22.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Hifadhi za Taifa kuanzisha shirika la ndege

kabwePatricia Kimelemeta na Grace Shitundu
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa miezi mitatu kwa Msajili wa Hazina kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa shirika jipya la ndege litakaloendeshwa na mamlaka za hifadhi za taifa ili kutoa huduma kwa abiria na watalii.
Mamlaka hizo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Akizungumza na wadau katika kikao cha majadiliano kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema mamlaka hizo zitashirikiana moja kwa moja na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kuangalia namna ambayo shirika hilo linaweza kufanya kazi zake, hivyo kusaidia Serikali kuongeza mapato.
“Lengo letu ni kuhakikisha Serikali inamiliki ndege zake binafsi ambazo zitaweza kubeba abiria na watalii wanaokuja nchini, hivyo kusaidia kuongeza mapato,” alisema Zitto.
Mwenyekiti huyo wa PAC alisema mchakato wa uanzishwaji wa shirika hilo ulianza mwaka 2011 ambapo wabunge kwa pamoja waliangalia namna ya kulishughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuzitaka mamlaka hizo kuanzisha mashirika ya ndege ili yaweze kufanya kazi hiyo.
Alisema ilipofika Novemba 2012, wabunge hao walifikia maazimio ya kuitaka Serikali kutekeleza maagizo yaliyotolewa na wabunge ili kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo, Serikali iliziandikia barua mamlaka hizo na kuwataka kuchangia uanzishwaji wa shirika hilo jipya bila ya kumiliki jambo ambalo ni kinyume na maazimio ya wabunge.
“TANAPA na Ngorongoro walikuja kwenye kamati na kulalamikia uamuzi wa kuchangia kwa madai kuwa wametwishwa mzigo kwa kuwa wanakatwa kodi nyingi.
“Kwa mwaka wanatoa wastani wa Sh bilioni 15 za pato ghafi kwenda hazina, halafu wanatoa asilimia 3 ya mapato yao kwa ajili ya kupeleka Wizara ya Maliasili na Utalii na asilimia 30 kwa ajili ya kodi,” alisema Zitto.
Alisema ikiwa watapunguziwa kodi na makato mbalimbali, wataweza kutoa Sh bilioni 30 kwa ajili ya uanzishwaji wa shirika hilo.
Alibainisha wakati wanaangalia namna ya kulishughulikia suala hilo kamati hiyo ilikaa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuangalia namna ambayo wanaweza kulishughulikia suala hili.
Alifafanua kutokana na hali hiyo, kamati imeamua kuwaita wadau wote hao ili kukaa kwenye kikao cha majadiliano na kufikia uamuzi wa kuanzishwa kwa shirika hilo hadi ifikapo Juni mwaka huu.
Alisema hadi sasa ATCL imekufa, jambo ambalo limewafanya wabunge kufikia uamuzi wa kuanzishwa kwa shirika hilo ili liweze kufanya kazi zake.
“Ki ukweli ATCL imekufa…hatuna shirika la Serikali linalomiliki ndege, jambo ambalo limetufanya kufikiria uamuzi wa kuanzishwa kwa shirika jipya la ndege litakaloweza kutoa huduma ya usafiri nchini, lakini mamlaka za hifadhi za taifa zitakuwa sehemu ya wamiliki,” alisema.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo, mikakati yote iliyoanzishwa na Serikali ya kutaka kulifufua shirika la ndege iingizwe kwenye mikakati iliyopo ili iweze kuboresha utekelezaji wa uanzishwaji wa shirika hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles