26.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 26, 2022

DK.SLAA: MVUMILIENI JPM

*SASA afikiria kurejea nchini


Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

BAADA ya kuishi nchini Canada kwa zaidi miaka miwili sasa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa amesema anakuna kichwa ili kupima mazingira yaliyomfanya aondoke nchini na familia yake kama yapo au laa.

Septemba,2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu Dk. Slaa alijiweka kando na siasa, kwa kile alichokieleza kutofautiana na chama chake juu ya masharti ya kumpokea aliyekuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),Edward Lowassa.

Hata hivyo Dk. Slaa ambaye amekuwa mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu mfululizo, hakuweza kuainisha mazingira yaliyomfanya aondokea nchini na kwenda kuishi ughaibuni. 

“Sina tabia ya kuyumbishwa…sina chuki na mtu yeyote, sipendi siasa za udanganyifu na propaganda. Nimeachana na siasa tangu Julai 28,2015, baada ya kuona misingi ya chama nilichoshiriki kukijenga imepotoshwa,”alisema Dk. Slaa siku alipotangaza kuachana na siasa.

Pamoja na mambo mengine, alisema sharti la kwanza ambalo alitaka Chadema izingatie ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya serikali ya CCM, kujisafisha dhidi ya tuhuma ya kashfa ya sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa Waziri Mkuu.

 

Kurudi nchini

Akizungumza na MTANZANIA akiwa nchini Canada jana, Dk. Slaa alisema amemaliza masomo yake na baada ya kufanya tafakari atarejea nchini wakati wowote.

“Ni kweli nimemaliza masomo yangu. Bado napima mazingira yaliyonifanya niondoke na familia yangu. Baada ya hapo tutaangalia uwezekano wa kurejea,”alisema.

 

Alisema kuhusu matarajio yake ya kisiasa, watu wameshindwa kumwelewa siku ambayo alitangaza kustaafu siasa za vyama.

 

Alisema alichomaanisha ni kwamba, pamoja na kuachana na siasa za vyama,atakuwa tayari kupiga kelele pale anapoona masilahi ya Taifa yanaumia.

“Hadi sasa sijapiga kelele kwa kuwa sijaona masilahi ya Taifa yakiangamizwa, hatua mbalimbali zinazochukuliwa ni kweli zinawaumiza wasiohusika.

“Ndio maana nilitumia katika makala mojawapo mtego wa panya huwakamata wanaohusika na wasiohusika. Hivyo, makosa madogo mimi hayanisumbui kwa kuwa hakuna binadamu kamilifu ,”alisema.

 

Rais Magufuli

Akizungumzia utendaji wa Rais Dk. John Magufuli, alisema watu waelewe hakuna nchi hata moja ambapo kiongozi atakubalika na watu wote kwa asilimia 100.

Alisema wako watu ambao masilahi yao yataguswa kwa namna moja au nyingine hivyo lazima watapiga kelele.

Kutokana hilo, alisema Rais Dk. Magufuli katika kundi ambalo halihitaji fedha ameyatekeleza yote kwa asilimia 99.9, ikiwa ni pamoja na uwajibikaji serikalini, kuchukua hatua kali dhidi ya rushwa, uwizi wa mali za umma, uwindaji haramu na kudhibiti dawa za kulevya.

“Hatua zote zimechukuliwa,zinapaswa kuwa endelevu. Kwa bahati mbaya mchwa wengine waliopenya mpaka ndani ya Ikulu na Serikali na huwezi kufagia Serikali nzima kwa siku mmoja.

“Kwa jinsi Rais ambavyo hayumbi na wala hayumbishwi, nina hakika atafikia malengo na kurudisha Taifa kwenye misingi ya tunu za Taifa ya uwazi, ukweli, uadilifu, kuheshimiana na kuthaminiana na hasa kujali utu.

“Hii ndiyo hali ambayo JPM kila siku anaiita ‘Transition’ (kipindi cha mpito). Tutafika tu, tunatakiwa kuwa wavumilivu na wenye uzalendo wa kweli ana nia njema ya kufikisha Taifa mahali pazuri. Hii inahitaji kuweka pembeni maslahi yetu binafsi kama mtu mmoja mmoja, viongozi wa Serikali au hata wa kisiasa,”alisema Dk. Slaa.

 

Upinzani

Kuhusu mwenendo huo endapo utasaidia upinzani kuingia Ikulu 2020, Dk. Slaa alisema wakija na ajenda mbadala na makini yenye kuwalenga wananchi moja kwa moja itawasaidia.

Dk. Slaa ambaye pia alipata kugombea urais kupitia Chadema mwaka 2010, alisema endapo wataendelea kurukia kauli za Rais, basi upinzani utafutika kabla ya 2020.  

“Kama nilivyorejea mara kadhaa, upinzani makini utaingia Ikulu kwa ajenda mbadala. Ajenda makini yenye kuwalenga wananchi moja kwa moja katika kuwatoa kwenye kero zao mbalimbali. 

“Hadi sasa ninachoona ni ‘kurukia’ kauli za JPM, lakini kauli si ajenda na hatupeani maksi kwa kuzungumzia usahihi wa lugha. Wako wanaotazama usahihi wa lugha na mahali pa kutazama usahihi huo. Kimsingi hayo ni masuala ya darasani au kwenye uandishi wa vitabu.

“Aidha kumtuhumu JPM kukiuka Katiba na sheria nayo haina tija. Wote wanaomtuhumu wanajua kuwa wakiambiwa waonyeshe kifungu mahususi alichokiuka yeye mwenyewe katika utendaji wake hawana majibu ya kuridhisha.

“Hivyo mimi sijaona mwenendo wa JPM unaosaidia kuingiza upinzani Ikulu. Isitoshe kama hawatakuja na ajenda makini na mkakati ulioandaliwa unaowatoa wananchi hapa walipo kwenda kwenye raha, upinzani unaweza kufutika kabla ya 2020,”alisema Dk. Slaa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,803FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles