KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando, baada ya kujiridhisha kwamba mikataba minne aliyoingia Uingereza kwa niaba ya shirika hilo haikuwa na nguvu ya kisheria.
Tido aliachiwa huru jana saa chache wakati kesi yake ikielekea kutimiza mwaka mmoja leo tangu afikishwe kwa mara ya kwanza mahakamani hapo na kusomewa mashtaka matano ya uhujumu uchumi likiwamo moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 887.1.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, alisoma hukumu jana ambapo Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai na upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili, Dk. Ramadhani Maleta.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shaidi, alisema ushahidi unaonyesha mshtakiwa alikuwa mwajiriwa wa TBC na aliingia mkataba na Kampuni ya Channel 2 group wa kubadili mfumo kutoka analojia kwenda dijitali.
“Mkataba huo ulifanyika bila kufuata utaratibu wa kisheria ikiwemo kushindwa kuhusisha wizara na wajumbe wa bodi.
“Wazabuni walishindanishwa ambapo Star Communication ilishinda na hakuna mahali ambapo Channel 2 ililalamika.
“Ni kweli lazima mkataba wa Serikali usainiwe na wahusika, ipitiwe kabla na imhusishe Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema.
Alisema mikataba minne iliyosainiwa na mshtakiwa haikusainiwa na wajumbe wa bodi wala AG, haikukidhi kuitwa mikataba kwani haikuwa na nguvu ya kisheria.
“Kwa maelezo hayo mahakama haiwezi kumtia hatiani mshtakiwa hivyo inamwachia huru, upande ambao haujaridhishwa wanayo nafasi ya kukata rufaa,” alisema.
Wakili Swai aliifahamisha mahakama kwamba anayo nia ya kukata rufaa.
Katika utetezi wake, Tido alidai kwamba mikataba aliyoingia ilikuwa inalenga kumwaminisha Channel 2 kwamba kuna mabadiliko ya mfumo yanatakiwa kufanyika na kampuni hiyo itashiriki katika zabuni lakini haikuwa mikataba rasmi.
Alidai alifanya hivyo baada ya Channel 2 kumtaka awahakikishie kwamba mchakato huo utakuwepo nao watakuwa miongoni mwa watakaoshiriki katika ushindani.
Tido katika kesi hiyo alijitetea mwenyewe na Jamhuri ilikuwa na mashahidi watano wakiwemo Ofisa Uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.
ALIPOFIKISHWA MAHAKAMANI
Wakati kesi hiyo ilipofikishwa mara ya kwanza mahakamani hapo Januari 26 mwaka jana, Swai alidai kuwa Juni 16, 2008, Tido akiwa Dubai kama mtumishi wa TBC alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya uendeshaji wa vipindi kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BVI) bila kutangaza zabuni na hivyo kuinufaisha channel hiyo.
Pia alidai Juni 20, 2008 akiwa huko huko Dubai kama Mkurugenzi Mkuu wa TBC, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya kiutendaji kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni.
Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai pia kama mwajiriwa wa TBC kwa makusudi alisaini mikataba ya kununua, kusambaza na kusimika vifaa vya kurushia matangazo kati ya TBC na Channel 2 group bila kutangaza zabuni ya manunuzi na kuisababishia channel hiyo kupata faida.
Swai alidai Novemba 16, 2008 akiwa Dubai kwa mara nyingine kwa makusudi alisaini mikataba ya uendeshaji wa miundombinu ya DTT kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni.
Alisema kitendo hicho kilikiuka kifungu cha 31 cha sheria ya manunuzi namba 21 ya mwaka 2004 na hivyo kuifanya chaneli hiyo ipate faida.
Katika kosa la tano alidaiwa aliisababishia mamlaka hasara ya Sh 887,112,219.19.
Pasipo kufafanua kwa kina hasara hiyo ilielezwa mahakamani hapo, Tido kwa mamlaka yake alisababisha hasara hiyo kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa Falme za Kiarabu, kama mwajiriwa wa TBC kwa cheo cha Mkurugenzi Mkuu.
Baada kusomewa mashtaka hayo, Tido aliyakana na alipatiwa dhamana baada ya mahakama hiyo kupewa kibali maalumu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) cha kusikiliza kesi hiyo, Hakimu Nongwa, alikubali ombi hilo na alimtaka mshtakiwa atoe ama fedha taslimu shilingi milioni 444 au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hiyo.
HUYU NDIYE TIDO
Tido ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Azam Media Limited, ana uzoefu wa zaidi ya miaka 40 kwenye tasnia ya utangazaji na uandishi wa habari, amejulikana na kuheshimika katika tasnia hiyo ukanda wa Afrika Mashariki na ulimwenguni kote.
Alianza kazi yake ya utangazaji kama DJ na Radio Tanzania, baadaye akawa mtangazaji wa michezo maarufu na habari nyingine.
Tido pia ameripoti katika mashirika makubwa ya habari ikiwa ni pamoja na Deutsche Welle (DW), Sauti ya Amerika (VOA) na Shirika la Utangazaji wa Kenya, ambalo lilijulikana wakati huo kama Sauti ya Kenya.
Alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kati ya 1999 hadi 2006 na baada ya hapo alirudi Tanzania kwa wito wa Serikali ya awamu ya nne ili kuja kuliendeleza Shirika la Utangazaji nchini (TBC).
Akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TBC kati ya mwaka 2006 na 2010, Mhando alifanya maboresho makubwa ya mfumo wa utendaji na kubadili programu mbalimbali kiasi cha kituo hicho kuanza kuonekana kuwa tishio hasa kwa washindani wake.
Wakati wa uongozi wa Tido, TBC mbali na kurusha taarifa za kampeni katika njia iliyoonekana kuwa si ya upendeleo hata kwa chama tawala, pia ilifanikiwa katika urushaji wa moja kwa moja wa matangazo ya mechi za mpira wa miguu na matukio makubwa ya kisiasa na kijamii, Bunge na kufanya kituo hicho kuwa na uwezo wa kupambana na vituo vingine vya watu binafsi na pia kuaminiwa na wananchi.
Hata hivyo, baada ya miaka minne Serikali iliamua kuachana naye baada ya mkataba wake kwisha. Baada ya kuondoka TBC, kabla ya kwenda Azam alipo hadi sasa, Tido alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Comunication (MCL) mwaka 2012 na kudumu miaka miwili na nusu.