23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi Mkuu Nigeria vita ya vijana, ‘wahenga’

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

NIGERIA inatajwa kuwa na watu wapatao milioni 190 lakini ifahamike wazi kwamba zaidi ya asilimia 60 ni vijana.  Kwamba, wengi wa kati ya watu wa taifa hilo wana umri chini ya miaka 25.

Hata hivyo, ukilitazama Bunge lao, utabaini kuwa sehemu kubwa ya wawakilishi ni wanasiasa wenye umri mkubwa ‘wahenga’.

Kwa maana nyingine, licha ya wingi wa vijana, maamuzi yanayohusu mustakabali wa taifa hilo la Afrika Magharibi yamekuwa yakifanywa na viongozi wenye umri mkubwa, ambao baadhi yao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu.

Itakumbukwa pia, tangu kurejea kwa Demokrasia nchini  Nigeria, mwaka 1999, ulingo wa siasa za taifa hilo umekuwa ukitawaliwa na ‘wazee’. Ni kama ilivyoelezwa na ripoti ya Umoja wa Afrika (AU), kwamba idadi kubwa ya marais barani humu (33) wana umri wa zaidi ya miaka 50.

Hata hivyo, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Februari 16, mwaka huu vijana wameonekana kuamka, wakiwa wamepania kuwaweka pembeni wakongwe, ndoto aliyowahi kuwa nayo  Rais wa zamani wa nchi hiyo, Ibrahim Babangida.

“Wazee wanatakiwa kuwapisha njia vijana. Tumeshakuwa analojia, hiki ni kizazi cha dijitali. Hivyo basi, vijana wanatakiwa kuungwa mkono ili waweze kutumia maarifa yao ya kidijitali kuipeleka mbele nchi,” alisema Babangida.

Aidha, alimtolea mfano Jenerali Yakubu Gowon, ambaye alikuwa Rais wa Nigeria kuanzia mwaka 1966 hadi 1975, akisema alifanya makubwa kwa kipindi chote cha uongozi wake kwa kuwa alikuwa na umri wa miaka 31 tu.

Nikirejea katika Uchaguzi wa mwaka huu, katika kiti cha Urais, Rais Muhammadu Buhari wa Chama tawala cha All Progressives Congress (APC), ambaye ana umri wa miaka 75, amekaliwa kooni na kundi la vijana wenye kiu ya kwenda Ikulu.

Nianze na mfanyabiashara mwenye makazi yake jijini New York, Chike Ukaegbu (35). Chike anayekumbukwa na Wanigeria wengi kwa ufadhili wake wa masomo kwa vijana 13 kupitia mfuko wake wa hisani.

Kama hiyo haitoshi, isisahaulike kwamba mwaka 2015 alitajwa na ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mmoja kati ya vijana 100 wenye ushawishi barani Afrika.

Ukiacha na mgombea huyo wa Chama cha Advanced Allied Party (AAP), yumo pia mwanasheria mwanamke mwenye nguvu kubwa ya ushawishi kwenye siasa za Nigeria katika siku za hivi karibuni, Eunice Atuejide (40).

Mwingine anayeingia katika orodha hiyo ya vijana wanaoufukuzia mlango wa Ikulu, ni mwandishi wa habari mwenye jina kubwa ndani ya taifa hilo, Omoyele Sowore (47).

Huyo anasema anataka kuona mabadiliko katika siasa za Nigeria kwa wakongwe kubaki kuwa washauri na si kuwa na sauti ya mwisho katika nyadhifa nyeti za serikalini.

Licha ya umri wake huo mdogo, msomi huyo aliyewahi kuwa Rais wa Serikali ya Wanafuzi ya Chuo Kikuu cha Lagos, akisimamishwa masomo mara kadhaa kutokana na ushiriki wake katika siasa, ndiye mwasisi wa Chama cha Party Leader of the National  Interest Party (NIP).

Aidha, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utamshuhudia akikiwakilisha African Action Congress (AAC).

Katika kile ambacho hata wachambuzi wa siasa za Nigeria wanakifurahia kwa sasa, wakati Buhari anashinda uchaguzi mkuu miaka minne iliyopita akiwa na umri wa zaidi ya miaka 70, Katiba ya Nigeria haikuwa ikiwapa nafasi vijana wa aina hiyo.

Kipindi hicho, Katiba ilieleza wazi kwamba ili kushiriki chaguzi mkuu, mgombea wa kiti cha urais anatakiwa kuwa na umri wa kuanzia miaka 40.

Mwaka 2016, vijana kupitia vikundi mbalimbali vya kiharakati waliendesha kampeni ya kutaka sheria hiyo ifanyiwe mabadiliko, juhudi zilizozaa matunda miezi 12 baadaye baada ya Rais Buhari kusaini muswada aliofikishiwa na Bunge.

“Kama muswada ungekwama au Rais (Buhari) angekataa kuusaini, basi nisingekubaliwa kugombea Urais,” alisema Chike katika mahojiano yake na CNN.

Kuhakikisha Buhari na wakongwe wenzake katika ngazi zingine za uongozi serikalini wanaziachia nyadhifa zao kwa vijana, tayari wagombea wenye umri mdogo kama Chike na Eunice wanaungwa mkono na kampeni mbalimbali zikiwamo zile za ‘Not Too Young To Run’ na ‘Ready To Run’.

Vijana wamekuwa wakitegemea maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kuwafikia na kuwashawishi wananchi. Facebook, Instagram, Twitter na WatsApp ni sehemu ndogo tu ya njia zao.

Akilizungumzia hilo, Eunice alisema kupitia mitandao hiyo si tu anasambaza sera zake, pia anaitumia kama njia ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kampeni zake za kwenda Ikulu mwaka huu.

“Nina imani kwamba Wanigeria kokote duniani wataanza kunichangia kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya kampeni,” alisisitiza.

Kupitia mitandao hiyo ya kijamii, mwandishi Sowore, ambaye pia ni mwasisi wa Chama cha African Action Congress (AAC), mmiliki wa Shirika la Habari la Sahara Reporters na mwanaharakati wa haki za binadamu, ameshachangiwa Dola 63, 000 (zaidi ya Sh mil 145 za Tanzania) na wanaomuunga mkono katika safari ya Ikulu.

Aidha, yapo malalamiko kutoka kwa vijana, kwamba wakongwe kwenye ulingo wa siasa wamekuwa wakitumia njia chafu kuwapiga bao, ikiwamo kutumia fedha nyingi katika kampeni na kuuza kwa bei kali fomu za kuwania nyadhifa mbalimbali.

Mathalani, mgombea anayeitaka fomu ya urais ndani ya Chama tawala, APC, anatakiwa kuwa na Dola za Marekani 125,500 (zaidi ya Sh mil 280 za Tanzania).

Ikumbukwe kuwa bado chama hicho kinahaha kujisafisha kutokana na kashfa yake ya kutumia Dola za Marekani milioni 7.9 katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Huku pia wazee wakiwataka wapiga kura kutowachagua vijana kwa kuwa hawana uzoefu, pia wamekuwa wakigawa vyakula, fedha na bidhaa zingine kwa lengo la kupata ‘sapoti’.

Hiyo ni kusema kwamba si rahisi kwa wagombea vijana kumudu gharama hizo, tofauti na wazee ambao wana utajiri wa kutosha waliouchuma katika nyadhifa zao serikalini.

Ni kwa mazingira hayo basi, ndipo inapoonekana kwamba vijana wana mlima mrefu wa kupanda kutimiza ndoto  yao ya kuwaweka benchi viongozi wenye umri mkubwa, ingawa uamuzi unabaki kwa wapiga kura wa Nigeria.

Huku kukiwa na mnyukano huo kati ya vijana na wazee wao, wafuatiliaji wa siasa za Nigeria wanaamini kundi lenye nafasi kubwa ya kupata matokeo chanya ni lile litakaloibuka na sera zitakazojibu kwa ufasaha maswali haya matatu.

Kwanza, ni kwa namna gani litaweza kukabiliana na hali tete ya kiusalama inayochagizwa na uwepo wa Kundi la Kigaidi la Boko Haram na migogoro kati ya wakulima na wafugaji?

Serikali imekuwa ikitangaza kukishinda kikundi hicho lakini kila uchwao Boko Haram wameendelea kuwanyima raha wananchi. Kwa mwaka 2017 pekee, magaidi hao waliweza kutekeleza mashambulizi 135.

“Hali ya usalama imezorota, matukio ya watu kutekwa ni kila mahali na Boko Haram wamekuwa wakisumbua zaidi… Boko Haram wana nguvu zaidi siku hizi kuliko zamani,” alisema Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo akiukosoa utawala wa Rais Buhari.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa zaidi ya watu 14 wamekumbana na kadhia hiyo katika maeneo mbalimbali nchini humo, ambapo milioni 1.7 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Isisahaulike kuwa hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uliotakiwa kufanyika Februari 14 ulilazimika kusogezwa mbele kwa wiki sita, ambapo mbali ya sababu zingine, ilikuwamo pia tishio la Boko Haram.

Pili, ni njia gani zitakazotumika kumaliza uhaba wa ajira, tatizo linalowasumbua zaidi vijana? Ripoti ya hivi karibuni ilieleza kuwa asilimia 38 ya vijana wenye umri chini ya miaka 24 wanashinda vijiweni, kwamba  hawana kazi.

Lakini, ripoti hiyo ya Serikali ilipingwa na ile ya Benki ya Dunia (WB) iliyodai kuwa ni asimilia 80 na si 38.

Ukubwa wa tatizo ulianikwa na tukio la mwaka 2014, ambapo watu 16 waliuawa wakati wakigombea nafasi za kazi katika Wizara ya Uhamiaji. Serikali ilitangaza nafasi 5,000 lakini waliofika ni 500,000.

“Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba msongo wa mawazo walionao vijana wa Afrika na Nigeria wasio na kazi unaweza kuwafanya siku moja wakalipuka,” alisema Obasanjo.

Tatu, ni mikakati gani iliyoandaliwa kukabiliana na vitendo vya rushwa vilivyotamalaki? “Hakuna nchi isiyo na rushwa hapa duniani lakini katika mataifa mengine hawajaifanya kuwa mtindo wa maisha. Ukibainika, unashughulikiwa. Hicho ndicho tunachohitaji,” anasisitiza Obasanjo.

Kwa Nigeria, rushwa inatajwa kuwa kwa kiwango cha juu zaidi katika siasa, kanisani, taasisi za elimu ya juu na ndani ya mamlaka za Serikali, vikiwamo vyombo vya dola.

Mfano, James Ibori, Gavana wa zamani wa Jimbo la Delta, alibainika kuhusika katika ufisadi wa Pauni milioni 150 (zaidi ya Sh bil 444 za Tanzania), ingawa alihukumiwa kifungo cha miaka 13 gerezani.

Akilizungumzia hilo, mgombea wa kiti cha urais kupitia Chama cha Alliance for People’s Trust (APT), Gbenga Olawepo-Hashim, anasema:

“Wakati Nigeria ikiwa chini ya Obasanjo, ilipiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa kuliko utawala wa sasa (chini ya Buhari)… Ni kipindi cha Obasanjo ambapo ungeweza kuona waziri akishitakiwa.

“Ni kipindi cha Serikali ambayo Ispekta wa Polisi angeweza kuvishwa pingu na mtu aliye chini yake na kufikishwa mbele ya televisheni ya taifa.”

Je, kwa changamoto hizo, vijana wataweza kupindua meza mbele ya wazee wao? Uamuzi wanao wapiga kura wa Nigeria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles