MADRID, HISPANIA
MSHAMBULIAJI mpya wa Real Madrid, Eden Hazard, amekabidhiwa jezi namba 7 ambayo alikuwa anaitumia aliyekuwa nyota wa timu hiyo Cristiano Ronaldo.
Hazard ambaye alikuwa anakipiga katika kikosi cha timu ya Chelsea kwa miaka saba, alikuwa anavaa jezi namba 10 kwenye timu hiyo kwa kipindi chote, lakini msimu ujao wa Ligi Kuu nchini Hispania ataonekana akiwa na uzi namba 7.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amejiunga na Real Madrid kwa mkataba wa miaka mitano, lakini atajiunga rasmi Julai 1 mwaka huu.
Wachezaji ambao wamewahi kuvaa jezi namba 7 katika kikosi cha Real Madrid ni pamoja na Cristiano Ronaldo (2010-2018), Raul Gonzalez (1994-2010), Emilio Butragueno (1985-1995) Juanito (1977-1985) Amancio Amaro (1962-1976) na Raymond Kopa (1956-1959).
Baada ya Ronaldo kuondoka katika kikosi cha Real Madrid na kujiunga na Juventus msimu uliopita, jezi namba hiyo ilikuwa inavaliwa na Mariano Mejía aliyejiunga mwaka jana akitokea timu ya Lyon, lakini sasa inabidi abadilishiwe baada ya kusajiliwa Hazard.
Uhamisho wa Hazard ulikamilika Ijumaa wiki iliopita kwa kitita cha pauni milioni 150 na kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Real Madrid kwa kitita kikubwa cha fedha katika historia ya timu hiyo.
Hazard kupitia ukurasa wake wa Instagram aliwashukuru mashabiki wa Chelsea pamoja na wachezaji wenzake kwa sapoti waliompa kwa kipindi chote cha miaka saba.
“Ninaamini kila mmoja sasa anaelewa kwamba natakiwa kufunua ukurasa wangu mpya wa maisha, nadhani kila mmoja ana ndoto ya kufanya jambo fulani na muda ukifika lazima afanye hivyo.
“Kuondoka Chelsea ni jambo kubwa pia ni maamuzi magumu sana katika maisha yangu ya soka. Lakini kwa sasa kila kitu kipo wazi, natakiwa kuyapenda maisha yangu wakati nipo Chelsea.
“Nilijitoa kwa kila namna, nilihakikisha ninapambana hata kama matokeo yalikuwa mabaya, nawashukuru sana mashabiki kwa sapoti.
“Moyo wa kupambana, kutokata tamaa ilikuwa ni sehemu ya utamaduni wa Chelsea, nitaendelea kuyakumbuka mengi na bado nitaendelea kuwa shabiki wa timu hiyo,” alisema Hazard.