30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Maria Nyerere: Taifa liko njia panda

Maria NyerereNa Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
MJANE wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amesema malumbano yaliyoibuka kuhusiana na mchakato wa Katiba Mpya linalifanya taifa kuwa njia panda.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani Dar es Salaam jana, Mama Maria alisema suala hilo ni zito kwa sababu iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba ilikuwa na mikakati mizuri lakini baadaye Bunge Maalumu la Katiba likaja na yake.
Alisema yote hayo yanatokea kwa sababu ya kutokuwapo miiko ya uongozi na kwamba bila hivyo nchi haiwezi kukua.
“Tume ya Warioba ilikuwa na majaji wazuri ikaja na mikakati mizuri, Bunge la Katiba nalo likaja na ya kwake, wanaohojiwa wana akili na yote yaliyotokea wameyaona. Sasa bila miiko ya maadili ya uongozi nchi haiwezi kukua.
“Miiko ya uongozi ni lazima na ikiwa viongozi hawana, halafu tukae tunabishana tu. Ninyi mkaandike hili kwa msamiati mnaoona inafaa,”alisema Mama Maria huku akionekana kutounga mkono Katiba Inayopendekezwa.
Kuzushiwa kifo
Akizungumzia kuhusu kuzushiwa kifo, alisema yote hiyo inatokana na hofu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kwamba katika kipindi hiki ni kawaida kuwapo uzushi wa aina hiyo.
Alisema hofu hiyo ya uchaguzi inatokana na makundi ambayo yanataka kugombea urais wa mwaka huu hivyo yanashindana kwa kuzushiana mambo mbalimbali.
“Sasa sijui marehemu anaongeaje (anacheka)…sasa kwa kifupi kwa kawaida inapofika kila uchaguzi huwa kuna watu wanapitapita, wengine wanapiga simu, wanaotukana wanatukana hivyo mimi halikunishtua ndiyo nikasema waiteni waandishi wa habari waje wamwone marehemu anayezungumza.
“Inawezekana ni mtu kawaza akapata mawazo na akaamua kuzusha tu. Sasa baada ya kuzushiwa nilikuwa napigiwa sana simu mara mtu anakupigia hujambo ukimjibu anakwambia nilikuwa nakuamkia tu.
“Mkamwana wangu alinipigia simu akasema mama hujambo baadaye akabadilisha sauti akasema huyu hatanielewa nikacheka lakini yeye akalia kwa sauti na akaweka simu chini,”alisema Mama Maria ambaye wakati wote alikuwa akitabasamu.
Alisema yote hayo ni hofu ya taifa na hata dunia nzima lakini yote ni ya kawaida.
“Hebu na ninyi waandishi mniambie mlipokeaje kifo changu? “alihoji mjane huyo wa Baba wa Taifa huku waandishi wakimjibu kuwa taarifa za kifo chake zilishtua taifa.
Alipoulizwa alijisikiaje mara ya kwanza aliposikia kazushiwa kifo alisema; “Ujue sisi ni wanaombi huwa tunafunga tunaombea ulimwengu mzima na huwa tunafunga kwa ajili hiyo.
“Sasa niliposikia nilifurahi nikasema sasa Novena yangu imefanya kazi. Tukasema shetani amechemka na amepata kipigo kwa sababu mashetani yalikuwa yakifanya fujo,” alisema.
Alipoulizwa nini kifanyike ili hofu hiyo isiendelee alisema; “Kungefanyika maombi ya siku nzima na nchi nzima ili tokemeshe haya yote”.
Akizungumzia kuhusu mtoto wake, Makongoro Nyerere, kutajwa kugombea urais alisema hana tatizo kwa sababu ni raia kamili kama walivyo wengine.
“Makongoro ni Mtanzania mwenzetu ni raia kamili hivyo ana haki ya kufanya apendavyo mradi asivunje sheria za nchi,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles