29.3 C
Dar es Salaam
Saturday, May 28, 2022

SEKTA YA HOTELI INAPATA HASARA KWA ASILIMIA 40

NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM


MAPENDEKEZO ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 , yaliyosomwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, yametoa jibu la sababu ya kilio cha wafanyabiashara wengi nchini.

Katika sehemu ya mapendekezo hayo, iliyozungumzia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo kwa kiasi kikubwa ililenga kubana matumizi, inasema fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa hadi Februari mwaka huu ni asilimia 34 pekee ya lengo.

Tafsiri ya hatua hiyo ni kwamba, fedha nyingi zilizotolewa ni za mishahara na matumizi mengineyo, hivyo kiasi kikubwa kilichotarajiwa kitolewe kwa ajili ya shughuli za maendeleo hazijatolewa, jambo linaloonesha mzunguko wa fedha mitaani lazima utakuwa mdogo.

Hotuba ya Dk. Mpango iliyosomwa mbele ya wabunge inasema, mwaka 2016/17 Serikali ilitenga Sh trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kati yake Sh trilioni  8.7 zikiwa za  ndani Sh trilioni 3.11 za nje.

Taarifa hiyo inasema jumla ya fedha zote za maendeleo zilizotolewa hadi Februari mwaka huu, zikiwamo za nje na za ndani na nyingine za  matumizi ya kawaida ambazo zimetumika katika mafungu mbalimbali kwa shughuli zenye asili ya maendeleo ni Sh trilioni 4.168 sawa na asilimia 35.26 ya lengo.

Ufinyu huu wa kutoa fedha za maendeleo, umeathiri sekta mbalimbali ikiwamo ile ya hoteli ambayo kwenye bajeti iliyobakisha miezi mitatu kwisha, maazimio ya taasisi za serikali kutofanya mikutano kwenye hoteli yalipitishwa.

Pia Bunge hilo lililopitisha bajeti hiyo, linadaiwa pia kupitisha kodi mbalimbali ikiwamo za utalii, vibali vya kuja nchini (Visa), na nyingine ambazo kwa ujumla zimetajwa kuathiri sekta hiyo kwa watalii kupungua pamoja na mikutano mingi ya kimataifa kuhamishiwa kwenye nchi jirani.

 

 Kwa mujibu wa mtandao wa hotels combined .com, Dar es Salaam pekee ina  hoteli 242 kati yake, zile za nyota moja 177,  nyota mbili nane, nyota tatu 31, nyota nne 19 na nyota tano zipo saba.

Akizungumza na Mtanzania, Mkurugenzi  Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Latifa Sykes, anasema biashara ya hoteli ni mbaya ukilinganisha na ilivyokuwa  miaka miwili iliyopita.

Anasema kinachoumiza zaidi kwenye biashara hiyo kwa sasa ni kukosa mapato kutokana na kukosa mikutano ya nje kwa kuwa wateja waliokuwa wakija wamehamia nchi za jirani zikiwemo Rwanda  na Kenya.

Anasema hali hiyo inasababishwa na kupanda kwa kodi za Visa ya biashara ambayo imatoka dola za Marekani 50 hadi 250.

 “Zamani wakati tozo ilipokuwa dola 50, walikuwa wakija kwa wingi lakini wameacha kwa madai kuwa tozo ni kubwa sana na kwamba hawawezi kulipia kiwango hicho kipya.

 “Kwa upande wetu sisi wadau hasa wenye mahoteli ya mijini kutokana na kukosa mikutano pato letu limeyumba na hali imekuwa mbaya,”alisema

Sykes anasema hoteli zenye nafuu kwa sasa ni zile za kitaalii zilipo porini, lakini za mijini ambazo pamoja na mambo mengine zilikuwa zikitegemea mikutano, sasa ziko kwenye hali mbaya.

“Wanaopeleka watalii mbugani (Camping), ambazo zinalenga wateja wao maalum ambao ni wale wenye kipato cha juu kidogo bado wana nafuu,” anasema.

Anasema kwa sasa mapato ya hoteli za mijini yamepungua kwa zaidi ya asilimia 40.

Taarifa mbalimbali zinaonyesha, mwaka 2016,  baadhi ya  wamiliki wa mahoteli walishindwa kurejesha mikopo mbalimbali waliyokopa kuendesha biashara zao jambo lililofanya takribani hoteli 405 zipigwe mnada nchini.

Mojawapo ya hoteli zilizopigwa mnada ni pamoja na Hoteli ya Tamali iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam ambayo iliuzwa kwa Sh bilioni 1.1 ambapo thamamni yake ilikuwa bilioni 2.2 na iliuzwa kutokana na kushindwa kulipa deni la Sh bilioni 1.6

Meneja wa Hoteli maarufu ya Rombo Green view, iliyopo maeneno ya Shekilango jijini Dar es Salaam, Benjamin Robert, anasema hali ya biashara kwa upande wa hoteli imekuwa ngumu hasa baada ya serikali kupiga marufuku taasisi zote za kiserikali kufanyia mikutano kwenye kumbi za binafsi.

“Tumeathirika kwa asilimia 100, miaka miwili iliyopita tulikuwa tunapata sana mapato kutoka kwa mikutano iliyokuwa ikifanywa na taasisi mbalimbali za serikali.

“Kwenye kumbi zetu kwa wastani tulipata mikutano minne hadi mitano kwa siku, kwa sasa mwezi mzima unapita na hatupati mkutano hata mmoja,”alisema

 Robert alishauri Serikali kufungua mianya kama ilivyokuwa awali angalau kwa kiasi kidogo, ili kuendeleza ushirikianao na wadau binafsi na pia kuimarisha  mapato kwa Watanzania ambao wanafanya juhudi ya kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wa tozo za kodi, Robert anasema ni changamoto kubwa kwa wamiliki wa mahoteli kwa madai kuwa tozo zimekuwa nyingi na wakati huohuo hali ya kibiashara imekuwa mbaya.

Akielezea hali ya uchumi wa taifa katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, anasema wageni walioingia nchini mwaka 2016 kwa ni wageni ikilinganishwa na mwaka 2015.

“Hivyo madai kuwa watalii wameikimbia Tanzania kwa sababu ya VAT kwenye baadhi ya huduma za utalii hayana msingi, na kama nia ni kutolipa kodi na wakati huohuo Serikali inadaiwa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii na huduma nyingine kwa wananchi, hilo halikubaliki!

“Nawaalika wadau wa sekta ya utalii waje wajenge hoja zenye mashiko wakati wa mapitio ya marekebisho ya kodi kwa ajili ya bajeti ya 2017/18,”alisema.

Taarifa za serikali zinaonyesha kuwa, Januari hadi Machi, mwaka jana, idadi ya watalii waliongia nchini ilikuwa 284, 378  kipindi kama hicho mwaka 2015, walikuwa ni 265,490.

Zinasema pia kwamba, robo  ya pili ya mwaka 2016, watalii walikuwa 239,221 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2015 ambapo walikuwa 242,460.

Pia katika pikindi cha robo ya tatu ya mwaka 2015, jumla ya watalii 335,610 waliingia nchini ambapo mwaka 2016 jumla ya wageni 369,355 walikuja nchini.

Hata hivyo wadau wa utalii wamekuwa wakipinga takwimu hizo wakisema,  kinachofanywa naserikali sasa ni kutaja idadi ya watu wote walioingia nchini bila kujali wamekuja kwa shughuli gani.

Ripoti ya  ya nusu mwaka ya hali ya uchumi iliyotolewa na Benki kuu ya Tanzania (BOT), imeonyesha kuwa pato la Taifa (GDP) limeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi cha robo tatu mwaka wa 2016  ukilinganisha na hali iliyokuwepo mwaka 2015 ambapo ilikuwa asilimia 6.3

Ripoti hiyo ikafafanua kuwa ongezeko hilo limetokana na maboresho katika sekta mbalimbali  zikiwemo sekta mbalimbali za usafirishaji na kuhifadhi kwa asilimia 15.4, sekta ya ujenzi kwa asilimia 11, sekta ya habari na mawasiliano kwa asilimia 9.5, sekta ya biashara ya jumla na rejareja kwa asilimia 9 na ya madini kwa asilimia 9. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,631FollowersFollow
542,000SubscribersSubscribe

Latest Articles