23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein aelezea mafanikio ya Serikali yake

Na MWANDISHI WETU – PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 visiwani hapo umeongezeka na kufikia Sh bilioni 688.7 huku kasi ya ukuaji wa uchumi ikiwa ni asilimia 7.7.

Kauli hiyo aliitoa jana katika Uwanja wa Gombani Pemba, Mkoa wa Kusini Pemba wakati wa kilele cha sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanywa Januari 12, 1964.

Dk. Shein alisema Sh bilioni 688.7 zilikusanywa mwaka 2017/2018 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) ikilinganishwa na Sh bilioni 521.8 zilizokusanywa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Alisema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la Sh bilioni 166.9 sawa na asilimia 32 na yameiwezesha Serikali kutekeleza mipango ya kuinua uchumi na kuwasogezea wananchi huduma za kijamii.

Pia alisema kasi ya ukuaji uchumi ilikua kwa asilimia 7.7 mwaka juzi ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2016, huku pato la mtu binafisi likiongezeka na kufikia Sh milioni 2.1.

Alisema mfumko wa bei umeendelea kudhibitiwa katika tarakimu moja kwa mwaka jana na kasi yake imefikia asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka juzi.

VIWANDA

Kuhusu viwanda, alisema Serikali inaimarisha uchumi wake ambao mchango wake katika Pato la Taifa umefikia Sh bilioni 631.6 kutoka Sh bilioni 524 sawa na asilimia 19.2.

“Ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa viwanda. Katika mwaka 2018 Serikali imekamilisha sera yake ya mapinduzi ya viwanda ambayo itaanza kutumika hivi karibuni.

“Katika kusimamia na kuendeleza viwanda vidogo vidogo na vya kati, Serikali imeanzisha wakala wake maalumu wa kuendeleza viwanda hivyo na vya kati inayoitwa SMIDA (Small and Medium Industries Development Agency),” alisema.

Pia alisema tayari maeneo maalumu yametengwa kujenga viwanda hivyo katika kila wilaya.

Kuhusu kilimo cha mwani, alisema mpango umekamilika wa kuanzisha kiwanda cha kuzalisha mwani kitakachoendeshwa kwa ubia na wataalamu kutoka Indonesia mwaka 2019-2020.

Dk. Shein alisema katika kipindi cha mwaka jana, jumla ya bidhaa za zao hilo zenye thamani ya Sh bilioni 54.19 zilisafirishwa kwenda nje ya nchi ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 145.76 zilizosafirishwa mwaka juzi.


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (katikati), Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (wa tatu kushoto), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto)
na viongozi wengine wakifuatilia sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar jana.

BIASHARA

Akizungumzia biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, alisema bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 17.21 zilisafirishwa kutoka visiwani hapa huku bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 232.59 ziliingizwa kutoka Bara kwa mwaka jana.

Mbali na hilo, pia alisema kwa miaka saba mfululizo Serikali inatekeleza sera ya kumlipa mkulima kiwango cha asilimia 80 ya bei ya karafuu katika soko la dunia sawa na Sh 14,000 kwa kilo ya karafuu kavu.

“Katika mwaka 2017-2018, jumla ya tani 8,572 za karafuu zenye thamani ya Sh bilioni 119.5 zilinunuliwa kutoka kwa wakulima wa Unguja na Pemba,” alisema.

Alisema tani nyingine 7,464 za karafuu zenye thamani ya Sh bilioni 131.955 ziliuzwa nje ya Zanzibar ikilinganishwa na tani 2,253 zenye thamani ya Sh bilioni 38 zilizouzwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

UTALII

Dk. Shein alisema sekta ya utalii inaimarika kila mwaka na idadi yao inaongezeka.

Alisema mwaka jana jumla ya watalii 520,809 waliwasili Zanzibar ikilinganishwa na 433,116 waliowasili mwaka juzi ikiwa ni ongezeko la watalii 87,693 sawa na asilimia 20.2.

Dk. Shein alisema lengo la Serikali la kufikia watalii 500,000 kwa mwaka ifikapo 2020 limefikiwa kabla ya wakati huo.

Alisema mwaka jana Serikali ilifanya maonesho ya kitalii ya kimataifa yaliyohudhuriwa na watu 4,022 kutoka ndani na nje ya nchi na kutokana na tija yatafanyika visiwani hapa kila mwaka.

UDHALILISHAJI WANAWAKE, WATOTO

 Dk. Shein alisema bado udhalilishaji wa wanawake na watoto unaendelea, na mwaka jana yaliripotiwa matukio 1,091 katika taasisi za sheria.

Alisema mpango wa miaka mitano wa kupambamba na vitendo hivyo uliozinduliwa Julai, juzi unaendelea kutekelezwa.

MAHAKAMA

Dk. Shein alisema shughuli za mahakama katika ngazi mbalimbali zimeimarishwa huku usikilizwaji wa kesi ukiongezeka baada ya Serikali kuongeza idadi ya majaji na mahakimu.

Alisema mwaka 2017/2018 kesi 8,912 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali za Unguja na Pemba, huku 6,816 zikitolewa uamuzi ikilinganishwa na kesi 6,945 zilizofunguliwa mwaka 2016/2017 ambako 5,854 zilitolewa uamuzi ikiwa ni ongezeko la kesi 856 zilizotolewa uamuzi kwa mwaka 2017-18 sawa na asilimia 15.4.

“Sh bilioni tano zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 ili kujenga jengo jipya la Mahakama Kuu ya Zanzibar pamoja na Chuo cha Sheria,” alisema.

BARAZA LA WAWAKILISHI

Dk. Shein alisema Baraza la Wawakilishi limeweza kukaa vikao vyake vinne vya kila mwaka huku jumla ya miswada 15 ikitungwa na kuwa sheria kati ya Januari hadi Desemba mwaka jana ikilinganishwa na miswada 14 kwa mwaka juzi.

Alisema mwaka jana, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ilipokea malalamiko 209 ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi ikilinganishwa na malalamiko 187 ya mwaka juzi.

USALAMA

Dk. Shein alisema kwa lengo la kuimarisha usalama wa wananchi, wageni na mali zao, Serikali ilianzisha mradi wa Amka Salama unaosimamiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na idara maalumu za SMZ uliozinduliwa Oktoba, mwaka jana.

Alisema mradi huo uligharimu Dola za Marekani milioni 28.95 kwa kununua vifaa mbalimbali vya mawasiliano, magari, pikipiki ambazo ni fedha za Serikali, ulifunga kamera 877za CCTV katika Mji Mkongwe, bandarini na uwanja wa ndege pamoja na maeneo mengine ya mji.

“Sehemu ya pili ya mradi huo unaohusika na uokozi na uzamiaji, uliozinduliwa Januari 3, mwaka huu umegharimu Dola 7,000.2 za Marekani ukijumlisha ujenzi wa vituo vitatu vya uokozi na uzamiaji, vifaa vya uokozi na boti za kisasa mpya,” alisema.

AJIRA

Kuhusu ajira, alisema katika juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupambana na tatizo la ajira, Serikali iliimarisha Mfuko wa Uwezeshaji na mwaka jana mikopo 851 yenye thamani ya Sh milioni 685 ilitolewa kwa wajasiriamali wa Unguja na Pemba.

Alisema katika kipindi hicho, vijana 2,338 wameajiriwa katika sekta binafsi  ikilinganishwa na 1,644 walioajiriwa mwaka juzi huku Serikali ikiajiri watu 2,968 kwa mwaka jana wakiwamo waliomaliza elimu ya sekondari na ile ya juu.

Kwa upande wa huduma za umeme, alisema hadi kufikia Desemba, mwaka jana Serikali ilifikisha huduma za umeme katika vijiji 2,694 kati ya 3,259 vya Unguja na Pemba ikiwa ni sawa na asilimia 83 na kati ya hivyo, 55 vilipatiwa umeme mwaka jana.

Pia alisema utafiti mwingine wa mafuta na gesi asilia ulianza kufanyika Novemba, mwaka jana katika maeneo yenye maji madogo huko Pemba na baadaye utaendelea kwa upande wa Unguja.

Alisema Kampuni ya Rakgas iliidhinishwa rasmi kufanya kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Pemba-Zanzibar.

Pia katika hatua za kuliimarisha Shirika la Meli la Zanzibar, alisema Serikali inajenga meli mpya ya mafuta itakayojulikana kwa jina la MT Ukombozi II ambayo ujenzi wake unafanywa na Kampuni ya Damen Shipyard ya Uholanzi na inatarajiwa kuwasili miezi michache ijayo.

Aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza na kuimarisha muungano uliopo.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa na viongozi wengine.

Dk. Shein alisema Rais Dk. John Magufuli alishindwa kuhudhuria sherehe hizo kutokana na kuwa na dharura.

Pia alisema si Dk. Magufuli peke yake aliyetoa udhuru, bali Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, nao pia hawakufika kutokana na dharura.

“Ndugu wananchi, napenda niwajulishe kuwa leo (jana) katika sherehe hizi, hayupo hapa pamoja nasi Rais Magufuli kwa sababu ya dharura aliyonayo. Hivyo hakuweza kuhudhuria ametaka niwape taarifa hiyo, naye anatuombea sisi kila la kheri kwenye sherehe hizi ambazo zina umuhimu wa pekee katika nchi yetu. Amenieleza yuko pamoja nasi kama kawaida,” alisema Dk. Shein.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles