la Challenge Cup kwa kuwafunga Ivory Coast kwenye Uwanja Taifa jijini Dar es Salaam, na kushinda taji hilo.

Lakini mara zote kikosi hicho kila kilipoenda kushiriki michuano mingine kilishindwa kutwaa taji lolote lile wala kufika hatua nzuri kama ya nusu fainali iliyofikia nchini Afrika Kusini hivi sasa. Kwa vyovyote vile haya ni mafaikio na hatutakiwi kuwabeza mashujaa wetu.

Kupitia hatua ya nusu fainali iliyoipata Stars katika michuano hiyo, Tanzania imepanda katika viwango vya Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) vinavyotolewa kila mwezi. Tanzania imepanda kwa nafasi 22.

Tanzania kwa sasa imefanikiwa kusogea hadi nafasi ya 135 kutoka nafasi ya 157. Mwezi Machi Tanzania imecheza mechi mbili ambazo ni dhidi ya Burundi ikashinda kwa goli 2-1 na dhidi ya Botswana iliyoshinda kwa goli 2-0.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here