27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

CUF MAALIM WAKESHA WAKILINDA OFISI Z’BAR

Na Waandishi Wetu-Dar/Zanzibar


WAKATI Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Ibrahim Lipumba, ikiendelea na vikao vyake Dar es Salaam, wafuasi zaidi ya 100 wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad wamekuwa wakikesha kulinda ofisi za Makao Makuu Zanzibar.

Hatua hiyo imekuja baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita, Profesa Lipumba kutangaza uteuzi wa wakurugenzi wa upande wa Zanzibar na kuahidi kwenda kuwakabidhi ofisi wiki hii Visiwani humo.

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA imeshuhudia kundi la wanachama hao wa CUF Zanzibar wanaomuunga mkono Maalim Seif wakilinda ofisi za chama hicho zilizopo Mtendeni na Vuga kwa lengo la kuwazuia wakurugenzi hao.

Hatua hiyo imekuja baada ya Maalim Seif kuwataka wafuasi wake juzi mjini Unguja kwamba wawe tayari kulinda ofisi za chama hicho na kupinga uteuzi wa wakurugenzi hao, huku wakiwaita ni feki.

Alisema hila zinazofanywa na Profesa Lipumba ni za makusudi, huku akisema jambo la muhimu ni kuhakikisha wanachama na viongozi wote wasiokubaliana naye wanaungana ili kuhakikisha kuwa hakuna uovu ama ukiukwaji wa sheria utakaofanywa ndani ya chama hicho.

“Ni lazima tulinde chama pamoja na viongozi wake na si vinginevyo, CCM wamekuwa wakifanya kila aina ya majaribu dhidi ya CUF kwa lengo la kumpotezea muda Maalim Seif, ila sisi kama wanachama katu hatukubali.

“Tutasimama imara kulinda kila aina ya mali na hata viongozi, lakini si kuwaruhusu hao wanaoitwa wakurugenzi wa Bwana Yule (Lipumba) kuingia hapa. Ninarudia tena, kama wakithubutu kuingiza hata pua habari yao wataipata,” alisema Masoud Salim Faki ambaye ni mwanachama wa CUF.

MTANZANIA ilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, ambaye alisema kuwa kauli ya Katibu Mkuu wake Maalim Seif ni ya kujihami na yenye hofu dhidi ya jambo fulani.

“CUF ni taasisi na ina ofisi mbili, moja ipo Zanzibar Mtendeni na Dar es Salaam Buguruni na Katiba inaeleza kuwa kiongozi yeyote wa chama ana haki ya kufanya kazi katika eneo lolote.

“Tunazo taarifa kuwa amechukua vijana kutoka shamba kama 100 ambao tangu jana (juzi) wamekuwa wakilinda ofisi ya Vuga na Mtendeni jambo ambalo anawapotezea muda tu hawa vijana,” alisema Sakaya.

Kutokana na hali hiyo, alisema wao wameendelea na vikao vya kawaida vya kuimarisha chama kuanzia juzi na jana ambapo wakurugenzi wote wanaotambulika kwa mujibu wa Katiba wamehudhuria.

Alisema ofisi za chama haziwezi kuwa kama mali au kampuni ya mtu binafsi kwani siku zote wenye mali zote huwa ni wanachama na si vinginevyo.

“Wakurugenzi walioteuliwa wataendelea na majukumu yao kwa upande wa Zanzibar na hata Bara maana hufanya kazi siku zote kwa pamoja na eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoelekezwa kwa mujibu wa Katiba ya CUF,” alisema Sakaya.

Wiki iliyopita, Profesa Lipumba alitangaza uteuzi wa wakurugenzi wapya na manaibu wao ambao ni Nassor Seif (Mipango na Uchaguzi), Mbunge wa zamani wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Kurugenzi ya Mambo ya Nje), Haroub Mohamedi Shamis (Naibu Fedha na Uchumi), Masoud Ali Said (Naibu Habari na Uenezi) na Thiney Juma Muhamed  akiteuliwa kuwa Kamanda wa Blue Guard Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles