25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RC Simiyu aitunishia msuli Wizara ya Mifugo

SAMWEL MWANGA, SIMIYU

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, ameikosoa operesheni maalumu inayoendeshwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayoitwa Nzagamba kwa sababu inawavuruga wafugaji.

Pia amepiga marufuku operesheni hiyo mkoani humo kwa sababu watendaji wa wizara hiyo wanaitekeleza bila weledi.

Akizungumza juzi mbele ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega, katika kikao cha viongozi wa Simiyu na wataalamu, alisema mkoa huo umekuwa ukiwathamini wafugaji kwa kuwafundisha kufuga kibiashara kwa kunenepesha mifugo yao ili wapate faida kupitia mifugo hiyo na si kuwavuruga kwa kutumia operesheni kama Nzagamba.

“Sisi tunawalea wafugaji kibiashara, tunawafundisha kunenepesha mifugo, tunawafundisha kufuga kwa faida ili kesho viwanda vya ngozi, maziwa na nyama viweze kupata malighafi lakini tukiendekeza hizi operesheni na kuwavuruga wafugaji tutapata wapi malighafi.

“Ni lazima mtumie lugha nzuri na hawa watu wanaotoka wizarani kuja kutekeleza operesheni hizi huku mikoani watumie lugha nzuri na wafanye kazi kwa weledi na wasifanye kazi kama mgambo na kwa Simiyu huu si mkoa wa Operesheni Nzagamba,” alisema.

Mtaka alisema wamekuwa wakianzisha minada ya mifugo na kuwahudumia wafugaji katika kuwasaidia ili waweze kufuga kwa faida, lakini cha kushangaza wizara hiyo imekuwa ikija kukusanya maduhuli na kupandisha hadhi minada na kuifanya kuwa ya upili lakini hawajawahi hata kuchimba shimo moja la choo kwa minada wanayoichukua.

“Hapa wizara kwa Mkoa wa Simiyu hamna kitu kabisa kwa sababu sisi tunawahudumia wafugaji wetu vizuri kwa mfano katika Wilaya ya Meatu tumeanza kuwapimia kila mfugaji eneo lake kwa ajili ya malisho na tunaanzisha minada.

“Lakini ninyi mnakuja kukusanya maduhuli tu na kupandisha hadhi minada kuwa ya upili na mnaichukua lakini tangu mchukue minada hiyo kwa Simiyu hamjawahi hata kuchimba tundu moja la choo katika minada hiyo,” alisema.

Naye Ulega alisema dhamira ya kuanzisha operesheni hiyo ni kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali yanayotokana na biashara ya mifugo na mazao yake.

Alisema operesheni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu imedhihirisha kwamba usimamizi thabiti wa sheria, kanuni na taratibu katika sekta ya mifugo unaleta tija kwa kuongeza uzalishaji bora wa mazao ya mifugo.

Alisema baada ya Serikali kubaini kila mwaka inapoteza jumla ya Sh bilioni 263  kutokana na kushamiri kwa utoroshaji wa mifugo nje ya nchi na uingizaji wa mazao ya mifugo usiozingatia sheria na taratibu.

Pia aliwaomba watendaji wa wizara hiyo wanaotekeleza operesheni hiyo kuheshimu mamlaka za mikoa wanayokwenda kufanya kazi zao na kushirikiana nao kwa sababu wote wanafanya kazi katika Serikali moja.

“Mkuu wa mkoa kwa kweli umetupiga viboko katika kikao hiki hivyo basi niwaombee msamaha kwa watendaji wetu wanaotekeleza operesheni hii kama walikwenda kinyume walipofika hapa Simiyu ila watambue kuwa kila mkoa una uongozi wake, ni lazima washirikiane nao wanapokwenda kufanya kazi na wasijigeuze na kujifanya wakubwa kuliko waliowakuta huku mikoani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles