26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wamtimua rasmi Zitto

zitto kutimuliwaNa Waandishi Wetu, Dar es Salaam
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemvua rasmi uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Hatua hiyo ya Chadema imekuja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupa kesi iliyofunguliwa na Zitto dhidi ya Bodi ya Udhamini ya chama hicho na Katibu wake, Dk. Willibrod Slaa.
Kesi hiyo ilitupwa jana na Jaji Richard Mziray baada ya kupitia hoja za mapingamizi matano yaliyowasilishwa na mawakili wa Chadema.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo wa mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alizungumza na waandishi wa habari na kusema tangu Zitto alipokishtaki chama hicho mahakamani, kwa mujibu wa kanuni na maadili ya viongozi wa chama hicho, alishajifukuzisha uanachama.
“Kwa mujibu wa kanuni zinazohusu maadili ya viongozi ya chama chetu, kanuni ya 10 inaeleza kuwa pale mwanachama anapokishtaki chama mahakamani anakuwa amejifukuzisha uanachama,” alisema Lissu.
Kutokana na hali hiyo, Lissu alisema tangu walipowachukulia hatua aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Kitila Mkumbo, walishamalizana na Zitto bali kilichokuwa kimebaki ni kusubiri uamuzi wa mahakama.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya chama chao, Kanuni ya Maadili ya Wabunge na Madiwani, Zitto si mwanachama wa Chadema na wala si mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Lissu alisema kwa sasa wanafuata utaratibu wa kumwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) ili kumtaarifu kwamba Zitto si mwanachama wa chama hicho.
“Kilichobaki sasa tutamwandikia barua mwenyekiti wa NEC kutimiza tu taratibu kwamba huyu Zitto si mwanachama wa Chadema na kama tulikuwa tuna madeni tumeshalipana.
“Sasa baada ya sisi kumwandikia barua mwenyekiti wa NEC, na yeye atamwandikia Spika wa Bunge ili amwandikie tena Zitto kuwa si mbunge wala mwanachama wa Chadema.
“Itakumbukwa kuwa tangu tulipowachukulia hatua Mwigamba, Kitila na Zitto, chama chetu kilitabiriwa mauti, sasa badala ya mauti chama kimepata nguvu sana na ile migogoro ya chini kwa chini na majungu tuliyamaliza, kwa sasa tuna nguvu kubwa kuliko wakati wowote ule,” alisema Lissu.
Alipoulizwa endapo Kamati Kuu itakaa kwa siku za karibuni kujadili suala hilo, alisema hawawezi kuitisha kikao chochote kuhusu Zitto kwa sababu walishamaliza na hawana mjadala tena.
“Naomba ieleweke kwamba ule udharura wa wakati ule mara Kamati Kuu inakaa kwa ajili ya masuala ya Zitto haipo tena, kwa sababu ile mipango ya maasi tulishakamata na Kamati Kuu haiwezi kuitisha kikao cha dharura labda kuja kusherehekea ushindi.
“Katiba yetu iko wazi na kwamba ‘consequence’ (matokeo) ya kwenda mahakamani ndiyo hayo. Sasa ni kwamba aliyetushinda akaenda mahakamani sasa tumemshinda… huyu si mwanachama wetu tena na Kamati Kuu haiwezi kujadili kwa sababu kwa kwenda tu mahakamani si mwanachama ,” alisema.
Lissu alisema Kamati Kuu itakapokaa kujadili mambo mbalimbali ya chama, itatambua rasmi kuwa Zitto si mwanachama wa Chadema.
Alisema wale ambao walikuwa wakimdanganya Zitto kwa nia ya kuiharibu Chadema, sasa watafute kitu kingine.
Lissu alisema Zitto tangu akiwa naibu katibu mkuu wa Chadema, alikuwa akifahamu Katiba ya chama hicho ya mwaka 2006 ya makatazo hayo ya mwanachama kukimbilia mahakamani.
Alipoulizwa mahusiano ya Zitto na Chadema tangu alipokimbilia mahakamani yakoje, Lissu alisema chama chao hakijawahi kuwa na mahusiano yoyote tangu alipokwenda mahakamani.
Alisema kwa sasa jopo la mawakili wa chama hicho lililokuwa linashughulikia kesi hiyo, litakaa na kuandaa gharama zote za usumbufu ili waweze kulipwa na Zitto.
Hata hivyo, alipoulizwa ushirikiano ambao ulionekana kumaliza tofauti zao kati ya Chadema na Zitto, hasa katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, Lissu alisema wabunge wa chama hicho walikuwa wakiunga mkono taarifa ya Kamati ya PAC na si Zitto.
“Pale tulipomfuta nafasi ya unaibu katibu mkuu wa chama tulizungumza na Watanzania na tulifika Kigoma Kaskazini tukawaeleza wananchi kwamba kiongozi waliyemchagua amekisaliti chama na kwamba chama hakiwezi kuwavumilia kina Yuda Eskarioti, na kwamba atapata malipizi ya usaliti,” alisema Lissu.
Itakumbukwa kuwa Kamati Kuu ya Chadema iliwavua nyadhifa zao Mwigamba na Profesa Kitila kwa kuandaa waraka wa mkakati wa mabadiliko ambao ulilenga kukiangamiza chama hicho.
Katika waraka huo, Zitto anatambulika kama MM (Mhusika Mkuu), Profesa Kitila M1(Mhusika wa Kwanza) na Mwigamba M3 ( Mhusika wa Tatu).

KESI YA ZITTO
Kesi ya Zitto ilivuta hisia za watu wengi na kuwafanya wanachama wa Chadema kugawanyika makundi mawili ambapo kila ilipokuwa ikitajwa walikuwa wakijazana mahakamani.
Zitto aliomba zuio la muda asivuliwe uanachama wake na Chadema ambapo mahakama ilikubali, lakini kutokana na mgawanyiko wa wanachama, alipata wakati mgumu kwani walikuwapo waliokuwa wakimzomea na wengine walitaka kumpiga.
Wakati wote wa kesi, polisi walikuwa na wakati mgumu kumnusuru Zitto hali iliyowalazimu kutumia nguvu nyingi kutuliza ghasia na ngumi zilizokuwa zikitokea nje ya mahakama.
Mawakili wanaoiwakilisha Chadema na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, Peter Kibatala, Lissu na John Mallya waliwasilisha hoja kumpinga Zitto.
Katika mapingamizi hayo, walidai kesi hiyo kufunguliwa Mahakama Kuu haikuwa sahihi kwa kuwa ilipaswa kufunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ama Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa mujibu wa sheria na muundo wa kesi za madai.
Pia kesi ilikosewa kufunguliwa katika Masijala Kuu ya Mahakama Kuu baada ya kusajiliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Mziray alisema baada ya kupitia hoja hizo na zilizojibiwa na wadai, mahakama imeamua kukubaliana na hoja za mapingamizi yaliyowasilishwa na imeamua kutupilia mbali kesi hiyo na imeamuru Zitto kuilipa gharama za kesi Chadema.
Zitto alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Januari mwaka jana, ikapangwa kusikilizwa kwa Jaji John Utamwa na baadaye kuhamishiwa kwa Jaji Mziray.
Katika kesi ya msingi, Zitto aliiomba mahakama iiamuru Kamati Kuu ya chama hicho na chombo chochote cha chama hicho kutojadili na kuchukua uamuzi kuhusu uanachama wake hadi rufani yake itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na Baraza Kuu la chama hicho.

ZITTO: NAPIGA KAZI
MTANZANIA ilimpotafuta Zitto ili kupata maoni yake baada ya uamuzi wa mahakama kutupa shauri lake na Chadema kumfukuza uanachama, alisema kwa sasa anaendelea na majukumu yake ya kazi na hana taarifa kuhusu suala hilo.
“Kwa sasa tumetulia, ninaendelea na shughuli zangu kama kawaida… nipo napiga mzigo, ila ninashauriana na mwanasheria wangu cha kufanya baada ya kupata taarifa rasmi ndiyo tutaeleza nini cha kufanya,” alisema Zitto.

MWANASHERI WA ZITTO
Kwa upande wake, mwanasheria wa Zitto, Albert Msando, alisema hana taarifa rasmi ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu kuhusu mteja wake na kufukuzwa uanachama wa Chadema.
Katika taarifa yake kwa umma kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, Msando alidai taarifa ya uamuzi wa Mahakama Kuu alizipata kupitia mitandao ya kijamii hali ya kuwa kesi yao ilikuwa imepangwa kusikilizwa Machi 12, mwaka huu.
“Kesi awali ilikuwa imepangwa Machi 12 (kesho), lakini kwenye rekodi inaonekana ilirudishwa nyuma na maamuzi hayo kusomwa leo (jana) bila sisi kuwa na taarifa.
“Tunafanya utaratibu wa kupata nakala ya maamuzi ili kujua nini cha kufanya, hatuna taarifa rasmi za kufukuzwa Mheshimiwa Zitto uanachama,” alisema Msando.
Alisema taratibu zote zitafuata endapo watapokea taarifa rasmi kutoka mahakamani na ndani ya chama, na kusisitiza kuwa ana matumaini jambo hilo halitoleta chuki zisizokuwa na sababu kati ya wahusika.

KUELEKEA ACT
Taarifa za ndani zinaeleza Machi 14, mwaka huu, Zitto atafanya mkutano mkoani Kigoma kwa lengo la kuwaaga wapigakura wake ambapo atatangaza rasmi kujiunga na chama kipya cha siasa cha ACT-Tanzania.
Mbali na hilo, Machi 18, mwaka huu alikuwa na mpango wa kutumia Bunge kuwaaga wabunge na kutangaza safari yake mpya ya mwelekeo wa kisiasa akiwa nje ya Chadema.

SAFARI YA ZITTO CHADEMA
Zitto alishika nafasi kadhaa za uongozi Chadema kabla ‘hajakorofishana’ na viongozi wenzake. Kwanza, alikuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje mwaka 2004 na wakati huo huo akiwa pia Mkurugenzi wa Uchaguzi na Kampeni.
Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2005, alichaguliwa kuwa Katibu wa Wabunge wa Chadema.
Mwaka 2007 alichaguliwa na Baraza Kuu la Chadema kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka jana baada ya kuondolewa na Kamati Kuu ya chama hicho.
Ndani ya Bunge, Zitto alipata kuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo anaitumikia hadi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles