22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wajue viungo walioshika roho za timu 20

MOHAMED KASSARA

LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018-19 imemalizika hivi karibuni, kwa kuishuhudia Simba ikitwaa ubingwa huo, huku timu za Stand United na African Lyon zikishuka daraja hadi Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Msimu huo, ulikuwa na michezo mingi kutokana na kuongezea kwa timu kutoka 16 za awali hadi 20.

Wachezaji wengi walitoa mchango mkubwa kwa timu zao.

Mabeki walifanya kazi yao ya ulinzi, washambuliaji walifunga mabao yalisaidia timu zo kuondoka na pointi tatu muhimu.

Washambulaji  Meddie Kagere, Heritier Makambo, Salim Aiye walikuwa rafiki wa nyavu.

Kelvin Yondani, Erasto Nyoni na Agrey Morris nao walifanya kazi kubwa ya kupambana na washambuliaji hao hatari.

Eneo la kiungo ni sehemu muhimu kwa uhai wa timu yeyote.Eneo hilo linaunganisha kati ya yale ya ulinzi na ushambuliaji.

Kifupi ndio uti wa mgongo wa timu yeyote, hivyo ni sehemu muhimu mno.

Kama eneo hilo litakuwa na upungufu kuna uwezekano mkubwa wa timu  kushindwa kupata matokeo mazuri.

Makala haya yanakuletea viungo 20 waliokuwa mhimili  mkubwa kwa timu zao msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mkude-Simba

Alikuwa na kazi kubwa ya kutengeneza uwinano kwenye kikosi cha Simba, uwezo mkubwa wa kumiliki mpira , kupiga pasi sahihi, kutuliza kasi ya mchezo na kuchezesha timu.

Viitu viliisadia Simba kuteka eneo la kiungo na kutawala michezo mingi.

Ufanisi wake uliwafanya Clatous Chama na Haruna Niyonzima kufanya kazi zao kwa uhuru mkubwa.

Ajib –Yanga

Ajib alikuwa mchezaji muhimu wa Yanga katika msimu uliopita akiisadia kumaliza nafasi ya pili.

Alimaliza msimu uliopita akiwa amepiga pasi 15 zilizozaa mabao, akiwazidi viungo wa timu zote 20.

Mabao mengi yaliyofungwa na Makambo yalitokana na pasi za Ajibu.

Sure boy- Azam FC

Kiungo huyo  ndiye roho ya Azam kwa miaka mingi.

Licha ya timu hiyo kuwa na viungo wengine kama Stephan Kingue, Mudathir Yahya, Frank Domayo na Salimin Hoza, bado Sure Boy amekuwa chaguo la kwanza kwenye eneo la kiungo mchezeshaji.

Licha ya udogo wa umbo lake, lakini utulivu na jicho la pasi za mwisho zinamuweka katika daraja tofauti na viungo wengine wa timu hiyo.

Aliamua timu ishambulie vipi, mpira uende wapi na kwa wakati gani, hata timu inapokuwa inahitaji kuutunza mpira usipotee kirahisi, basi kiungo huyo amekuwa akiifanya kazi hiyo kwa ufasaha mkubwa.

Ubora wake pia uliisadia Azam kutwaa ubingwa wa Kombe la  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu Kombe la Azam na kurejea katika michunao ya kimataifa.

 Nditi-Mtibwa Sugar

Nditi ni miongoni mwa viungo wakongwe katika Ligi Kuu.

Licha ya ukongwe wake, bado ana kiwango kizuri cha kuiendesha Mtibwa Sugar.

Anasifika kwa utulivu, nidhamu na akili ya kuusoma mchezo.

Amekuwa kiongozi wa kiungo cha ulinzi cha timu hiyo akisadiana na Henry Joseph.

Keny-Singida United

Kiungo huyo yupo kwenye rada za Yanga, wakisaka saini yake.

Kenny ndiye mhimili mkuu wa eneo la kiungo la Singida United aliyojiunga nayo msimu uliopita akitokea Mbeya City.

Kenny alikuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo, alipokosekana hasa katika kipindi cha mwishoni mwa msimu.

Singida United ilianza kupoteza dira na kupoteza michezo hatua iliyosababisha kujikuta katika nafasi za kugombania kujiokoa na kushuka daraja.

Mvuyekure-KMC

Hakuna shaka kwamba KMC ilikuwa miongoni mwa timu zilizowapa joto vigogo wa soka Simba, Yanga na Azam FC  msimu uliopita.

Kati ya wachezaji walikuwa wanaipa jeuri timu hiyo ni kiungo kipenzi cha kocha wa timu hiyo, Etiene Ndayiragije, Emmanuel Mvuyekure.

Mvuyekure ni kiungo wa shoka kweli kweli, kutokana na uhodari wake kumiliki mpira kupiga pasi sahihi na kupiga chenga.

Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochangia mafanikio ya timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne ukiwa ni ushiriki wake wa kwanza katika Ligi Kuu, baada ya kupanda daraja.

Balama-Alliance

Alliance ilikuwa na msimu bora chini ya Kocha, Malale Hamsini aliyeichukua timu hiyo kati kati ya msimu.

Ilitambulisha wachezaji vijana wenye vipaji, mmoja wao ni Balama Mapinduzi ambaye alionyesha kiwango cha juu.

Balama mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira,kupiga pasi makini na kupandisha timu anazitoa udenda Yanga, Simba na Azam.

 Elifadhali- Prisons

Elifadhali ni kiungo wa ulinzi wa Prisons ambaye alikuwa msaada mkubwa kwenye kikosi hicho.

Akiwa na urefu wa kutosha na mwili uliojengeka kwa mazoezi, alikuwa mhimili mkuu wa safu ya kiungo cha Wajela jela hao  na kuisadia kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kama ilivyo kwa Nditi, Elifadhali anasifika pia kwa uwezo wake mkubwa wa kuzuia mashambulizi, kumiliki mpira na kupiga pasi sahihi.

 Massawe-Stand United

Licha ya Stand United kushuka daraja, lakini Jacob Masawe alipiga kazi ya maana kwenye eneo la kiungo na kuifanya timu hiyo kusumbua msimu uliopita.

Alikuwa mchezaji kiongozi ambaye mbali na uwezo wa kufunga, pia alikuwa na jukumu la kudhibitia eneo la kiungo.

 Tangalu-Lipuli Fc

Fredy Tangalu si jina maarufu sana kwenye soka la Tanzania, lakini ubora aliouonyesha msimu uliopita akiwa na kikosi cha Wana Paluhengo kilikuwa cha juu.

Ni fundi wa kupiga pasi na kumiliki mpira, ni miongoni mwa wachezaji waliosadia Lipuli kucheza  fainali ya Kombe la TFF.

Samatta-Mbeya City

Ni kaka wa damu wa nahodha waTaifa Stars, Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji.

Mohamed Samatta ni kiungo mchezeshaji wa Mbeya City, ambaye licha ya staili yake ya kucheza taratibu, pia anasifika kwa umakini awapo na mpira, kupiga pasi murua na kutengeneza nafasi za kufunga.

Uwezo huo uliifanya Mbeya City ambayo pia inafahamika kama Wagonga Nyundo kusumbua msimu uliopita.

Seseme-Mwadui FC

Kiungo huyo ambaye anasifika kwa udambwi dambwi mwingi awapo na mpira, jicho la kupiga pasi na kupiga chenga za maudhi zilizowavuruga wapinzani.

Abdalah Seseme ni fundi wa mpira anaweza kufanya lolote akiwa na mpira na kuwavuruga kabisa viungo wa timu pinzani, waulize Tshishimbi, Feisal Salumu, walitoka hoi siku hiyo walipokutana na Mwadui.

Abushee- Coastal Union

Issa Abushee ni miongoni mwa wachezaji  waliopiga kazi ya maana kwa Wagosi wa Kaya.

Kiungo huyo ndiye alikuwa anaratibu mipango yote ya ushindi ya kikosi hicho kilichorejea Ligi Kuu msimu uliopita, baada ya kushuka daraja.

Licha ya uwepo kiungo mkongwe Athuman Idd ‘Chuji’, Abushee alikuwa chaguo sahihi la kocha Juma Mgunda.

Msala-Ruvu Shooting

Shaaban Msala ni miongoni wanaochipukia.

Alifanya vizuri msimu uliopia akiiongoza Ruvu Shooting katika eneo la kiungo.

Ndiye alikuwa silaha muhimu kwenye kikosi hicho kutokana na ufundi wake wa kuuchezea mpira, kupiga pasi makini na kutengeneza nafasi kufunga mabao.

Kazimoto-JKT Tanzania

Mwinyi Kazimoto ni miongoni mwa viungo wa shoka, anasifika kwa uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga pasi murua na pasi za mwisho.

Alikuwa  mhimili wa safu ya kiungo ya timu hiyo, akiisadia timu hiyo kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Said- Mbao

Kiungo huyo mshambuliaji wa Mbao anasifika kwa jicho la goli, kumiliki na kupiga pasi za uhakika.

Said Said alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotoa mchango mkubwa wa kutengeneza nafasi nyingi za mabao pamoja na kufunga .

Atakumbukwa kwa kufunga bao lililoisababishia Simba kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Jabir Aziz-African Lyon

Aziz ni miongoni mwa wachezaji waandamizi katika  Ligi Kuu.

Ni mtaalamu wa kupiga pasi fupi na ndefu aliyetakata na Lyon iliyoshuka daraja.

Mohamed-Ndanda FC

Muhsin Mohamed ni mmoja wa viungo ambao hawakutajwa sana , lakini kazi aliyopiga ilionek katika kikosi cha Wana Kuchele.

Ilikuwa rahisi kwa Ndanda kushinda kama Mohamed alikuwa kwenye kiwango chake, alishiriki kutengeneza mabao mengi ya Vitalis Mayanga, aliyemaliza kinara wa mabao kwenye timu hiyo.

Kassim Khamis-Kagera Sugar

Kassim Khamis alikuwa miongoni mwa wachezaji waliong’ara zaidi kwenye kikosi hicho msimu uliopita.

Ndiye alikuwa akiratibu mwenendo wa timu hiyo, kushambulia na kuzuia.

alitengeneza nafasi nyingi zilizotumiwa na wenzake kufunga mabao.

Mpakala-Biashara United

Juma Mpakala ni kiungo wa ulinzi aliyekuwa injini ya timu ya Biashara ya Mara.

Alikuwa kila kitu kwenye eneo la kiungo la timu hiyo, alikaba, akamiliki mpira na kupiga pasi zilizoifanya timu hiyo kutakata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles