21.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

HANS PLUIJM: Afunguka kwa Kessy

pluijmNa THERESIA GASPER-DAR-ES SALAAM

KOCHA mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, ameelezea umuhimu wa beki, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, ndani ya timu hiyo kutokana na umahiri wake wa kuimudu nafasi ya beki wa kulia anapokosekana Juma Abdul, lakini akafunguka zaidi na kudai Mbuyu Twite anafaa zaidi wanapocheza mechi kubwa.

Kauli ya kocha huyo raia wa Uholanzi, ilitokana na pigo alilolipata baada ya Abdul kuumia na kutolewa nje kipindi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC uliochezwa juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Pluijm alifanya mabadiliko ya kumuingiza Twite kucheza nafasi ya Abdul, huku akieleza kuwa Kessy ndiye mbadala sahihi, lakini Mburundi huyo ni muhimu kutokana na uwezo wake wa kucheza kama kiungo, beki wa kulia na wa kushoto.

“Tukicheza na timu kubwa kama Azam, unatakiwa kuangalia mchezaji sahihi unayeona anafaa kwa mchezo husika, Kessy alikuwa ni mchezaji sahihi anayeweza kumudu kucheza upande wa beki wa kulia, lakini Twite ana uwezo wa kucheza namba tofauti kwa wakati mmoja,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, Mholanzi huyo alikiri kikosi chake kuzidiwa kipindi cha pili ingawa waliweza kutawala zaidi dakika 45 za kwanza na kukosa mabao matatu ya wazi.

Aliongeza kuwa, baada ya Andrew Vincent ‘Dante’ kutoka kutokana na kupata majeraha, kasi ya mashambulizi uwanjani ilipungua na kuwaongezea nguvu wapinzani wao ambao walitawala zaidi kipindi cha pili ambacho kilikuwa kigumu zaidi kutokana na ushindani uliokuwepo.

Pluijm alisema wachezaji wake hawakupata nguvu ya kushambulia kipindi cha pili kutokana na pengo lililoachwa na Dante, kwani kulingana na mabadiliko aliyoyafanya, straika mmoja alilazimika kurudi nyuma na mwingine kubaki mbele.

“Kwa matokeo yaliyopatikana, si kwamba Yanga haiwezi kuifunga Azam kwani pamoja na mchezo kuchezwa kwa kiwango sawa kwa pande zote, tumepata nafasi za wazi lakini tukashindwa kuzitumia ipasavyo,” alisema Pluijm.

Matokeo ya sare ya juzi yaliwawezesha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, baada ya kufikisha pointi 15 kutokana na michezo nane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,717FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles