24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

DPP ATATHMINI UPELELEZI KESI YA NIDA

Na Kulwa Mzee -Dares Salaam


JALADA la kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake, lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kutathmini upelelezi uliofanyika.

Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.16 ilipokuwa inatajwa.

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, kwamba upelelezi haujakamilika akaomba kesi iahirishwe.

Hakimu Mwijage alisikiliza na kukubaliana na hoja za Jamhuri, kesi ikaahirisha hadi Aprili 20, mwaka huu kwa kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Maimu, Meneja Biashara wa NIDA, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa TEHAMA,Joseph Makani.

Wengine ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Inadaiwa katika hati ya mashtaka kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1,169,352,931.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa Maimu na Mwakatumbula kati ya Januari 15 hadi 19, mwaka 2010 makao makuu ya NIDA  wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo,  walitumia madaraka  vibaya.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na  Benki Kuu ya Tanzania,   kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

Maimu na Mwakatumbula katika shtaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo, walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wanadaiwa Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh milioni 6 kwa GIL bila ya kupiga hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 14,661,676.76.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya NIDA waliidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni na kuisababishia NIDA kupata hasara ya Sh 167,445,676.76.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles