25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

ETHIOPIA YAMALIZA MGOGORO WA MPAKA NA ERITREA

ADDIS ABABA, ETHIOPIA


CHAMA tawala nchini Ethiopia, People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kimetangaza kutekeleza makubaliano ya amani ya Algiers yanayohusu mpaka wa Eritrea na Ethiopia bila ya masharti yoyote.

Kwa mujibu Kituo cha Televisheni ya Taifa (Fana), Taifa hilo litafanya kazi kwa bidii kuyatekeleza makubaliano hayo baada ya awali kugoma kuyatekeleza.

Tangazo hilo linamaanisha Ethiopia inakubali uamuzi wa ugawaji wa mipaka uliofikiwa mjini Algiers, Algeria mwaka 2000, ambao uliipa Eritrea haki ya kumiliki maeneo waliokuwa wakiyazozania ikiwa ni pamoja na mji wa Badme.

Licha ya makubaliano hayo, Ethiopia bado imeweka wanajeshi wake katika eneo hilo.

Aidha, mapema juzi wabunge wa Ethiopia walipiga kura ya kuunga mkono uondoaji wa hali ya hatari iliyokuwa imetangazwa nchini humo.

Hali hiyo ya hatari ya hivi karibuni iliwekwa katikati ya Februari baada ya kutokea maandamano makubwa dhidi ya Serikali katika maeneo ya Oromia na Amhara.

Hatua za kukubali makubaliano hayo ya amani na Eritrea na kuondosha hali ya hatari ni mabadiliko muhimu ya karibuni chini ya uongozi wa Waziri Mkuu mpya, Abiy Ahmed ambaye amekuwa akizungumzia wazi juu ya haja ya kuleta mageuzi.

Raia wa Eritrea 54,000 walipoteza makazi wakati wa mapigano kati ya Ethiopia na Eritrea mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Hali kadhalika, waziri mkuu huyo amewaachilia huru wafungwa wa kisiasa na kuanzisha mazungumzo na makundi ya upinzani tangu aingie madarakani Aprili.

Mbali na hayo, Ethiopia pia imesema jana kuwa shirika lake la simu linaloendeshwa na Serikali pamoja na shirika la usafiri wa ndege yatakaribisha uwekezaji wa sekta binafsi.

Ni sera muhimu ambayo inatarajiwa kupunguza udhibiti wa Serikali katika uchumi wa nchi.

Taifa hilo la Afrika Mashariki lenye idadi ya watu wapatao milioni 100, linaongoza barani Afrika kwa kuwa na uchumi unaodhibitiwa na Serikali.

Muungano tawala wa EPRDF, ambao umekuwa madarakani tokea 1991, kwa muda mrefu umekuwa ukiunga mkono uchumi unaodhibitiwa na Serikali.

Lakini muungano huo umesema jana kwamba Ethiopia inahitaji mageuzi ya kiuchumi ili kupata ukuaji wa haraka na kuimarisha mauzo yake ya nje ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles