26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Flora Mbasha: Nipo tayari kurudiana na mume wangu

Pg 4Veronica Romwald na Jacqueline Swai (RCT), Dar es Salaam
MUIMBAJI wa muziki wa Injili, Flora Mbasha amesema yupo tayari kurudiana na mume wake Emmanuel Mbasha, ikiwa atakwenda kumuangukia miguuni na kumuomba msamaha.
Flora alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake juu ya kesi ya ubakaji inayomkabili Mbasha ambayo inasikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
“Mbasha nimemsamehe siku nyingi na nipo tayari kuishi naye iwapo atakuja kuniangukia miguuni na kuniomba msamaha… lakini hili (ubakaji) ni suala la mahakama,” alisema.
Alipoulizwa baba halali wa mtoto wake wa kike aliyejifungua hivi karibuni, alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo hivi sasa.
“Siwezi kulizungumzia nikifanya hivyo nitakuwa simtendei haki mwanangu. Siwezi kubadili mitizamo ya watu jinsi wanavyotafakari kuhusu jambo hili,” alisema.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga alisema awali Flora alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Flora Mjaya na kueleza alivyosimuliwa na binti huyo anayedai kubakwa na Mbasha.
Katuga alikuwa akitoa ufafanuzi huo kwa waandishi kwa vile kesi hiyo inasikilizwa katika mahakamani ya siri kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2003 sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu ili kulinda haki ya binti huyo.
Wakili alisema Flora aliieleza Mahakama kuwa Mei 23 mwaka jana, alimkuta binti huyo akiwa mnyonge huku amelala kitandani na kujifunika shuka.
Alisema alimhoji binti huyo kama alikuwa anaumwa au la lakini hakumjibu chochote.
Flora alisema siku iliyofuata Mei 24, waliondoka na kwenda kanisani yeye na watoto waliokuwapo nyumbani lakini Mbasha hakuongozana nao.
“Flora alipotoka kanisani na watoto aliwarudisha nyumbani kisha akaondoka na kwenda hotelini kwa sababu alikuwa na ‘stress’ (mawazo) lakini akiwa huko alipigiwa simu na mdogo wake Suzan (shahidi wa pili) akimueleza kile alichoambiwa na binti huyo,” alisema Katuga.
Alisema Flora baada ya kuambiwa jambo hilo kwa simu alimwambia mdogo wake huyo ampeleke binti huyo katika hoteli iliyoko Sinza.
Alisema walipofika binti huyo alimsimulia tukio hilo la kubakwa na ndipo akawaambia waende wakatoe taarifa hizo kituo cha polisi kabla ya kwenda hospitalini.
Mahakama hiyo ilisikiliza ushahidi wa Flora kwa takriban saa nne.
Awali wapiga picha walizuiliwa na ndugu zake kumpiga picha huku wakidai kuwa watawashtaki.
“Mnataka kumpiga picha za nini, mmetumwa… mnajua sheria za nchi nyinyi,” alisikika mmoja wa ndugu zake.
Tukio hilo lilizua minong’ono mingi kutoka kwa wananchi waliofika mahakamani hapo kufuatilia kesi mbalimbali.
“Jamani kwani hawa si wapiga picha… waandishi si wanaruhusiwa kuchukua matukio na kwenda kuyaripoti kulikoni hawa wazuiliwe…jambo hili linashangaza kweli kweli,” alisema mwanamke mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Tukio hilo lilimshangaza pia Wakili George Mwalali aliyekuwa mahakamani hapo ambaye alisema kitendo hicho ni kosa.
“Haiwezekani mzuiliwe kupiga picha mpo sahihi kwa sababu hapa ni nje ya Mahakama, nitakwenda kuzungumza na wakili mwenzangu juu ya jambo hili,” alisema.
Baadaye ndugu hao wa Flora waliwafuata waandishi na kuwauliza kwa nini walikuwa wakipiga picha hizo na kudai kuwa walikuwa wakiwazuia kwa vile walipata taarifa kwamba kuna mtu amewapa fedha wapige picha hizo.
“Hapana ndugu yangu, sisi hakuna aliyetupatia fedha… tunachotaka ni habari hii na si vinginevyo,” alisema mmoja wa wapiga picha.
Mmoja wa ndugu hao alisema kilichokuwa kikiwaogopesha na kuamua kuzuia utekelezaji wa hatua hiyo ni kitendo cha baadhi ya waandishi kuweka kwenye mitandao ya jamii habari ambazo si sahihi.
“Kwa mfano zile picha zilizosambazwa mwanzoni zilitushangaza kwani si za huyu binti aliyebakwa, sijui walizitoa wapi, huko ni kuchafuliana majina,” alisema.
Baada ya ndugu hao kuridhishwa na ufafanuzi waliopewa na wapiga picha waliokuwa mahakamani hapo waliwaruhusu kuendelea na kazi yao.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi April 16 mwaka huu itakapotajwa tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles