AGATHA CHARLES
WAKATI Mkoa wa Kilimanjaro ukiendelea kushika nafasi ya kwanza tangu mwaka juzi katika matokeo ya kitaifa ya Mtihani wa Kidato cha Nne, mikoa mingine saba imeonekana kupanda kwa kasi katika matokeo ya 2018 yaliyotangazwa juzi.
Katika matokeo hayo ambayo yamewekwa pia kwenye tovuti ya Necta, Kilimanjaro imeongoza kwa kupata GPA 3.7616.
Ukiwa na idadi ya vituo 316, umepata idadi ya ufaulu kama inavyoonekana kwenye mabano ambapo daraja la I (1,538), II (3,653), III (4,571), IV (10,807) huku 0 (4,906).
Wakati Kilimanjaro ikisalia katika nafasi hiyo, mikoa saba iliyopanda kwa kasi katika matokeo ya mwaka 2018 yaliyotangazwa juzi ni Mbeya ambayo imetoka nafasi ya sita mwaka 2017 hadi kushika nafasi ya pili katika matokeo hayo.
Mkoa mwingine uliopanda ni Arusha ambao umeshika nafasi ya nne kutoka ile ya saba ya mwaka 2017.
Mbali ya huo, Mkoa wa Kigoma nao umevuta kasi kutoka nafasi ya 10 mwaka 2017 hadi ile ya tano katika matokeo yaliyotangazwa juzi.
Mkoa wa Simiyu nao umeshangaza kwa kupanda kutoka nafasi ya 11 hadi ile ya tisa huku Mkoa wa Njombe ukipanda nafasi tano kutoka namba 15 hadi 10.
Mkoa wa Iringa nao umepanda kutoka nafasi ya 17 katika matokeo ya 2017 hadi ile ya 12 (2018) huku Songwe ukitoka nafasi ya 21 hadi ile ya 15 kwenye matokeo hayo.
Nafasi kimkoa
Ukiacha Kilimanjaro iliyoshika nafasi ya kwanza, Mkoa wa Mbeya uliokuwa na idadi ya vituo 211, umeshika nafasi ya pili kimkoa huku ufaulu wake katika idadi ya madaraja ukiwa kama ifuatavyo; daraja la I (798), II (2,528), III (3,819), IV (9,061) na 0 (2,729).
Nafasi ya tatu imekamatwa na Mkoa wa Shinyanga uliokuwa na idadi ya vituo 138, ukiwa na ufaulu wa madaraja kama ifuatavyo; I (503), II (1,246), III (1,821), IV (4,501) na 0 (1,764).
Mkoa wa Arusha ambao ulitoa mtahiniwa bora wa kwanza katika matokeo hayo, Hope Mwaibanje wa Ilboru, uko katika nafasi ya nne ukiwa na idadi ya vituo 218 ambao ulipata GPA 3.7945.
Katika mkoa huo, waliopata daraja la I (920), II (2,646), III (3,995), IV (9,649) na 0 (3,661).
Kigoma ambao uko nafasi ya tano, ukiwa na idadi ya vituo 171, umepata alama kama ifuatavyo; daraja I (348), II (1,465), III (2,141), IV (4,570) na 0 (1,807).
Mkoa ulioshika nafasi ya sita ni Tabora ambao ulikuwa na idadi ya vituo 173 ukiwa na I (339), II (1,281), III (1,756), IV (4,517) huku 0 (1,639).
Mkoa ulioshika nafasi ya saba ni Pwani ambao ulikuwa na vituo 164, ukiwa na ufaulu daraja I (910), II (1,294), III (1,639), IV (5,091) na 0 (2511).
Nafasi ya nane imeshikwa na Mkoa wa Kagera ambao ulikuwa na idadi ya vituo 241, ulikuwa na daraja la I (823), II (2,146), III (3,131), IV (8,178) na 0 (3,256).
Mkoa wa Kagera umepanda nafasi moja kutoka ile ya tisa mwaka 2017 hadi ya nane ukiwa na GPA 3.8149.
Kwa upande wa Mkoa wa Simiyu ambao umeshika nafasi ya tisa katika matokeo ya sasa umepata I (215), II (953), III (1,407), IV (3,236) na 0 (1,228) huku ukiwa na GPA 3.8225.
Mkoa wa Njombe ambao umeshika nafasi ya 10 una daraja la I (270), II (975), III (1,486), IV (4,284) na 0 (1,163) huku ukipata GPA 3.8267.
Mbali na huo, Mkoa wa Manyara ambao umepanda nafasi moja kutoka ile ya 12 mwaka 2017 hadi 11, katika matokeo haya ufaulu wake ulikuwa daraja la I (233), II (1,210), III (1,953), IV (4,431), 0 (1,457) ukiwa na GPA 3.8277 na idadi ya vituo 150.
Mkoa wa Iringa ambao uko nafasi ya 12, uliokuwa na idadi ya vituo 162, ufaulu wa madaraja ulikuwa I (532), II (1,315), III (2,264), IV (6,377) na 0 (1,920) ambapo ulipata GPA 3.8412.
Mkoa wa Mwanza ambao katika matokeo haya umeporomoka kutoka nafasi ya tano mwaka 2017, umeshika nafasi ya 13 ukiwa na daraja la I (1,043), II (3,133), III (4,673), IV (11,683), 0 (6,030) ukiwa na GPA 3.8766.
Aidha, katika matokeo haya, Mkoa wa Rukwa ambao umeporomoka kwa nafasi moja ukilinganisha na mwaka 2017, umeshika nafasi ya 14 , ukiwa na daraja I (94), II (568), III (1,108), IV (2,896) na 0 (808) huku GPA ikiwa ni 3.8806.
Mkoa wa Songwe ulio nafasi ya 15, uliokuwa na vituo 106, umekuwa na ufaulu daraja la I (133), II (844), III (1,212), IV (3,225) na 0 (1,233).
Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kushika nafasi ile ile ya 16 kwa miaka miwili mfululizo ukiwa na daraja la I (1,658), II (3,999), III (5,799), IV (16,864) na 0 (8,834).
Mkoa wa Morogoro ambao ulikuwa na idadi ya vituo 236, umeshika nafasi ya 17 ukiwa na I (689), II (1,839), III (2,514), IV (7,849), 0 (3,988) ukiwa na GPA 3.9200.
Singida umeshika nafasi ya 18 ukiwa na vituo 158 ambao daraja la I ilikuwa (204), II (845), III (1,329), IV (4,270) na 0 (1,678).
Mkoa wa Geita ambao umeporomoka kutoka nafasi ya nane katika matokeo ya mwaka 2017 katika matokeo ya sasa umeshika nafasi ya 19, ukiwa na daraja la I (313), II (1,019), III (1,765), IV (4,842) na 0 (2,534).
Mkoa wa Ruvuma umeonekana kupanda kutoka nafasi ya 25 mwaka 2017 hadi ile ya 20 katika matokeo haya ukiwa na
daraja la I (238), II (992), III (1,676), IV (5,738) na 0 (2,065).
Nafasi ya 21 imechukuliwa na Mkoa wa Dodoma ukiwa umeanguka kutoka nafasi ya 19 mwaka 2017 ukiwa na daraja la I (342), II (1,154), III (1,837), IV (5,969) na 0 (2,745).
Mara imepanda kwa nafasi moja zaidi kwa kushika nafasi ya 22 kutoka 23 ya mwaka 2017 ukiwa na I (330), II (1,325), III (2,301), IV (6,301) na 0 (3,508).
Mkoa wa Katavi ndio uliotolewa na Mara safari hii ukishika nafasi ya 23 kutoka ile ya 22, ukiwa na I (43), II (235), III (414), IV (1,380) na 0 (625).
Mkoa wa Tanga umebaki katika nafasi yake ile ile ya 28 ukiwa na I (589), II (1,323), III (2,391), IV (8,842) na 0 (4,519).
Mkoa wa Mtwara umeporomoka kutoka nafasi ya 20 hadi 25 ukiwa na I (196), II (518), III (990), IV (4,339) na 0 (1,728).
MIKOA ILIYOANGUKA
Miongoni mwa mikoa iliyoonekana kuanguka katika matokeo haya ni Tabora ambao umetoka nafasi ya tatu katika matokeo ya mwaka 2017 hadi nafasi ya sita katika matokeo haya ya mwaka 2018.
Mwingine ni Mkoa wa Pwani ambao ulikuwa na watahiniwa wanne katika watahiniwa 10 bora, uko katika nafasi ya saba katika matokeo haya ukiporomoka kutoka nafasi ya pili mwaka 2017.
Mkoa wa Mwanza umeporomoka kwa kasi kutoka nafasi ya tano mwaka 2017 hadi nafasi ya 13 katika matokeo haya.
Rukwa ambao ulikuwa na vituo 90, ulishuka nafasi moja kutoka ile ya 13 mwaka 2017 hadi 14 mwaka huu.
Mkoa wa Morogoro umeporomoka kutoka nafasi ya 14 hadi ya 17.
Mkoa wa Geita nao umeporomoka kutokana nafasi ya nane 2017 hadi ya 19 mwaka huu na Dodoma imeporomoka kutoka nafasi ya 19 hadi ile ya 21 ukiwa na ufaulu wa madaraja kama ifuatavyo, I (342), II (1,154), III (1,837), IV (5,969) na 0 (2,745).
MIKOA ILIYOBAKI PALE PALE
Mbali na Kilimanjaro ambao mwaka 2017 ulikuwa nafasi ya kwanza na katika matokeo haya umeendelea kushikilia nafasi hiyo hiyo, Mkoa wa Dar es Salaam nao umeendelea kubaki katika nafasi yake ile ile ya 16 kwa miaka miwili mfululizo.
Mwingine ni Mkoa wa Singida ambao umeshika nafasi ya 18 kwa miaka miwili mfululizo.
Pamoja na hilo, mikoa ambayo imeonekana kufanya vibaya kwa mara nyingine na kubaki katika nafasi ile ile ni Tanga nafasi ya 4, Mjini Magharibi (26), Lindi (27), Kusini Pemba (28), Kaskazini Pemba (29), Kusini Unguja (30) na Kaskazini Unguja (31).
MWISHO