24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein aongoza mazishi ya Brigedia Jenerali Faki

MWANDISHI WETU – ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana ameongoza mazishi ya Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki yaliyofanyika kijijini kwao Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, dini na serikali pamoja na wananchi, ndugu na jamaa walihudhuria  katika mazishi hayo akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye amemuwakilisha Rais Dk. John Magufuli.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Brigedia Jenerali wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar Fadhil Omar Nondo, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,  Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mapema Rais Dk. Shein aliungana na viongozi wa dini, vyama vya siasa na Serikali, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika sala ya kumsalia Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki katika Msikiti Mushawar, Mwembeshauri, Mjini Unguja sala iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kahbi.

Mazishi ya Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki yalifanyika kwa taratibu zote za Kidini na Kijeshi ikiwa ni pamoja na kutolewa salamu za heshima, salamu za Kijeshi pamoja na kupigia mizinga 17 zoezi lililoongozwa na Gwaride chini ya kiongozi wake Himid Alawi Nguzo

Akisoma Wasfu wa Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki , Waziri Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed alisema kuwa Marehemu amezaliwa mwaka 1930 katika Kijiji cha Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kuwa marehemu amesoma elimu ya msingi hadi darasa la nane na baada ya kuhitimu masomo yake, alijiunga na Jeshi la Polisi  ambapo pia, alipata mafunzo kwa muda wa miezi minane huko Sotch Logosk, iliyokuwa USSR.

Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki kwa maelezo ya Waziri Aboud, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Watu 14 ya Chama cha Afro Shirazi (ASP) iliyoongoza Mapinduzi Matukufu ya Januari 12 mwaka 1964 chini ya uongozi wa Jemedari Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Pamoja na hilo pia alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi (MBM) Mwaka 1964 hadi mwaka 1984 ambapo pia, Marehemu amefanya kazi katika Jeshi la Polisi kwa muda wa miaka 14 akipitia ngazi mbali mbali kuanzia “Full Inspector, Acting Superintendent” mwaka 1964 hadi mwaka 1966 akawa “Full Superintendent.

Waziri Aboud alieleza kuwa Marehemu Ramadhan Haji Faki mnamo mwaka 1964 hadi mwaka 1966 alikuwa Kiongozi wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar,  na mwaka 1964 hadi mwaka 1977 Marehemu alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Umoja wa Vijana wa ASP na akawa mwanzilishi wa Kambi za Vijana Zanzibar.

Aidha, alieleza kuwa alikuwa Mwanachama Mtiifu wa Chama cha ASP hadi mwaka 1977 kilipozaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa na kadi nambari 000061 ya CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles