27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara yatoa mafunzo kuikabili corona

MWANDISHI WETU – ARUSHA

WIZARA ya Afya kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii imeanza kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Ustawi wa Jamii pamoja na Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa unaoenezwa na virusi vya corona.

Akifungua mafunzo hayo kwa maofisa wa eilaya na kata zote za Mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki jijini hapa, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Hargeney Chitukuro, aliwataka maofisa hao kutumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kwa usahihi kuhusu maambukizi na namna ya kujikinga na ugonjwa wa corona bila hofu.

Alisema kuwa tangu ugonjwa huo ulipoingia mkoani Arusha, mafunzo mbalimbali yameshatolewa kwa wataalamu na kuwaelekeza namna ya kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga.

“Katika kipindi cha takribani wiki mbili tangu ugonjwa huu uingie tayari tumeshatoa mafunzo kwa wataalamu wa Afya 240 kwenye wilaya zetu na halmashauri zote. Kwa mafunzo haya tunatarajia kuwafikia wataalamu wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii zaidi ya 185,” alisema

Aliwaomba pia wadau wote kuelekeza nguvu zao kushirikiana na serikali katika kufanikisha ukarabati wa kituo cha dharura mkoani Arusha pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kujikinga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Patrick Golwike, alitoa wito kwa maofisa hao ili kuepusha msongamano watumie redio za jamii zilizopo kwenye maeneo yao kuelimisha jamii.

“Baadhi ya halmashauri zina televisheni zao pamoja na redio za kijamii. Vyombo hivi vikitumika vizuri kwenye kusambaza elimu ya kujikinga na virusi vya corona ili kuepuka msongamano, zitakuwa ni sehemu mojawapo ya kusaidia kufikisha ujumbe,” alisema

Akitoa mada kwa washiriki hao, Dk. Meshack Chinyuli kutoka Wizara ya Afya, kitengo cha Elimu kwa Umma amewasisitiza kutumia takwimu sahihi zinazotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na hapa nchini ni Wizara ya Afya.

Awali akitoa lengo la mafunzo hayo kwa washiriki, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Zakia Mohamed alisema kuwa mafunzo hayo yatawajengea uelewa wa kufahamu njia za maambukizi, dalili zake na inapotokea mtu amepata dalili ni wajibu wa maafisa hao kuelekeza wapi pa kwenda kupata huduma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles