24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Hekaheka za Uchaguzi Mkuu Nigeria

*Rais ni Buhari au Abubakar?

OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI

USAFIRI katika miji mikubwa ya Afrika ni jambo lisilotabirika, ni tatizo kubwa. Na pale chama tawala cha Nigeria, APC (All Progressive Congress) kinapowaalika watu wahudhurie mkutano wa hadhara wa kuanzisha kampeni zake za uchaguzi katika Jiji la Lagos lenye wakaazi milioni 18, safari ya kwenda hadi uwanja wa ndege huwa ni ya kishindo.

Inahitaji mtu awe na subira. Huo ni wakati ambapo wafuasi wa Rais Muhammadu Buhari wanasafirishwa kwa mabasi madogo. Wengi wa watu hao huvaa mashati ya rangi ya chama- samawati, kijani na nyeupe. Anayegharamia kuchapisha mashati hayo ni Babajide Sanwo-Oulu, mgombea wa kiti cha ugavana kwa Mkoa wa Lagos katika uchaguzi ujao.

Katika msongamano wa barabarani siku kama hiyo, magari ni nadra kuweza kusafiri mwendo wa hata sentimita moja kwa dakika. Baada ya tukio hilo magazeti yaliripoti kwamba alikuwapo jambazi aliyejiingiza miongoni mwa kundi la wanachama wa APC na kufyatua risasi. Si chini ya watu wawili waliuawa.

Kampeni za uchaguzi zimeanza Nigeria. Lakini hazionekani waziwazi kila mahala kama ilivyo katika Jiji la Lagos. Wagombea sasa wanaanza kutangatanga katika nchi hiyo kubwa yenye wakaazi milioni 191. Mkaazi wa kutoka Mkoa wa Niger, kaskazini ya nchi, anasimulia kwamba hadi sasa, kinyume na ilivyokuwa zamani, hajashuhudia fedha zikisambazwa ili kununua kura.

Jumuiya isiyokuwa ya kiserikali ambayo inaangalia namna uchaguzi huu unavyoendeshwa, Afrika Ylaga, hata hivyo, inasema kwamba kila siku ya uchaguzi inapokaribia ndipo zawadi zinapozidi kutolewa. Februari 16 zitafanywa chaguzi za urais na bunge na wiki mbili baadaye zitafuata za magavana wa mikoa na pia mabunge ya mikoa. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi watu milioni 84 wamejiandikisha kupiga kura, ikiwa ni milioni 14.3 zaidi ya watu waliojiandikisha miaka minne iliyopita.

Uchaguzi wa mwaka 2015 ulitoa mshangao. Rais Goodluck Jonathan wa Chama cha People’s Democratic (PDP), ambacho kilitawala Nigeria tangu nchi hiyo ilipoachana na tawala za kijeshi mwaka 1999, siku tatu  baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo, alimpongeza mshindani wake, Muhammadu Buhari na akakiri kushindwa.  Lilifuata zoezi la amani la kukabidhiana madaraka katika nchi hiyo ambayo hapo kabla ilijionea mapinduzi ya kijeshi ya kila mara. Tukio hilo lilikuwa muhimu kwa Bara la Afrika. Uchumi wa Nigeria ni mkubwa kabisa barani Afrika na utulivu wa nchi hiyo unategemewa na Afrika Magharibi yote.

Sasa ni kufa na kupona. Kuna wagombea 25 wa urais. Chama cha PDP, ambacho miaka minne iliyopita kilipoteza mamlaka, kinataka kurejea madarakani na mgombea wake wa urais ni Atiku Abubakar (miaka 72). Abubakar, mfanyabiashara, aliwahi kuwa makamu wa rais  kati ya mwaka 1999-2007. Rais wa sasa, Muhammadu Buhari anauwania tena wadhifa huo. Wagombea wengine hawatiliwi dau hata kidogo. Buhari na Abubakar wanatokea Kaskazini ya Nigeria ambako wakaazi wengi ni Waislamu.

Nigeria ni moja ya nchi duniani zenye uwakilishi mdogo sana wa wanawake katika  shughuli za siasa. Mara hii mtetezi wa kike, Oby Ezekwesite wa Chama cha Allied National Congress (ACPN), ni ishara kwamba mambo yameanza polepole kubadilika.

Hakuna uchunguzi wa maoni ya watu wenye kutegemewa ulioonesha wazi hasa nani atakuwa mshindi, lakini mambo yalivyoonesha ushindi utakiendea Chama cha APC kama ilivyokuwa mwaka 2015. Licha ya hayo, Buhari amedhihirika kuwa ni rais dhaifu. Zaidi ya hayo, yeye mara nyingi, tena kwa vipindi virefu, alikuwapo London kwa ajili ya matibabu- ilisemekana anakabiliwa na ugonjwa wa saratani ya tezi dume. Katika miezi iliyopita mamia ya wanasiasa wamebadili vyama, kama vile Spika wa Senate, Bukola Saraki, kutoka Chama cha APC kwenda Chama cha PDP. Miaka minne iliyopita mambo yalikuwa kinyume na hivyo.

Wafuasi wa Buhari wanamsifu mwanasiasa huyo (aliwahi kuwa mwanajeshi) kuwa si mpenda makuu, mtu wa watu. Lakini kuna watu (hasa wale wanaoishi katika miji mikubwa) wanaomlaumu rais huyo mzee kushindwa kuyafikia malengo ya ahadi zake alizotoa mwaka 2015  katika kampeni za uchaguzi- kurejesha usalama nchini, kupambana na rushwa na ufisadi na kuuimarisha uchumi. Huko Kaskazini Mashariki ya Nigeria kundi la kigaidi la Boko Haram bado linaendesha mashambulio ya silaha. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu milioni 1.9 wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani nchini humo.

Katikati ya Nigeria mivutano imezidi baina ya wakulima na wafugaji na maelfu ya watu  wameuawa. Huko Kaskazini Magharibi ya nchi, Mohammed Hamisu mwenye umri wa miaka 23 na ambaye kijiji chake kilivamiwa karibuni, alisema: Hatuwezi kupiga kura kwa utulivu. Kuna woga mwingi.

Sababu ya kuzidi kukosekana usalama: ni hali mbaya ya uchumi inayoambatana na ughali mkubwa wa maisha na uchumi kwenda chini. Yote hayo yamesababisha watu kuwa maskini zaidi. Ikiwa ni muda mfupi sasa kabla ya uchaguzi, kima cha chini cha mshahara kimepandishwa kutoka Naira 18,000 (sawa na bei ya gunia la mchele la kilo 50) hadi Naira 30,000. Yaani kutoka dola za Kimarekani 38 hadi 63. Huo ni ushahidi kwamba maisha ni magumu kwa mtu wa kawaida huko Nigeria. Pia kote nchini humo watu wanalalamika juu ya uhaba wa ajira.

Hiyo ndio sababu mfanyabiashara Abubakar sasa amejichovya katika kampeni za uchaguzi. Yeye ameahidi kuondosha ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa wastani milioni 50. Buhari anamtuhumu Abubakar kwamba ni fisadi mkubwa na anaitaja ripoti ya Baraza la Senate la Marekani iliyomnyooshea kidole Abubakar.

Katika ripoti hiyo ilitajwa kwamba Atiku Abubakar na mmoja wa wake zake baina ya mwaka 2000 hadi 2008 alihamisha zaidi ya dola milioni 40 kutoka Nigeria kwenda Marekani. Kwa miaka hajapewa viza, yaani ruhusa ya kuingia Marekani. Tayari kuna makisio yanayosema kwamba upinzani utashindwa tena katika uchaguzi huu.

Mtu yeyote anayesafiri kwa gari ndani ya Nigeria ataweza kuona vizuizi vingi barabarani. polisi, maafisa wa forodha na wa kukusanya kodi mara kadhaa wengi wao hupokea noti kutoka kwa madereva na baadaye kuwapungia mkono waendelee na safari zao.

Hivi karibuni katika Mji Mkuu wa Abuja ilianza kesi ya ufisadi dhidi ya Rais wa Mahakama Kuu, Walter Samuel Nkanu Onnoghen: Inasemekana alikuwa na akaunti ya akiba ya fedha nje ya nchi ambayo hajaitaja. Buhari ameshamvua jaji huyo wadhifa wake, ama sivyo jaji huyo angeweza kuamua juu ya kuidhinishwa matokeo ya uchaguzi huu baada ya kutangazwa hapo Februari.

Kwa ufupi, uchaguzi huu utaamuliwa na mambo matatu kama iliyokuwa mwaka 2015- kukosekana usalama, uchumi na ufisadi. Kura za vijana zitaamua mshindi atakuwa nani. Nigeria ni nchi yenye vijana wengi, lakini bado uchaguzi huu unaonesha kwamba wazee wanadhibiti siasa ya Nigeria. Wachunguzi wa mambo wanasema shida ya siasa za Nigeria ni kwamba hamna tofauti ya nadharia baina ya vyama vikuu viwili vya siasa katika nchi hiyo, hivyo ni shida kwa mpigaji kura kuamua, hasa vijana wanaotaka kujua nani atawapatia ajira na nani atahakikisha usalama wao. Pia vizingiti vya kitamaduni huko Nigeria vinawaweka wazee kuwa juu zaidi kuliko vijana, hivyo kufanya mabadiliko yawe shida kufikiwa.

Waafrika wote wana kila sababu ya kufuatiliza kitu gani kitajiri Nigeria baada ya Februari 16. Nigeria inajivunia kuwa Kaka Mkubwa wa Afrika na somo itakalotoa Februari 16 litakuwa ni muhimu kwa ndugu zake wadogo barani Afrika.

Kila la heri kwa Kaka Mkubwa. Mategemeo  ya kila mtu, kama mdogo au mkubwa, ni uchaguzi Huru wa Haki na wa salama kabisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles